Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema,
Zanzibar ina kila sababu ya kuanzisha mfumo wezeshi kwenye biashara
zinazochipukia zenye uwezo wa kukua kwa haraka ili kustawisha maisha ya mtu
mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Dk. Mwinyi
ameyasema hayo alipofungua mkutano wa tatu wa pamoja wa taasisi ya Utafiti na Uchambuzi
wa Sera za Kijamii na Uchumi Zanzibar, (ZRCP) leo tarehe 17 Septemba, 2024
kwenye ukumbi wa hoteli ya Madinatul Bahri, Wilaya ya Magharibi B.
Amefahamisha
kuwa Zanzibar ina wajasiriamali vijana wenye vipaji wanaochipukia kwenye ujasiriamali,
hivyo ni muhimu kuwakuza kwaajili ya uchumi jumuishi na endelevu wa Taifa.
Pia Dk. Mwinyi alisema, kuna
umuhimu mkubwa wa kuwawekea mazingira bora na rafiki ili wavumbue biashara
zenye faida kubwa na kuviendeleza vipaji vyao kwa maslahi mapana ya Taifa.
Alifahamisha,
nchi nyingi duniani zikiwemo Uholanzi, India, Korea Kusini pamoja na
nchi za Afrika kama Kenya, Tunisia, Afrika ya Kusini na Nigeria zimetumia mfumo
huo ipasavyo katika kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii, kukuza utajiri
wa nchi zao, kuongeza pato la taifa na kutengeneza ajira zenye maslahi
makubwa.
Rais Dk.
Mwinyi amezielekeza taasisi zilizoratibu mkutano huo, kuongoza mijadala na mada
zitakazojadiliwa kwa umakini ili ziletee tija nchini kulingana na mazingira ya kiuchumi
na biashara ya Zanzibar.
Aliwahakikishia
wadau na washiriki wa mkutano huo kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira
mazuri ya kuziimarisha Taasisi za kukuza Uchumi ili kuhakikisha vijana wanakuza
taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika kuvumbua na kuendeleza vipaji vyao.
Halikadhalika Rais
Dk. Mwinyi alitoa wito kwa taasisi za Serikali kuzitekeleza kwa vitendo sera na
miongozo mbalimbali itakayoanzishwa na ile iliyopo yenye lengo la kusimamia
utekelezaji wa maazimio ya kukuza vipaji vya wataalamu kupitia nyanja zote za
ubunifu na teknolojia.
Naye, Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Saada Mkuya Salum amesema utafiti
unofavywa na kituo cha ZRCP unalengo la kuweka msukumo wa kufanikisha malengo
ya Serikali na kuleta mageuzi kwa kiasi kikubwa yanayotokana na sayansi na
teknolojia kwa vile Zanzibar inakusudia kuanzisha soko la mitaji hivyo, ni
vyema kuwa na namna bora ya kufuatilia matokeo yanayotokana na utafiti ili
kufikia malengo.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZRCP Juma Reli, amesema ZRCP imekusudia kuwa kituo
bora chenye kutoa tafiti za hali ya juu na zenye manufaa kwa jamii katika
ukanda wa Afrika Mashariki na kuihakikishia Serikali kwamba kituo hicho, kipo
tayari kufanyakazi na Serikali kwa weledi, ukweli na uadilifu.
Mkutano huo wa
siku mbili imewakutanisha pamoja wadau kutoka taasisi mbalimbali za umma na
binafsi, washirika wa maendeleo na taasisi za kimataifa, unalengo la kutafuta
na kujadili namna bora ya kutumia teknolojia na utafiti ili kubaini changamoto
na mwelekeo mpya wa kuwakuza wajasiriamali wanaochipukia.
No comments:
Post a Comment