Na.Mwashamba Juma Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza ujenzi wa miundombinu imara kwa Sekta za Maendeleo nchini.
Dk. Mwinyi ameeleza
hayo uwanja wa Jamuhuri wa Skuli ya Sekondari Utaani Wilaya ya Wete, Mkoa wa
Kaskazini Pemba, alipofungua skuli ya Sekondari ya wanawake ya Ghorofa tatu iliyojengwa
upya na serikali baada ya kupata ajali ya kuunga moto na kuteketeza kila kitu Mwezi
Machi mwaka 2022.
Alisema, ujenzi wa
skuli hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya serikali iliyoitoa baada ya tukio la moto
lililoteketeza skuli ya awali iliyokuwa na madasa 11 na kuahidi kujenga skuli
bora zaidi ambayo kwasasa ina madarasa 41.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kujenga dahalia kubwa ya kisasa itakayoendana
na hadhi ya skuli hiyo.
Katika kuboresha haiba njema ya mandhari mpya ya eneo la skuli
hiyo, Rais Dk. Mwinyi ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kusimamia
ujenzi uliobakia wa ukumbi wa mikutano na uwanja wa michezo itakayoendana na
hadhi ya mwonekano mzuri wa skuli hiyo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameridhia ombi la wananchi wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba la kuimarishiwa skuli ya Jadida iliopo Wete Pemba na kueleza
kwamba Serikali itajenga skuli mpya ya msingi ya ghorofa pamoja.
Alisema katika hatua ya kuiboresha hadhi ya kisiwa cha Pemba,
Serikali kupitia Shirika la nyumba la Zanzibar (ZHC) itafanya ukarabati mkubwa
wa nyumba za maendeleo za kisiwa hicho au kujenga nyumba mpya 4,000 zenye hadhi
ya juu kwa Unguja na Pemba.
Akizungumzia bandari ya Wete, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza
wananchi wa kisiwa Pemba kwamba Serikali pia imedhamiria kujenga bandari ya
kisasa ya Wete ambapo hatua za awali za ujenzi wa bandari hiyo zimekamilika.
Pia, Rais Dk. Mwinyi ameeleza hatua za Serikali ilivyofikia juu
ya ujenzi wa bandari ya Mkoani na ya Shumba mjini.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), alisifu
jitihada za Rais Dk. Mwinyi kwa uwekezaji mkubwa anaouendeleza wa wizara hiyo
na kuahidi kupitia ushirikiano mkubwa wa Wizara hiyo utaendeleza juhudi za Mhe.
Rais kwa kuzitunza skuli zote ziendelee kubakia kwenye ubora wake.
Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Wete, ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar, Harusi Said Suleiman alimshukuru Rais Dk.
Mwinyi kwa kuendelea kuboresha maendeleo ya nchi zikiwemo barabara safi za mijini
na vijini, ujenzi wa skuli za ghorifa na kuimarisha huduma za jamii za afya na
maji safi na salama.
Akizungumza kwenye ghafla ya ufunguzi wa Utaani Sekondari, Katibu
mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla alisema, ujenzi wa
Skuli hiyo ulianza mwezi Mei mwaka jana na uligharimu shilingi bilioni 6.2
umejumuisha madarasa 41, ofisi nne za walimu, ofisi ya mwalimu mkuu, vyoo 32, maktaba,
maabara, chumba cha kompyuta na stoo.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatibu alisema,
wananchi wa mkoa huo sasa wanajali zaidi maendeleo na wameachana na siasa za
zamani za chuki wanaendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano baina yao bila
kujali tofauti zao, jambo alilolisifu ni kuimarika kwa maendeleo kwenye utawala
wa Dk. Mwinyi.
Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi, kwa niaba ya Naibu Katibu
Mkuu wa Chama hicho, Zanzibar, Dk. Muhammed Said Muhammad (Dimwa), Mkuu wa
Idara ya Oganaizesheni Ofisi kuu ya chama hicho Kisiwandui, Zanzibar ambae pia
ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM - Taifa, Omar Kilupi alisema ufunguzi wa
Skuli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya 2020 – 2025 ambayo tayari
imepitiliza malengo iliyojipangia kuwaletea wananchi wa Zanzibar Maendeleo
makubwa.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment