Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Afungua Mkutano Mkuu wa Skaut Tanzania


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussen Ali Mwinyi amesema Serikali zote mbili zinatambua mchango mkubwa wa Chama cha Skauti Tanzania kwa namna wanavyojinasibisha  na Serikali kwa kufanya mambo makubwa na mazuri katika jamii hususan katika kundi kubwa la vijana.

Ameyasema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzani uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi Zanzibar.

Amesema kuwa Chama cha Skauti kinafanya kazi kubwa ya kuwajengea uwezo vijana kuweza  kujitambua kuwa na maadili mema na kuwakuza kiuzalendo ili kutengeneza Taifa ambalo litaendelea kuwa na viongozi bora ambao watasukuma mbele maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa Viongozi wa Serikali zote mbili wanaridhishwa na Chama cha Skauti kwani  ni chama pekee ambacho ni tofauti na  Asasi nyengine hapa nchini kwa kulea vijana kwa kuzingatia misingi, kanuni na taratibu maalumu kupitia elimu isiyo rasmi inayozingatia tunu za kizalendo na maadili yanayoendana na Taifa letu.

Aidha Rais Dkt Mwinyi amekitaka Chama Cha Skauti Tanzania kuendelea kuwasimamia vijana kwa kuwapa elimu juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamiii kwa kuitumia katika kujielimisha ili kukuza uwelewano kwani matumizi mabaya ya mitandao yanaweza kupelekea kushindwa kufikia malengo katika maisha yao ya baadae.

Sambamba na hayo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha Skuli na Vyuo vinakuwa na Skauti na Walimu wanaopewa mafunzo bora ya kuendesha uskauti katika maeneo yao.

Dkt. Mwinyi  ametowa wito kwa  Viongozi wa Skauti nchini kuzingatia  utekelezaji wa Sera ya Usalama dhidi ya madhara ya ya unyanyasaji (Safe From Harm Policy) na kuhakikisha vipengele vitakavyoingzwa katika katiba ya Skauti vinaendana na matakwa ya Sera hiyo ili kuendana na agizo lililotolewa katika Mkutano Mkuu wa Skauti  Duniani uliofanyika mwaka 2021ambao ulisisitiza utekelezwaji wa Sera hiyo.

Nae  Raisi wa chama cha Skauti Tanzania ambae pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknoloji  Mhe. Profesa Adolf Mkenda amesema miongoni mwa Taasisi muhimu nchini ni Skauti taasisis ambayo inafanya kazi ya kuwalea vijana katika malezi yaliyo bora, kuwaweka pamoja katika kufanya maamuzi pamoja na kuwafundisha uzalendo wa kulitumikia Taifa lao.

Mhe. Mkenda amesema Mkutano Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania utatoa fursa ya kufanya mchakato wa upatikanaji wa katiba ambayo ndio muhimili Mkuu wa chama hicho  itakayosaidia kutatua changamoto zinazowakabili sambamba na kusimamia malengo ya maendeleo ya Skauti Tanzania.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ambae pia ni makamo wa Rais wa Skauti Tanzania Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema uwamuzi wa kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Skauti hapa Zanzibar sio tu kudumisha Muungano bali ni utayari wa kuwasaidi Viongozi wakuu wa nchi katika kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora wa baadae.

Amesema kuwa ni dhahiri faida ya uwepo wa Skauti nchini inaonekana kwani vijana wanaopitia katika chama hicho wanalelewa katika maadili mema ambayo yanawasaidia katika jamii na katika Ujenzi wa Taifa letu.

Mapema  Skauti Mkuu wa Tanzania Ndg Rashid Kassim Chapa  amesema chama cha skaut ni hazina kubwa ambayo ni chimbuko kuu la viongozi  wengi wenye uzalendo na nchi yao.

Amesema licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Chama cha Skauti Tanzania lakini bado  kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na uhaba wa maeneo ya makambi kwa ajili ya kuwapatia mafunzo Skauti na uhaba wa Ofisi za kufanyia kazi kwa ngazi za Mikoa na Wilaya.

Mkutano huo Mkuu wa siku Moja (1) wa Chama cha Skauti utajikita katika kuangalia mchakato wa kutengeneza katiba mpya ya Skauti, utunzaji wa mazingira na utawala bora kwa kuweka mikakati imara itakayosaidia kuboresha Uskauti Tanzania.

Imetolewa na kitengo cha habari (OMPR)

Leo terehe 19.12.2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.