Habari za Punde

MAKADHI WAKUTANISHWA KUJADILI CHANGAMOTO ZA ONGEZEKO LA TALAKA NA UTELEKEZAJI WA WATOTO

Mkurugenzi  Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali akizungumza na Makadhi wa Mikoa ya Zanzibar katika kikao cha kujadili changamoto za kukabiliana na ongezeko la Talaka na utelekezaji wa Watoto huko Sebleni Wilaya ya Mjini.

Mkuu wa divisheni ya jinsia na Mratibu wa mapambano ya vitendo vya ukatili  na udhalilshaji wa Wanawake na Watoto katika Idara ya maendeleo ya Jamii, jinsia na Watoto Omar  Haji Omar akitoa maelezo kikao cha kujadili changamoto za kukabiliana na ongezeko la talaka na utelekezaji wa Watoto, kikao ambacho kimefanyaka Sebleni Mjini Zanzibar.

 

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO.

Na Fauzia Mussa Maelezo. 10.06.2024.

Idara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inekuasudia kuanzisha kitengo cha usuluhishi katika Mahkama za Kadhi ili kuwapunguzia mrundikano wa kesi zinazohusiana na Wanawake na Watoto.

 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo Siti Abasi Ali wakati alipokuwa akizungumza na Makadhi wa Mikoa ya Unguja, kikao ambacho kimefanyika huko  Sebleni Wilaya ya Mjini.

 

Amesema lengo la kuanzisha kitengo hicho ni kuweka mikakati bora na imara ya kutatua kesi hizo kwa uhakika na kuondosha manung'uniko kwa jamii.

 

Amesema Makadhi hao wanapokea kesi nyingi na wakati mwengine wanalazimika kutoa fat-wa kwa haraka kutokana na wingi wake jambo ambalo linachangia ongezeka la Talaka na kupelekea  utelekezaji wa Wanawake na Watoto.

 

Mbali na hayo, amesema vituo hivyo vitapunguza kesi katika jamii ikiwemo mirathi, migogoro ya ndoa na huduma za watoto.

 

Kwa upande wake Mratibu wa mapambano ya vitendo vya ukatili na udhalilshaji wa Wanawake na Watoto katika Idara hiyo Omar Haji Omar amesema Tafiti zinaonyesha kuwa, idadi kubwa ya Talaka inasababisha utelekezaji wa  Watoto katika jamii.

 

Hivyo amewataka Vijana kuacha kufunga ndoa kwa kufuata mkumbo  na mihemko na badala yake wapate elimu  kabla ya kufunga ndoa na kuifanyia kazi.

 

Amesema talaka ni chanzo cha Watoto kutelekezwa na kuharibika na kuwataka wanandoa kufikiria Watoto wao kabla ya kuachana ili kuwaondoshea usumbufu unaojitokeza.

 

Nao baadhi ya Makadhi hao, akiwemo Kadhi wa Wilaya ya Mjini Sheikh Ali Juma Machano na Kadhi wa Wilaya ya Magharibi B Sheikh Abubakar Ali mohammed wamesema  juhudi za kutoa elimu katika jamii bado zinahitajika ili kuondosha utoaji wa Talaka  kiholela.

 

Aidha Wameishauri Idara hiyo, kuwa na mpango wa kuhakikisha  masuala ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa inaanzia katika  Madawati ya jinsia katika ngazi ya Shehia pamoja na kuwepo Mikakati  madhubuti  ya kuzinusuru ndoa kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.