Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 18, 2023 kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa
Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania inatanufaika na fedha za miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa kauli hiyo leo Desemba 18, 2023
jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 28 wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai, Umoja
wa Falme za Kiarabu.
Dkt. Jafo amesema kupitia mkutano huo
uliofanyika Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 Tanzania inatarajia kunufaika na
teknolojia na Programu ya Afrika ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na afya.
Amesema kuwa programu hiyo inaunga mkono
juhudi za Serikali za kuhamasisha kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo
yanasababishwa na ukataji wa miti.
Pamoja na manufaa hayo, Waziri Jafo amesema
kuwa pia utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha uhimili katika katika sekta ya
maji, misitu na bahari ambayo ni mojawapo ya rasilimali muhimu kwa uchumi wa
buluu.
“Katika Mkutano wa COP28 wafanyabiashara na
wawekezaji wa Tanzania walikutana na wenzao kutoka nje ya nchi na kujadiliana
kuhusu fursa za uwekezaji kwenye eneo la mabadiliko ya tabianchi ambapo jumla
ya taasisi na kampuni zaidi ya 56 zimeonesha nia ya kuwekeza nchini kwa
kushirikiana na sekta binafsi nchini,” amesema Dkt. Jafo.
Halikadhalika amebainisha kuwa katika
kuwezesha ushiriki kikamilifu, Tanzania iliandaa msimamo wa taifa uliosaidia
kuongoza dira ya ushirikiri na majadiliano ya wajumbe wa Tanzania, ulioandaliwa
kwa ushirikianao na wadau mbalimbali.
Aidha, Dkt. Jafo ameongeza kuwa ujumbe wa Tanzania
ulikuwa ni ‘Kuimarisha Hatua za Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu’, iliyolenga kuchochea
hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa na kilimo endelevu na
kutumia vizuri fursa za uchumi wa buluu.
Hivyo, Mkutano wa 29 (COP 29) umepangwa kufanyika nchini Azerbaijan kuanzia Novemba 11 hadi 22, wakati COP30 itafanyika nchini Brazil kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025.
No comments:
Post a Comment