HOTUBA
YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN
ALI MWINYI, KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 60 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
TAREHE: 11 JANUARI, 2024
Assalamu Aleikum
Ndugu Wananchi,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
kwa kutupa uhai na afya njema na kutuwezesha kufikia siku ya leo, tukiwa katika
mkesha wa Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi, tuna wajibu pia wa kuwakumbuka Waasisi wetu chini ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, viongozi na wananchi wenzetu waliotangulia mbele ya haki, ambao waliitumikia nchi yetu kwa moyo, ujasiri na uzalendo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi. Na wale walio hai, Mola awape afya njema na umri mrefu tuendelee kushirikiana nao katika kujiletea maendeleo.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wote
kwa kujitokeza kwa wingi katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa katika
Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi. Ni matarajio yangu kuwa na kesho siku ya
kilele, mtajitokeza tena kwa wingi katika uwanja wa Amani ili kufanikisha
sherehe zetu.
Tofauti na mara nyengine zote safari hii
sherehe yetu itafanyika mchana ili kutoa fursa kwa waumini wa Dini ya Kiislamu
kupata nafasi ya kutekeleza ibada ya sala ya Ijumaa.
Mara hii tulikuwa na miradi iliyozinduliwa 65 na miradi 45 imeekewa mawe ya msingi. Hii ni idadi kubwa sana ya miradi ambayo hatujawahi kuifikia katika kipindi cha sherehe kama hizi. Vile vile, tumeandaa matukio makuu maalum na sherehe za aina yake ambazo kilele chake kitafanyika katika uwanja wa Amani. Kadhalika, tuna ujio wa baadhi ya wageni mashuhuri tutakao kuwa nao katika maadhimisho yetu haya.
Ndugu Wananchi,
Mafanikio tuliyoyapata miaka 60 tokea
Mapinduzi ya mwaka 1964, yametokana na uongozi thabiti wa Waasisi wa Taifa letu
na viongozi wote wa awamu zilizotangulia kwa ushirikiano na uzalendo kati yao
na nyinyi wananchi. Serikali ya Awamu ya Nane tokea ilipoingia madarakani miaka
mitatu iliopita, inayaendeleza mafanikio hayo na kufanya juhudi za kuhakikisha
Zanzibar inazidi kupiga hatua za maendeleo
katika sekta zote na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
Nilipoingia madarakani mwaka 2020, nilieleza dhamira yangu ya kuunganisha Malengo ya Mapinduzi na uchumi, nikilenga kuimarisha jitihada za kukuza uchumi ili kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar. Lengo la Serikali ninayoiongoza ni kuendeleza umoja, mshikamano na maridhiano ili kila Mzanzibari apate fursa ya kuchangia maendeleo na kunufaika na matunda ya Mapinduzi kwa misingi ya usawa. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika kuifikia dhamira hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane.
Ndugu
Wananchi,
Katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka
mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, tunafurahia mafanikio tuliyo nayo katika
kudumisha na kuendeleza Amani, Umoja na Mshikamano. Misingi hii muhimu imetuwezesha
kupiga hatua katika maendeleo ya uchumi, ujenzi wa miundombinu, kuimarisha
huduma za jamii, biashara na kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya
nchi.
Natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM kwa ushirikiano mkubwa anaonipa. Vile vile, nawashukuru viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na asasi za kijamii, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote kwa kunipa ushirikiano na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini kwa faida ya kizazi cha sasa cha baadae. Nawahakikishia wananchi na wageni wote wanaotutembelea kwamba nchi yetu ipo salama na kwamba Serikali zetu zote mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria katika kulinda amani, utulivu na usalama wa mali zao.
Ndugu Wananchi.
Katika hotuba yangu hii ya kuadhimisha miaka
60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na miaka mitatu Serikali ya Awamu ya Nane,
nitaelezea kwa muhtasari mafanikio, changamoto na mipango yetu ya utekelezaji
wa majukumu ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Serikali iliwapa
jukumu mawaziri wote kuelezea kwa kina kupitia vyombo vya habari, mafanikio,
changamoto na mipango ya kila wizara ili wananchi wafahamu utendaji wa Serikali
yao. Nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutekeleza kwa mafanikio agizo hilo.
Ndugu Wananchi
Juhudi zinazochukuliwa na Serikali
zimewezesha uchumi wetu kuzidi kuimarika. Thamani ya Pato halisi la Taifa (GDP
at constant Price) imeongezeka kutoka TZS.
Trilioni 3.116 kwa mwaka 2020 na kufikia thamani ya TZS. Trilioni 3.499 mwaka 2022. Vile vile ukusanyaji wa mapato
umeongezeka kufikia TZS. Trilioni 1.4 mwaka
2022/2023 kutoka TZS. Bilioni 790.48 mwaka
2020/2021, sawa na ongezeko la asimilia 56.4.
Aidha, kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2022 imefikia wastani wa asilimi 6.8 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020. Kiwango cha ukuaji
wa uchumi wetu ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea.
Kukuwa kwa uchumi wetu kumetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwa kutekelezwa miradi ya Maendeleo ya kipaumbele ikiwemo miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, huduma za maji safi na salama, uimarishaji wa huduma za nishati ya umeme, masoko na kuimarika kwa sekta ya huduma kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii. Pato la mtu binafsi nalo limeongezeka kutoka USD 1,099 sawa na TZS. Milioni 2.5 mwaka 2020 na kufikia USD 1,230 sawa na TZS. Milioni 2.8 mwaka 2022. Aidha, jitihada zilizochukuliwa na Serikali zimeweza kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kuendelea kuwa katika tarakimu moja. Kwa mwaka 2023 mfumko wa bei ulikuwa ni wa wastani wa asilimia 6.8 hali inayomuhakikishia mwananchi kupata mahitaji ya lazima.
Ndugu Wananchi
Serikali za awamu zote zilizopita baada ya
Mapinduzi zilichukuwa juhudi za uwekezaji kwa ujenzi wa miundombinu, majengo ya
Ofisi, huduma na maakazi, viwanda na kuwakaribisha wawekezaji kuzitumia fursa
na rasilimali zilizopo nchini katika kuchangia ukuaji wa uchumi.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na Miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya
Nane tumeshuhudia mafanikio makubwa katika jitihada zetu za kuvutia wawekezaji. Kasi ya uwekezaji nchini imeongezeka ambapo
jumla ya miradi 296 yenye thamani ya USD.
Bilioni 4.5 imeidhinishwa. Miradi hiyo inakadiriwa kutoa ajira zipatazo 17,479 ikihusisha uwekezaji katika
visiwa vidogo 16 wenye thamani ya USD. Milioni
377.5, ujenzi wa hoteli za kitalii 112, viwanda 36, biashara ya majengo 56
na miradi mingine ya kiuchumi.
Mafanikio haya yametokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ikiwemo uimarishaji wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo sasa wawekezaji wanaweza kupata huduma zote za uwekezaji katika kituo kimoja (One Stop Center) ndani ya masaa 24. Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa zilizopo katika maeneo ya bandari jumuishi ya Mangapwani na ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, maji na umeme katika maeneo ya uwekezaji.
Ndugu Wananchi
Kwa kuzingatia umuhimu wa biashara kwa Zanzibar, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbali mbali kuimarisha mazingira ya
ufanyaji wa biashara. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na mitatu ya
Serikali ya Awamu ya Nane, sekta ya biashara ya usafirishaji na uingizaji
bidhaa kwa ujumla inaendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022 Zanzibar imefanya
biashara yenye thamani ya TZS. Trilioni 1.4 ukilinganisha na TZS.
Bilioni 913.1 kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 57.6.
Zanzibar imesafirisha nje bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 180.4 kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 174.7 ikilinganishwa na usafirishaji wa bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 65.7 kwa mwaka 2020. Kwa mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha tani 6,452.8 za karafuu yenye thamani ya TZS. Bilioni 118.3 ikilinganishwa na tani 3,506.8 zilizosafirishwa mwaka 2020, zenye thamani ya TZS. Bilioni 38.37 sawa na ongezeka la fedha la asilimia 208.1. Kwa upande wa mwani Zanzibar imesafirisha Tani 13,972.5 zenye thamani ya TZS. Bilioni 16.0 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na tani 11,382.6 wenye thamani ya TZS. Bilioni 11.7 kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 36.8.
Kuhusu biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 37.64 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 15.03 zilizosafirishwa mwaka 2020. Kwa upande wa uagiziaji katika kipindi cha mwaka 2022, Zanzibar imeagizia bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 375.80 kutoka Tanzania Bara ikilinganishwa na uagiziaji wa bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 243.81 kwa mwaka 2020.
Ndugu Wananchi
Kwa
madhumuni ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi, Serikali imechukua hatua za kuimarisha
uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kupambana na umaskini. Serikali imepata
mafanikio katika uimarishaji wa vikundi vya ushirika ambapo jumla ya vikundi
1,546 vya ushirika vimesajiliwa. Idadi hiyo imewezesha kufikia vikundi 3,662
vya ushirika vilivyosajiliwa nchini. Kupitia fedha za Ahuweni ya UVIKO - 19, Serikali
imetoa jumla ya TZS Bilioni 60.
Fedha hizi zinajumuisha TZS. Bilioni 29
zilizotolewa kwa ajili ya sekta za Uchumi wa Buluu, TZS Bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa Masoko na TZS. Bilioni 15 kwa ajili ya Programu ya Inuka yenye lengo la kutoa mikopo
kwa wajasiriamali na wafanyabiashara.
Programu ya Inuka ilianza na mtaji wa TZS. Bilioni 15.0. Hadi sasa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 22.4 imeshatolewa kupitia programu hii. Ongezeko la thamani la mikopo hiyo limetokana na fedha za marejesho ambazo zinaendelea kutolewa mikopo mipya (Revolving Fund). Mikopo hiyo imewezesha kuzalisha ajira za moja kwa moja (direct employment) kwa Wananchi 43,360. Aidha, programu ya Khalifa Fund imetoa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 2.10 kwa miradi 18 ya wananchi. Kadhalika, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi jumla ya TZS Milioni 852.17 zimetolewa kwa wananchi.
Kupitia Programu ya Mikopo kwa Makundi Maalum, hadi sasa Serikali imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS. Bilioni 1.9 kutoka Halmashauri za Wilaya. Fedha hizi zimelengwa kutumika kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Ndugu Wananchi
Katika
kuhakikisha suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linapata mafanikio, Ujenzi wa
miundombinu umezingatiwa ambapo vituo viwili vya kusarifu asali vinavyogharimu TZS. Milioni 529.29 vimejengwa Unguja
na Pemba. Aidha, ujenzi wa kituo cha
mafunzo ya usarifu mazao utakaogharimu USD.
Milioni 1.29 umeanza kwa matayarisho ya awali.
Kadhalika, wajasiriamali wamepatiwa vifaa vya uzalishaji wa asali ikiwemo Mizinga yenye thamani ya TZS. Milioni 459.98, vifaa vya nyuki vyenye thamani ya TZS Milioni 194.34, Vifaa vya maabara vyenye thamani ya TZS Milioni 34.40 na Pikipiki 9 zenye thamani ya TZS Milioni 35.91.
Serikali pia, imeanzisha Wakala ili kuimarisha usimamizi wa utoaji wa Mikopo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB. Vile vile, mafunzo yanaendelea kutolewa kwa wajasiriamali ili kuwajengea uwezo zaidi ambapo wajasiriamali 2,225 wameshapatiwa mafunzo hayo kwa kipindi hiki.
Jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi cha miaka mitatu, zimewezesha kupatikana kwa jumla ya ajira 187,651. Idadi hiyo imevuka malengo ya ajira 180,000 kwa miaka mitatu, sawa na ongezeko la asilimia 104.3
Ndugu Wananchi,
Serikali
imezingatia haja ya kuwapatia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo mazingira
bora ya kufanyia kazi zao. Ujenzi wa vituo 14 vya wajasiriamali na
wafanyabiashara wadogo vilivyogharimu TZS
Bilioni 16.03 vimejengwa Unguja na Pemba ambapo baadhi yake vimeanza
kutumika. Vile vile, jumla ya masoko 10 yamejengwa kwenye Wilaya 6 yenye
thamani ya TZS. Bilioni 4.93. Aidha,
ujenzi wa masoko makubwa ya kisasa unaogharimu TZS. Bilioni 102.41 unaendelea katika maeneo ya Mwanakwerekwe,
Jumbi na Chuini. Ni matumaini yetu kuwa masoko haya yatakamilika mwaka huu 2024
na kuanza kutumika.
Hadi kufikia tarehe 20 Disemba, 2023 jumla ya wajasiriamali 7,227 wamesajiliwa na kupatiwa vitambulisho katika Serikali za Mitaa Unguja na Pemba. Vile vile, mafanikio yamepatikana katika ukusanyaji wa mapato kwa Serikali za Mitaa, ambapo ukusanyaji wa mapato umeongezeka kwa asilimia 26 kutoka TZS Bilioni 15.24 zilizokusanywa mwaka 2020 hadi kufikia TZS Bilioni 20.71 mwaka 2023.
Ndugu Wananchi
Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Nane imekuja
na dhana ya Uchumi wa Buluu unaotilia mkazo matumizi ya rasilimali za bahari na
shughuli nyengine za kiuchumi zinazohusiana na bahari. Tunapoadhimisha miaka 60
ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio
yamepatikana katika sekta kuu za uchumi wa buluu ambazo ni utalii, uvuvi na
kilimo cha mwani, bandari, mafuta na gesi asilia na biashara inayohusiana na
usafiri wa majini.
Kuhusu utalii, ni sekta iliyopewa mazingatio katika kuleta fedha za kigeni na ajira katika awamu zote za Serikali baada ya Mapinduzi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi. Juhudi mbali mbali zimefanywa na viongozi wa awamu zilizopita ili kuongeza michango ya sekta hii katika Pato la Taifa pamoja na upatikanaji wa ajira. Sekta ya utalii imeendelea kupata mafanikio makubwa. Idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia 143.6, kutoka watalii 260,644 mwaka 2020 hadi 638,498 mwaka 2023. baada ya UVIKO - 19.
Miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa idadi ya watalii ni ongezeko la idadi ya ndege za kimataifa zilizotua nchini kutoka 4,253 mwaka 2020 hadi 10,548 mwaka 2022 kulikochochewa na uimarishaji wa huduma ya kiwanja chetu cha ndege cha AAKIA. Aidha, ongezeko la hoteli za daraja la juu nchini kumechangia kuimarisha sekta ya utalii kwani kumevutia kutembelewa na wageni wengi. Katika kipindi hiki, idadi ya miradi ya utalii imeongezeka kutoka 620 mwaka 2020 hadi miradi 709 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 15.
Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi,
Zanzibar haikuwa na mipango madhubuti ya kuimarisha uvuvi na mazao mengine ya
bahari licha ya nchi hii kubarikiwa rasilimali hiyo kila upande. Katika kipindi
chote baada ya Mapinduzi, jitihada zimefanywa na Serikali kuimarisha sekta hii
hasa kwa kuwashajiisha wavuvi wadogo wadogo wanaoishi pembezoni mwa mwambao wa
bahari. Serikali ya Awamu ya Nane katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa
buluu, imeongeza juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani.
Mafanikio yameanza kupatikana katika dhamira hiyo baada ya Serikali kuwapatia wananchi
vifaa, fedha za mitaji, mafunzo na miundombinu ikiwemo ujenzi wa soko la kisasa
la samaki Malindi na kiwanda cha kusarifu bidhaa za mwani Chamanangwe Mkoa wa
Kaskazini Pemba. Serikali pia imeanza kuvutia uwekezaji katika Mpango mkakati
wa Uchumi wa Buluu ili kuwezesha kuongezeka kwa miradi ya maendeleo.
Kiwango cha uzalishaji wa samaki kwa
mwaka kimeongezeka kutoka Tani 38,107
mwaka 2020 zilizokuwa na thamani ya TZS.
Bilioni 205.4 hadi kufikia Tani 80,085 kwa mwaka 2023 zenye
thamani ya TZS. Bilioni 569.08. Aidha,
usafirishaji wa dagaa umeongezeka kufikia Tani 10,695 zenye thamani ya TZS. Bilioni 39.1 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka
2020 ambao ulikuwa Tani 3,500 zenye thamani ya TZS. Bilioni 12.3. Mafanikio
hayo yamewezesha kuongezeka kwa pato la Taifa katika sekta ya uvuvi kutoka asilimia 4.5 na kufikia asilimia 6.32
mwaka 2023.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu
zao la mwani, Selikali ilitoa jumla ya boti 500 pamoja na kamba na taitai kwa wakulima
wa mwani 5,000. Jitihada hizi zimechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mwani
kutoka tani 8,785 zenye thamani ya TZS. Bilioni 5.38 mwaka 2020 na kufikia tani 16,653 zenye thamani ya TZS. Bilioni 16.35 kwa mwaka 2023. Pia, katika kuendeleza mnyororo wa thamani
wa zao la mwani, tumekamilisha ujenzi wa Kiwanda cha kusarifu mwani cha
Chamanangwe Pemba kwa awamu ya kwanza. Kwa ushirikiano na wadau wetu wa
maendeleo kutoka Korea, Kiwanda chengine cha pili kikubwa cha kutengeneza
bidhaa za mwani kitajengwa Pemba. Vilevile, viwanda vitatu vidogo vidogo vya
ujasiriamali wa wakulima wa mwani vitajengwa kwa Mikoa ya Unguja.
Kuanzishwa
kwa Kampuni ya Mwani ya Serikali, kumeongeza ushindani katika ununuzi wa mwani
kutoka kwa wananchi. Hali hii imesababisha kuongezeka kwa bei ya mwani. Bei ya
mwani wa Spinosum imepanda kutoka TZS 600 kwa kilo hadi TZS. 1,000 kwa kilo. Mwani
wa Cottonii unauzwa kwa TZS. 2,200 kwa kilo kutoka TZS. 1,000. Ahadi ya
Serikali ni kufanya kila linalowezekana katika kuhakikisha bei hiyo inazidi kuongezeka
ili kumpa faida zaidi mkulima.
Ndugu Wananchi,
Serikali baada ya Mapinduzi ilianza kuchukua
hatua za kuimarisha huduma za bandari na usafiri wa majini kutokana na umuhimu
wake kwa uchumi wa visiwa kama ilivyo Zanzibar na kurahisisha huduma za
usafiri. Serikali, ilifanya upanuzi wa bandari zetu, ujenzi wa gati, ununuzi wa
vifaa na mashine mbali mbali pamoja na ujenzi wa majengo ya Ofisi na kuhudumia
abiria. Pia, Selikali ilinunua meli mpya na kuruhusu sekta binafsi kuanzisha
usafiri wa boti za mwendo wa kasi kwa madhumuni ya kuimarisha usafiri wa
majini.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi jitihada za kuimarisha bandari zetu na usafiri wa majini nazo zimepata mafanikio. Kwa upande wa bandari, Serikali ilifunga mkataba na Africa Global Logistic (AGL) inayomilikiwa na kampuni ya MSC, shirika lenye kumiliki meli za usafirishaji. Kampuni hii inahusika na uendeshaji wa bandari ya Malindi kwa kipindi cha miaka mitano na imesajiliwa kwa jina la Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT). Tayari Kampuni hii imeanza kazi ya kushughulikia meli za makontena pamoja na mizigo ili kuongeza ufanisi wa huduma za bandari ya Malindi.
Mafanikio ya hatua hiyo yameanza kupatikana ikiwemo kupunguza muda wa meli kukaa ukutani, wafanyabiashara kupata makontena yao ndani ya muda mfupi, kujengewa uwezo wafanyakazi na stahiki zao kuongezeka. Pia gharama za usafirishaji zimepungua, ulinzi na usalama bandarini umeimarika na mapato yameanza kuongezeka.
Aidha, utoaji wa huduma kwa wateja kupitia mifumo ya kidijitali umeimarishwa kwa kuweka mifumo na taratibu zilizo wazi zenye malengo ya kurahisisha kupata huduma bora kwa wadau (customer-oriented service). Utaratibu wa kuwa na bandari kavu umeanza ili kupunguza mrundikano wa makontena katika bandari ya Malindi. Serikali tayari imetoa eneo la Maruhubi kutumika kuhifadhia kontena. Vile vile kwa kushirikiana na wawekezaji Serikali imeanzisha bandari ya mizigo katika eneo la Fumba. Sambamba na hilo Serikali ipo mwishoni kukamilisha hatua zote muhimu za kuanza ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mwangapwani. Hatua za uwekaji wa miundombinu muhimu katika bandari ya Mangapwani zinaendelea ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko (Ring Road).
Mipango ya Serikali ni kuifanya bandari hiyo kuwa ndio lango kuu la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutoa huduma bora zenye ufanisi katika kuhifadhi na kusafirisha mizigo, matengenezo ya vyombo vya majini na kuwa kituo kikuu cha kutoa huduma ya mwanzo katika ukanda wa bahari ya hindi. Pamoja na hatua hiyo Serikali inadhamira ya kuzifanyia matengenezo makubwa bandari zote nchini ili zitowe huduma zilizo bora. Aidha, Serikali imetiliana saini na kampuni ya ZF DEVCO ya Uholanzi juu ya mradi wa ujenzi wa Bandari kubwa ya kisasa ya abiria katika eneo la Mpigaduri. Tumedhamiria kuikarabati bandari ya Malindi iwe kubwa zaidi ndani ya Afrika Mashariki ya kutoa huduma za abiria na kuruhusu meli kubwa za kitalii kuweza kufunga nanga Zanzibar.
Katika kuimarisha usafiri wa baharini, Serikali imeamua kuifanyia matengenezo meli ya Mapinduzi 2 chini ya wataalam kutoka Jamhuri ya Korea ya Kusini (South Korea) wakisaidiana na wahandisi wetu wa ndani ili kukabiliana na changamoto ya usafiri iliyopo hasa baina ya Unguja na Pemba. Nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati wenzetu wa sekta binafsi Kampuni Azam Marine na Zan Fast farries kwa mchango wao katika kusaidia kukabiliana na changamoto hii kwa kuimarisha usafiri kati ya bandari ya Unguja, Pemba, Dar es Salaam na Tanga.
Ndugu Wananchi,
Sekta ya mafuta na gesi asilia haikupewa
mazingatio kabla ya Mapinduzi. Kufuatia taarifa za kuwepo kwa rasimali hizo
hapa nchini, Serikali baada ya Mapinduzi katika awamu mbalimbali za uongozi
ilianza kuchukua hatua za kufanya tafiti zitakazowezesha kupatikana kwa mafuta
na gesi asilia hapa Zanzibar. Serikali ya Awamu ya Nane nayo inaendelea na
jitihada hizo. Serikali imekamilisha kazi ya ugawaji wa vitalu katika eneo la
baharini kupitia taarifa zilizokabidhiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mwezi Agosti 2022. Kazi hiyo imefanywa kwa kushirikiana na Kampuni ya
Kimataifa ya Schlumbeger ambapo vitalu 12 vimegaiwa katika eneo la baharini.
Aidha, katika mwezi Julai 2023, Serikali ilitangaza rasmi kufungua maeneo ya
uwekezaji kupitia vitalu vilivyogaiwa. Hatua hiyo ina lengo la kukuza sekta hii
kwa kuwakaribisha wawekezaji wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Ndugu Wananchi
Ujenzi wa miundombinu ni muhimu katika
kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya ustawi wa jamii. Katika
miaka 60 ya Mapinduzi jitihada mbali mbali zimefanywa na Serikali katika ujenzi
wa barabara na uimarishaji wa viwanja vya ndege.
Serikali ilianza ujenzi wa barabara
za lami na madaraja, shamba na mjini na kufanyiwa matengenezo kwa vipindi
tafauti pamoja na kujengwa mpya katika awamu mbali mbali za serikali kwa lengo
la kurahisisha usafiri. Serikali ya Awamu ya Nane nayo imeanza kwa mafanikio
kazi ya ujenzi wa barabara kuu KM 103.5, barabara za ndani mjini na vijijini KM
275 pamoja na ujenzi wa barabara za mjini KM 100 na madaraja ya juu mawili katika
Manispaa ya Mji wa Zanzibar. Miradi hii inatekelezwa
na Makampuni mbali mbali toka nje ya nchi.
Ndugu
Wananchi
Tunapoadhimisha miaka 60 ya
Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio makubwa
yamepatikana katika kuimarisha huduma za viwanja vya ndege na usafiri wa anga. Mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali kwenye
viwanja vya ndege na usafiri wa anga, yamewezesha Mapato ya Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege kuongezeka kutoka TZS.
Bilioni 11.6 mwaka 2019/2020 hadi kufikia TZS. Bilioni 29.3 mwaka 2022/2023. Aidha, kuna ongezeko kubwa la abiria wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa
kutumia Viwanja vya Ndege kutoka abiria 1,609,235 mwaka 2019 (Kabla ya
UVIKO - 19) na 840,599 mwaka 2020 (wakati wa UVIKO - 19) hadi kufikia
abiria 1,904,459 mwaka 2023.
Ndugu Wananchi,
Mafanikio mengine ni kuanza kazi kwa kampuni ya Emirate leisure inayoendesha biashara
katika jengo jipya la TB3 pamoja na
kampuni ya Dnata inayohusika na uhudumiaji wa ndege. Kupitia
Kampuni hizi uwanja wa ndege wa AAKIA umeweza kupata tuzo ya Kimataifa kuhusu
mabadiliko ya huduma bora za chakula na vinywaji kutoka “Airport Food &
Bevarage (FAB) + Hospitality Conference & Awards’’ Bangkok nchini
Thailand.
Kadhalika, Serikali imeingia Makubaliano na Kampuni ya SEGAP ya Ufaransa kuisaidia Menejimenti katika huduma za uendeshaji viwanja kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma za usafiri wa Anga hapa nchini. Vile vile, kazi ya upembuzi yakinifu (feasibility study) imekwishanza kwa ajili ya ujenzi wa jengo la nne la abiria - TB4 katika kiwanja cha AAKIA. Ripoti ya awali tayari imeshakamilika na Serikali ipo katika hatua za kukamilisha utaratibu wa upatikanaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.
Kwa upande wa ujenzi wa Uwanja wa Pemba, Serikali imeshakamilisha hatua za tathmini na kuanza kulipa fidia. Sambamba na hilo, Serikali imekamilisha kazi ya uwekaji wa taa za kuongozea ndege katika njia ya kurukia ndege (Portable AGL lights system) ili kuziwezesha ndege kutua na kuruka kwa usalama zaidi wakati wa usiku na wakati wa mvua na mawingu.
Ndugu Wananchi
Katika awamu zote baada ya
Mapinduzi, Serikali ilifanya jitihada za kuwezesha upatikanaji wa huduma za
umeme kwa wananchi pamoja na miradi ya kiuchumi. Tunapoadhimisha miaka 60 ya
Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio yamepatikana katika
kuimarisha upatikanaji wa huduma za umeme nchini.
Kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za umeme kwa urahisi, Serikali imepunguza bei ya kuunganisha umeme kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 50. Punguzo hilo ni kutoka TZS. 464,000 kufikia 200,000 kwa gharama za uungaji usiozidi mita 30. Vile vile, kutoka TZS. 1,700,000 kufikia 690,000 kwa gharama za uungaji wa nguzo moja na kutoka TZS. 2,600,000 kufikia 1,040,000 kwa gharama za uungaji wa nguzo mbili.
Hatua hiyo imesababisha idadi ya wateja wanaoomba
kuunganishiwa umeme kuongezeka hadi kufikia wastani wa wateja mia mbili (200)
kwa siku katika kipindi hiki kutoka wastani ya wa wateja 50 kwa siku hapo
awali. Wananchi wengi wameweza kufikiwa na huduma ya umeme ambapo Shirika la
ZECO limeweza kuwaungia umeme wananchi 93,124; (Unguja 78,122 na Pemba 15,002)
sawa na ongezeko la wateja kwa asilimia 45 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kufuatia kuimarika kwa huduma za usambazji umeme vijijini
katika kipindi cha miaka mitatu (3), Serikali imeweza kuviungia umeme jumla ya
Vijiji 190 ambapo Unguja ni 116 na Pemba 74, sawa na asilimia 62 ya Vijiji 305
kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.
Katika kuhakikisha Zanzibar inapata vyanzo vyake vya ndani
vya uzalishaji umeme, Serikali imesaini mkataba wa mauziano ya umeme (PPA) na
Kampuni ya Generation Capital Ltd kwa lengo la kuwekeza katika nishati ya umeme
wa jua kwa kujenga mtambo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 130. Aidha,
Serikali imetiliana saini na Kampuni ya ESR ya Ujerumani ambayo itazalisha
megawati 15 za umeme wa jua kwa ajili ya kisiwa cha Pemba. Sambamba na hatua
hiyo, Serikali inashirikiana na mshauri elelezi kutoka Kampuni ya NOVAVIS
INTERNATIONAL ya Marekani kufanya upembuzi yakinifu wa kutafuta ufumbuzi wa
changamoto ya umeme mdogo katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Vile vile,
mshauri elekezi wa Kampuni ya WSP ya Canada amepatikana kwa ajili ya upembuzi
yakinifu wa mradi wa ujenzi wa laini kubwa ya kilowati 132 ya Mkoa wa Kusini na
Kaskazini Pemba kwa ufadhili wa AfDB, KOICA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ndugu Wananchi
Kabla ya Mapinduzi watoto
wengi wa Zanzibar hawakupata elimu kwa kukosa uwezo wa kuilipia, ubaguzi na uchache
wa skuli. Baada ya Mapinduzi, fursa za upatikanaji wa elimu zimeimarika katika
ngazi zote. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi, mafanikio makubwa
yamepatikana katika uimarishaji wa miundombinu ya elimu na ongezeko la
uandikishaji wa wanafunzi.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi cha miaka mitatu ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya elimu kwa ujenzi wa skuli mpya zikiwemo za ghorofa, ujenzi wa maabara, ujenzi wa vyoo pamoja na ukarabati wa skuli mbali mbali. Jumla ya madarasa 2,273 yamejengwa ambapo madarasa 1,131 yamekamilika na tayari yanatumika. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la madarasa 773 katika lengo la kujenga madarasa 1500 kwa mujibu wa ilani ya CCM 2020 - 2025. Vile vile ujenzi wa maabara 10, vyoo 1,693 na ukarabati wa Skuli 24 umekamilika.
Juhudi hizi za Serikali zimeanza kuzaa matunda kwa kuimarisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa ya darasa la 7, kidato cha 4 na 6. Kwa upande wa matokeo ya darasa la 7 ufaulu umeongezeka kutoka wanafunzi 2,167 waliofaulu madarasa ya michepuo na vipawa mwaka 2021 na kufikia wanafunzi 6,666 mwaka 2023. Aidha Takwimu zinaonesha kuwa, ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 74 mwaka 2022. Pia, matokeo ya kidato cha sita ya mwaka 2023 yametupa taswira bora zaidi, ambapo asilimia 99.3 ya wanafunzi wamefaulu kuendelea na masomo ya chuo kikuu. Kati yao, asilimia 65.9 wamefaulu katika masomo ya Sayansi. Aidha, wanafunzi wawili tu kati ya wanafunzi 2,587 waliofanya mtihani walipata divisheni zero ikilinganishwa na wanafunzi 99 waliopata divisheni 0 mwaka 2021.
Kwa kuwazingatia wenye mahitaji maalum, Serikali imewajengea Skuli maalum mbili pamoja na kujenga ngazi mteremko (ramps) kwa ajili ya kuwasaidia wenye mahitaji maalum katika Skuli 43 Unguja na Pemba. Pia Serikali inakamilisha matayarisho ya ujenzi wa vyuo vitano vya mafunzo ya Amali na kuvifanya kuwa kumi kwa madhumuni ya kuzidi kupanua fursa za elimu ya ujuzi. Serikali pia imeimarisha mafunzo ya juu ya fani za ufundi katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia hadi ngazi ya shahada ya kwanza. Aidha, katika kuimarisha elimu jumla ya madawati 4,012 yaliyogharimu TZS Bilioni 1.98 kwa ajili ya Skuli za msingi yamenunuliwa na ajira 2,050 za walimu zimetolewa ili kupunguza tatizo la upungufu wa walimu.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi, mafunzo ya walimu yameendelea kuimarishwa katika vyuo viwili vya ualimu vya Serikali na katika vyuo vikuu vilivyopo Zanzibar ambapo kabla ya Mapinduzi kulikuwa na Chuo kimoja tu cha ualimu cha Beit Raas. Fursa ya Elimu ya juu nayo imeimarika ambapo mwaka 2023, Vyuo vikuu vimedahili wanafunzi 11,272 katika fani mbalimbali kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamivu.
Ndugu Wananchi,
Bajeti
ya Serikali katika Sekta ya elimu imeongezeka kutoka TZS Bilioni 265.5 mwaka 2021/2022 na kufikia TZS Bilioni 457.2 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia
72.2. Aidha, Serikali inaendelea kuwapatia mikopo na udhamini vijana
wanaojiunga na elimu ya juu ndani na nje ya nchi. Bajeti ya Serikali kwa Bodi
ya Mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka TZS Bilioni 19 kwa mwaka 2022/2023 na kufikia TZS Bilioni 29.4 kwa mwaka 2023/2024. Ongezeko hili limenufaisha
wanafunzi wa elimu ya juu 6,060 wanaosoma vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.
Hatua hii imewezesha kuzalisha wataalamu kwa wingi katika fani mbali mbali na
kupunguza tatizo la kutegemea wataalam kutoka nje ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi,
Juhudi kubwa imefanywa na
Serikali katika kipindi cha miaka 60 iliyopita kwa madhumuni ya kuimarisha
huduma za afya ambazo kabla ya Mapinduzi zilitolewa kwa ubaguzi na
hazikutosheleza mahitaji. Katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane,
mafanikio yamezidi kupatikana kutokana na mabadiliko makubwa ya muundo na
uendeshaji wa huduma za afya nchini. Serikali imejenga Hospitali kumi (10) za Wilaya ambazo zimeshaanza kazi.
Aidha, Serikali imedhamiria kujenga hospitali za Mikoa, ambapo kwa sasa ujenzi
wa hospitali ya Mkoa wa Mjini magharibi iliopo Lumumba umeshakamilika na imeshaanza
kazi.
Kuwepo hospitali hizi kumeboresha mfumo wa rufaa nchini kwa wagonjwa kuanza kupata huduma katika vituo vya Afya ya Msingi, Hospitali za Wilaya badala ya wagonjwa wote kukimbilia Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja. Hospitali za Wilaya hivi sasa zinatoa huduma bora za uzazi, upasuaji, maabara, rediolojia na ICU katika Wilaya zote Unguja na Pemba. Hatua hii imefungua ukurasa mpya wa upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini.
Mafanikio mengine ni kuimarika kwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kutokana na kuongeza bajeti ya dawa kutoka TZS. Bilioni 17 mwaka 2020 hadi TZS Bilioni 37.3 mwaka 2023/2024. Hivi sasa vituo vya afya vinapelekewa dawa kila mwezi. Dawa za Pemba zinapelekwa moja kwa moja na msambazaji bila ya kupitia Bohari kuu ya Dawa ya Unguja - Maruhubi.
Ndugu Wananchi,
Kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali imetoa ajira mpya 1,050 katika sekta ya Afya kati ya
hizo 738 Unguja na 312 Pemba. Madaktari bingwa
wameongezeka kutoka 50 mwaka 2020 hadi kufikia 90 mwaka 2023. Maslahi ya wafanyakazi
yameboreshwa, mishahara imeongezwa kutokana kiwango cha elimu, muda wa ajira na
kada muhimu. Mafanikio mengine ni
kuanza kwa Mfuko wa Huduma za Afya (ZHSF) kuanzia Oktoba
2023. Huduma zake zinapatikana katika Hospitali za Umma na Binafsi. Hadi
kufikia tarehe 31 Oktoba 2023, jumla ya Watumishi wa Sekta za Umma 53,490 wameingizwa katika mfumo.
Ndugu Wananchi,
Uimarishaji wa huduma za Afya nchini umepelekea kupunguza
tatizo la mama wajawazito kujifungulia majumbani na vifo vya watoto wachanga. Vifo
vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 120 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi vifo 99 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka
2022. Hali hii kwa kiasi kikubwa imechangiwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa,
vifaa tiba, wataalam na kuimarika kwa elimu ya Afya kwa jamii.
Vile vile, ufanisi umepatikana baada ya kuanza kwa utaratibu wa kutoa huduma za afya kwa ushirikiano na Sekta Binafsi. Utaratibu huu umeondosha usumbufu kwa wananchi wanaofika kupata huduma na vipimo vyote wanavyohitaji bila ya kulazimika kwenda hospitali binafsi. Aidha, usimamizi wa Hospitali za Wilaya unaofanywa na Taasisi binafsi umeimarisha hali ya usafi, upatikanaji wa chakula cha wagonjwa na mazingira ya nje kwa kupanda bustani. Utaratibu huu unahakikisha dawa zote muhimu zinapatikana katika hospitali zote za Wilaya.
Ndugu
Wananchi,
Sekta
ya maji ni miongoni mwa sekta muhimu kwa maisha ya watu na maendeleo yao. Baada
ya Mapinduzi, Serikali ilianza jitihada ya kuwapatia huduma ya maji safi na
salama wananchi wa Zanzibar wanaoishi mijini na vijijini. Jitihada hizo
zimeendelezwa katika awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, huduma ya maji safi na salama zimeimarika kwa kuongeza uzalishaji, uhifadhi na usambazaji. Katika awamu hii ya Nane tumeweza kutekeleza miradi miwili mikubwa. Miradi hiyo ni Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar wenye thamani ya Dola za Kimarekani TZS Milioni 92.18 na Mradi wa Ahueni ya UVIKO – 19 wenye thamani ya TZS Bilioni 40.2.
Katika kipindi hiki
cha miaka mitatu, jumla ya visima 102
vimechimbwa vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 201,552,000 kwa siku. Hatua hiyo itawezesha uzalishaji wa maji
kuongezeka kufikia lita 345,388,735 tutakapomaliza
kufungua miradi yote ya maji ambapo mahitaji kwa sasa ni lita 264,568,220. Jumla ya Skimu 9 mpya za
maji tumeshazifungua rasmi katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 60 ya
Mapinduzi, kati ya Skimu 17 mpya.
Ndugu
Wananchi,
Jumla ya matangi 15
ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 134,000,000
yamejengwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi kupitia Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji
wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar. Aidha, Matangi 10 yamejengwa Unguja na Pemba yenye ujazo wa lita milioni 1 kila moja
kupitia Mradi wa Ahueni ya UVIKO - 19 yenye jumla ya ujazo wa lita 10,000,000 kuwezesha uhifadhi mpya wa
lita 144,000,000 katika matangi
mapya 25 ya miradi yote miwili.
Kabla ya ujenzi huo
kulikuwa na matangi 64 kwa Unguja na Pemba yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 46,915,000. Kukamilika kwa Miradi
miwili mikubwa tutaweza kuwa na uhifadhi wa maji lita 190,915,000. Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 144 ya
uhifadhi.
Ndugu
Wananchi,
Kazi ya ulazaji mabomba
ya kusambazia Maji kwa miradi yote miwili itafikia jumla ya KM 785.9, kwa mradi wa Exim Bank KM 466.0 na mradi wa Ahuweni ya UVIKO - 19
KM 319.0 katika kipindi cha miaka
mitatu. Aidha, Serikali kupitia ZAWA imeanzisha Mfumo shirikishi (Intergrated
Water Management System) unaosaidia kusimamia utekelezaji wa huduma ya maji,
zikiwemo kuwafahamu wateja wa Mamlaka ya maji, kupeleka bili, kupokea malipo,
kupata taarifa za uvujaji na ujazo wa maji katika matangi.
Jitihada hizi za
Serikali hadi sasa, zimewezesha kupeleka huduma za maji safi na salama katika
shehia 342 kati ya shehia 388 kwa kusambaza mtandao wa maji
Unguja na Pemba. Lengo la Serikali ni kuwafikishia huduma endelevu za maji safi
na salama wananchi wote wa Zanzibar kwa saa 24.
Miradi mingine mipya
ya maji safi na salama iko njiani kutekelezwa ili kuimarisha zaidi upatikanaji
wa huduma hii ikiwemo Mradi wa KfW wa Ujerumani wenye thamani ya € Milioni 25
(Grant), Mradi wa JICA Yen Milioni 100, Mradi wa Mkopo wa Exim Bank USD Milioni
35 na Mradi wa NEC wenye thamani ya USD Milioni 26.
Ndugu
Wananchi,
Ujenzi wa majengo kwa ajili ya makaazi,
Ofisi na biashara umepewa umuhimu katika awamu zote za Serikali baada ya
Mapinduzi. Kwa kuzingatia haja ya wananchi kupata makaazi bora, Serikali
ilianzisha ujenzi wa nyumba za maendeleo mijini na vijijini na kuwapatia wananchi.
Aidha, majengo ya huduma za kiofisi, hospitali na Skuli yalijengwa baada ya
Mapinduzi ili kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kuongeza ufanisi.
Vile vile, ujenzi wa majengo ya Umma na Binafsi ya biashara unaendelezwa.
Katika kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, jitihada ya ujenzi wa majengo ya makaazi, biashara na Ofisi za Serikali umeshamiri. Ujenzi wa nyumba za makaazi kwa Mchina na Tomondo unaendelea. Vile vile Serikali imejenga maduka ya kisasa Darajani. Maandalizi ya ujenzi wa mji wa Serikali Kisakasaka yameanza pia ujenzi wa eneo la maonesho ya biashara Nyamanzi umikamilika na limeanza kutumika. Kwa lengo la kuimarisha haiba ya mji na kuondoa changamoto ya maegesho, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) inaendelea na mradi wa kituo cha mabasi Kijangwani na ujenzi wa maegesho ya kisasa katika eneo la Malindi. Serikali inaendelea kuwakaribisha Wawekezaji katika Sekta ya ujenzi zikiwemo nyumba za gharama nafuu, kumbi za mikutano na majengo ya biashara.
Ndugu Wananchi,
Nchi yetu ina historia ndefu ya maendeleo ya sekta ya habari
na michezo kabla na baada ya Mapinduzi. Kuhusu sekta ya habari, juhudi kubwa
zimechukuliwa na Serikali katika awamu zote za uongozi baada ya Mapinduzi kwa madhumuni
ya kuimarisha utoaji na upatikanaji wa habari nchini. Serikali ya Awamu ya Nane
imeziendeleza juhudi hizo kwa kuliimarisha Shirika la Utangazaji la Zanzibar
(ZBC)
kwa kulipatia vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi na mafunzo kwa wafanyakazi ili
kuongeza ufanisi katika kutoa huduma zake. Pia, Serikali imepanga kuimarisha
Kampuni ya Uunganishaji Maudhui Zanzibar (ZMUX) kwa kuweka miundombinu ya
urushaji wa matangazo na vifaa vya kisasa, gari la kurushia matangazo (OB VAN)
pamoja na wataalamu ili kufanya kazi kwa ufanisi. Aidha, Shirika la Magazeti ya
Serikali limeimarishwa kwa kupatiwa jengo jipya la Ofisi na mtambo wa kuchapia
magazeti. Hatua hii imeliongezea Shirika ufanisi kwa kuhimili gharama na
kuongeza uzalishaji na usambazaji wa magazeti kwa asilimia 80 ya Wilaya zote za
Tanzania bara.
Kwa upande wa sekta ya michezo, Serikali ya Awamu ya Nane, imekamilisha matengenezo makubwa ya viwanja vya Amani na Gombani kuwa na kiwango cha kimataifa. Vile vile, katika uwanja wa Amani, ujenzi wa viwanja viwili vya mpira wa miguu vya nje, ukumbi wa judo na viwanja vya ndani vya michezo midogo umekamilika. Kadhalika, ukarabati mkubwa wa hoteli ya uwanja wa Amani unaendelea na kutarajiwa kukamilika hivi karibuni. Aidha, kupitia mradi wa michezo kwa ushirikiano na Serikali ya Ujerumani, tunakamilisha zabuni ya ujenzi wa viwanja vitatu vya michezo katika maeneo ya Mkokotoni, Kangani na Mchanga mdogo. Kwa lengo la kuimarisha sekta ya michezo, Serikali imeruhusu mchezo wa ngumi hapa Zanzibar ili kuwapatia nafasi wapenzi wa mchezo huo.
Ndugu Wananchi,
Utumishi
bora wa Umma ni miongoni mwa vigezo vya Utawala Bora unaotekelezwa na
kusimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi chote cha miaka
sitini 60 iliyopita. Katika miaka mitatu 3 hii, Serikali imechukua hatua mbali
mbali za kuimarisha mazingira ya Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi.
Serikali imeongeza maslahi ya Watumishi kwa kupandisha mishahara na maposho kwa
kuzingatia viwango vya Elimu, Kada na Uzoefu. Hatua hii, imeweza kuondoa
malalamiko yaliyokuwepo ya kutozingatiwa suala la Elimu, Kada na Uzoefu katika
Miundo ya Awali.
Katika
marekebisho hayo, Serikali ilitumia jumla ya TZS. Bilioni 58.1 kwa mwezi kutoka TZS. Bilioni 35.5. Kiwango
hicho ni ongezeko la TZS. Bilioni 22.6, sawa
na asilimia 38.85. Vilevile, Serikali ilifanya marekebisho ya kima cha chini
cha Pencheni kwa Wastaafu kutoka TZS.
90,000 kwa mwezi kwenda TZS. 180,000
sawa na asilimia 100. Kwa upande wa
Pencheni jamii, Serikali imepandisha Pencheni hiyo kutoka TZS. 20,000 kwenda TZS.
50,000 kwa mwezi sawa na asilimia 150.
Mbali na Pencheni, Serikali imefanya mabadiliko katika mifumo ya ulipaji wa
Kiinua Mgongo kwa Wastaafu ambapo awali walikuwa wakilipwa kwa awamu mbili au
tatu, lakini kwa sasa ulipaji umekuwa ukilipwa kwa awamu moja tu.
Ndugu Wananchi,
Kupitia Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
tumeweza kuimarisha kiwango, mbinu pamoja na kasi ya ukaguzi wa matumizi
ya fedha za umma, ukusanyaji wa mapato pamoja na utunzaji wa rasilimali za
umma. Kwa kiwango kikubwa tumeimarisha ukaguzi katika utekelezaji wa miradi ya
Serikali. Kwa lengo la kuongeza uwazi, tumeanzisha utaratibu wa kusomwa Ripoti
ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali (CAG) hadharani. Hatua hiyo
imesaidia sana kukomesha ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Aidha, niliahidi kuendeleza Uchumi wa
kidigitali na kuhakikisha kwamba tunatumia mifumo ya kielektroniki katika
utoaji huduma na uendeshaji wa Serikali. Katika kipindi hiki cha Serikali,
tumeendeleza na kuanzisha mifumo mbali mbali ambapo hivi sasa mifumo 29 muhimu
inaendeshwa na kusimamiwa na Wakala wa Serikali Mtandao.
Ndugu
Wananchi,
Sekta ya Sheria ni miongoni mwa sekta kongwe nchini katika
uendeshaji na usimamizi wa masuala ya kusimamia haki. Tunapoadhimisha miaka 60 ya
Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio makubwa
yamepatikana katika sekta ya Sheria. Zanzibar imepiga hatua katika
kuimarisha utendaji wa Mahakama katika ngazi zote. Hivi sasa, Mahkama maalum ya
kusikiliza kesi za udhalilishaji imefunguliwa rasmi katika Mahkama za Mikoa
Unguja na Pemba. Pia, mfumo wa uendeshaji kesi kwa njia ya kieletroniki tayari
umeandaliwa na kufanyiwa majaribio kwa ajili ya kuongeza kasi ya uendeshaji wa
kesi, juhudi zetu hizi zimeimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi. Katika
kuhakikisha mahakama zetu zina mazingira mazuri ya kufanyia kazi, Serikali
inazifanyia matengenezo makubwa Mahakama katika ngazi mbali mbali Unguja na
Pemba.
Ndugu Wananchi,
Kuimarika kwa
ushirikishwaji wa wananchi katika vyombo vya kutunga sheria, ni matokeo ya Mapinduzi
Matukufu ya mwaka 1964. Zanzibar ilianzisha Baraza la Wawakilishi mwaka 1980 ili
kutoa fursa ya kuwakilishwa Wananchi katika kujadili na kupitisha mipango ya
maendeleo, kuisimamia Serikali na kutunga Sheria. Kazi kubwa imefanywa na Baraza
la Wawakilishi katika utekelezaji wa majukumu yake tokea lilipoanzishwa. Katika
kipindi hiki cha miaka mitatu, Baraza la Wawakilishi limewezesha kupitishwa kwa
sheria mbali mbali na kupitisha bajeti ya Serikali. Vile vile, kupitia Kamati
za Baraza, Baraza la Wawakilishi linahoji utendaji wa taasisi za Serikali na
kutoa ushauri kwa madhumuni ya kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Nachukua fursa hii kutoa shukurani kwa Mheshimiwa Spika, Naibu Spika,
Wenyeviti, Wajumbe wote na Watumishi wa Baraza la Wawakilishi kwa ushirikiano
wanaotupa katika kutekeleza mipango ya Serikali.
Ndugu Wananchi,
Muungano wa Tanzania ambao ni
matunda ya Mapinduzi, mwaka huu wa 2024 unatimiza miaka 60 tokea kuasisiwa kwake.
Muungano wetu umetuwezesha kupata mafanikio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na
ustawi wa jamii.
Tokea kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano mwaka 2006, jumla ya hoja 25 zimejadiliwa na 18 kati ya hizo zimepatiwa ufumbuzi. Aidha, Zanzibar imeendelea kunufaika na mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada kutoka nje. Vile vile, hivi sasa Zanzibar inafaidika na miradi 10 ya maendeleo inayotekelezwa katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo ile ya TASAF, MIVARF na PADEP. Miradi hii imekuwa ikileta mabadiliko makubwa katika miundombinu, upatikanaji wa huduma mbali mbali za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.
Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na Sheria wa kuwatumikia wananchi wote kwa misingi ya usawa na kuwaletea maendeleo. Tutahakikisha tunaitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Malengo ya kikanda na kimataifa pamoja na ahadi tulizozitoa katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020.
Ndugu Wananchi,
Namalizia hotuba yangu kwa
kutoa shukurani kwa wasaidizi wangu wakuu; Mheshimiwa Makamo wa Kwanza wa Rais
na Makamo wa Pili wa Rais kwa kutekeleza vyema dhamana zao. Pia, nawashukru
Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, watendaji na watumishi
wote wa Serikali, viongozi wa dini, sekta binafsi na washirika wetu wa
maendeleo wakiwemo Serikali za nchi rafiki, mashirika na Taasisi za Kitaifa na
Kimataifa kwa ushirikiano wao. Natoa shukrani maalumu kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa; Dkt. Samia Suluhu Hassan, viongozi na
wanachama wote wa CCM, Jumuia zake na viongozi wengine wa vyama vya siasa kwa
kutupa ushirikiano katika kufanikisha majukumu ya Serikali hadi tunapoadhimisha
miaka 60 ya Mapinduzi yetu.
Shukrani za pekee nazitoa kwenu ndugu wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na kushirikiana na Serikali yenu katika kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za maendeleo. Ahadi yangu kwenu ni kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kuyadumisha mafanikio tuliyoyapata katika miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na tuongeze kasi, uwajibikaji na uadilifu kwa lengo la kupata mafanikio. Tumuombe Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamano na atuwezeshe kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi zaidi. Nakutakieni nyote kila la kheri katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
MAPINDUZI DAIMA!
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment