Habari za Punde

UKUSANYAJI WA MAONI YA MPANGO KAZI WA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tanzania, Khatib Mwinyichande Khamis  akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu ukusanyaji wa maoni kwa wadau mbali mbali  wanaohusika na mambo ya Utalii, Uchumi wa Buluu na Nishati,  katika Ukumbi wa Sanaa, Rahaleo.

 

Na Rahma Khamis – Maelezo  26/07 /2024.

Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tanzania, Khatib Mwinyichande Khamis  amewataka Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo katika ukusanyaji wa maoni kwa wadau mbali mbali ili kufanikisha utekelezaji wa  Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara.

 

Hayo ameyasema katika Ukumbi wa Sanaa, Rahaleo wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusiana maandalizi ya mpango huo.

 

Amesema lengo la ukusanyaji wa maoni hayo ni kuhakikisha linawafikia wadau  wanaohusika na mambo ya Utalii, Uchumi wa Buluu na Nishati pamoja na ushirikishwaji na wajumbe wengine katika mikoa yote ya Zanz ibar.

 

Aidha amefahamisha kuwa Serikali zote mbili ziko katika maandalizi ya mpango huo ambao unaandaliwa  chini ya Uratibu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).

 

Ameeleza kuwa Tume hiyo tayari imeshatekeleza jukumu Hilo kwa upande wa Tanzani Bara ambapo kwa sasa inatarajia kuanza katika Mikoa ya Zanzibar  kuanzia Julai 29 Hadi Agost 2 mwaka 2024.

 

"Tume ya Haki za Binadamu na Utwala Bora ni chombo chenye jukumu la kuhamasisha hifadhi za Haki za Binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala Bora nchini" alisema Kamishna.

 

Amesema kuwa maoni na michango hiyo itakusanywa kwa baadhi ya wadau wa Mamlaka ya Uhifadhi na Utekelezaji wa Mji Mkongwe, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Mamlaka ya Kukuza Uwekekezaji Zanzibar ( ZIPA).

 

Nyengine ni Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Umoja wa Hoteli Zanzibar (HAZ) Umoja wa wawekezaji wa watalii Zanzibar (ZATI) Umoja wa waongoza watalii Zanzibar, (ZATOGA) pamoja na Umoja wa waendesha Utalii Zanzibar ( ZATO)

 

Hata hivyo ameelezea wadau wengine wanaohusishwa kutoa maoni yao ni baadhi ya wafanyakazi  wa Hoteli na baadhi ya Hoteli za kitalii zilizopo Nungwi ,Kendwa na pamoja na wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hoteli hizo.

 

Kwa upande wa uzinduaji wa Nishati  Kamishnamesema kuwa wadau wataofikiwa ni Wizara ya Maji Nishati na Madini Zanzibar,  Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Gesi Asilia, Kampuni ya Mafuta Zanzibar pamoja na Zanzibar Petroleum Regulatory Authority

 

Amesema zoezi la ukusanyaji wa maoni pia litawashirikisha wananchi wanaoishi katika eneo la uchimbaji wa mchanga Donge Chechele pamoja na Eneo la uchimbaji na uchakataji wa matofali Pemba.

 

Kamishna amesema kwa upande wa wadau wa  Uchumi wa Buluu ambao  watafikiwa ni Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Kampuni ya Uvuvi, Shirika la Bandari, Shirika la Biashara, wakulima na wavuvi na wafanyabiashara wa samaki katika masoko ya Unguja na Pemba.

 

Hata hivyo ametowa wito kwa wananchi wa Zanzibar na kuwataka

kujitokeza kwa wingi katika zoezi la  ukusanyaji wa maoni hayo ili kupata taarifa sahihi zitakazosaidia kuandaa mpango huo .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.