Habari za Punde

Mama Maryam Mwinyi akutana na uongozi wa UWT

MLEZI wa Jumuiya ya CCM ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mariam ameipongeza jumuiya hiyo kwa kuwa na viongozi imara wenye dira ya maemdeleo endelevu na mioyo ya kujituma kuwapambania wanawake wa Tanzania na vijana.

Mama Mariam Mwinyi alitoa pongezi hizo alipozungumza na uongozi wa UWT ukiongozwa na Katibu mkuu wake, Jokate Mwegelo na ujumbe wake waliofika Ikulu ya Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), aliueleza uongozi huo kuhusu taasisi ya (ZMBF) inavyounga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sera yake ya Uchumi wa Buluu unaoshajihisha wananchi zaidi kuzitumia fursa za bahari kuleta maendeleo ya kiuchumi na kujiongezea kipato kupitia kilimo cha mwani.

Alisema, taasisi ya ZMBF imewawezesha kiuchumi wanawake na vijana hasa wakulima wa mwani baada ya kuwaweka pamoja kinamama wa Unguja na Pemba kwa lengo la kuwapa mikopo nafuu ili kuendeleza zao hilo linaloongoza kulimwa Zanzibar na kuwa nchi ya kwanza Afrika na ya pili kwa dunia nzima ikiongozwa na Ufilipino.

Alisema, kilimo cha mwani Zanzibar kinakamata asilimia tatu ya pato la taifa baada ya Utalii unaochangia asilimia 30 ya pato la taifa na kilimo cha Karafuu.

Alisema. mbali na fursa nyingi zinazotokana na zao la mwani ikiwemo kutumika kama, chakula, dawa, vipodozi, virutibisho vya mwili na kuongeza lishe mwilini pia zao hilo linaimarisha sana afya za mama wajawazito.

Mbali na shughuli nyingi zinazofanywa na taasisi ya ZMBF ikiwemo udhalilishaji masuala ya wanawake, vijana na watoto pia kuendeleza Kampeni yake ya “Mariam Mwinyi Walkathon” ambayo imewagusa wananchi wengi na kuwafuata walipo ili uchunguza afya zao na kufanya matibabu, Mama Mariam Mwinyi aliwaeleza UWT kwamba lengo la kampeni hiyo ni utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwafikishia huduma bora za matibabu wananchi wake.

Pia Mama Mariam Mwinyi alimpongeza Katibu Mkuu Jokate Mwegelo kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni na kukipongeza chama cha CCM kwa kufanya uteuzi sahihi.

Vile vile, Mama Mariam Mwinyi alipongeza hatua ya UWT kupongeza juhudi za miaka mitatu ya uongozi wa Rais D.k. Hussein Ali Mwinyi nakueleza wanafanya uamuzi sahihi.

Naye, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Wanawake Tanzania, Jokate Mwegelo alipongeza hatua ya Mama Mariam Mwinyi kujikurubisha kwa wananchi na kushirikiana nao kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuishajihisha jamii kufanya mazoezi kwa kuungana nao pamoja na kuimarisha afya zao ili kuepukana na maradhi mbalimbali ya kuambukiza na yasiyoyakuambukiza.

Alisema, UWT inabeba agenda zote zinzazowahusu wananwake bila kujali tofauti zao kisiasa, dini, ukabila, rangi wala kipato na uchumi wao.

Katibu Joketi pia alipongeza mabadiliko ya maendeleo yanayofanywa na Rais Dk. Mwinyi kwa kipindi kifupi Zanzibar imekua na maendeleo makubwa na kusifu jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa kwenye suala zima la kuimarisha miundombinu ya barabara na mawasiliano na huduma za jamii ikiwemo afya, maji safi na elimu.

Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, hivi karibuni ilimteua Katibu Mkuu Jokate Mwegelo kushika wadhifa huo, awali aliwahi kushika nafasi mbalimbali za chama na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Pwani, Temeke na Korogwe Mkoani Tanga.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.