Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
akiweka Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho
Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya
Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tarehe 11 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuacha tabia ya kuficha watoto wenye ulemavu majumbani na kuwakosesha haki ya kupata elimu.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Amesema ni vema watoto hao wakapata elimu ili kuweza kutumia vipaji walivyonavyo kwani serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia ikiwemo ya shule jumuishi.
Makamu wa Rais amesema Rasilimaliwatu ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini ambapo elimu bora ndiyo inayowezesha uendelezaji wa rasilimaliwatu ili kuchangia kikamilifu katika kujenga Taifa na kuleta maendeleo kwa ujumla. Amesema sekta ya elimu ni kipaumbele cha Serikali zote mbili zinazoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili kujenga jamii iliyoelimika na yenye maarifa muhimu.
Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba katika Miaka 60
ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni vema kujivunia hatua kubwa ya Maendeleo iliyofikiwa katika
sekta mbalimbali hususani elimu kama vile
kuongezeka na kuboreshwa kwa
miundombinu ya elimu katika ngazi zote, kuongezeka kwa idadi ya
wanafunzi kutoka 25,432 mwaka 1964 hadi kufikia wanafunzi 592,781 mwaka 2023.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa ujifunzaji na ufundishaji kwa
wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuongezeka
kwa Vyuo vinavyotoa elimu ya juu ambapo hivi sasa vimefika 7 kutoka 0 Mwaka
1964 pamoja na ongezeko la uwekezaji katika elimu ya juu kutoka nje ya nchi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi kutambua jukumu la kulinda na kudumisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kukemea vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na dhamira hiyo. Amewaasa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya kila mmoja na Taifa kwa ujumla pamoja na vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea ama kuleta utengano.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela
Muhammed Mussa amesema kukamilika kwa mradi huo ni jitihada mbalimbali
zinazofanywa na serikali ili kuhakikisha elimu inapatikana katika mazingira
mazuri. amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kufanya mapinduzi
makubwa ya kielimu ambapo yanajumuisha uboreshaji wa miundombinu, kuongeza
maslahi ya walimu pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa katika vituo vya kutolea
elimu.
Amesema katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt.
Hussein Mwinyi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imefikia lengo la asilimia
150 katika utekelezaji wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu.
Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele imegharimu
shilingi bilioni 3.7.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
11 Januari 2024 Zanzibar.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati alipowasili katika ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tarehe 11 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria Ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tarehe 11 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
akisikiliza maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said wakati akikagua miundombinu mbalimbali
katika Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja
mara baada ya kuizindua ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tarehe 11 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wasioona wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Elimu Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tarehe 11 Januari 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi viziwi pamoja na walimu wao ambao
wanafanya Sanaa ya kucheza ngoma wakati wa ufunguzi wa Skuli ya Msingi ya Elimu
Mjumuisho Jendele iliyopo Wilaya ya Kati, Unguja ikiwa ni shamrashamra za
Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tarehe 11 Januari
2024.
No comments:
Post a Comment