Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha.
Cyprian Luhemeja akifungua kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano
wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP
29), uliofanyika Oktoba 29,2024 mkoani Dodoma.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema suala la
mazingira ni mtambuka hivyo linahitaji ushirikiano kutoka wizara, taasisi pamoja
na wadau ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa endelevu.
Amesema
hayo leo Oktoba 29, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Makatibu
Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa
Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) unaotarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 11 hadi
22, 2024 Baku, Azerbaijan.
Mhandisi
Luhemeja amesema kuwa pamoja na juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari
za mabadiliko ya tabianchi changamoto hiyo bado ni kubwa hivyo, amezitaka
wizara, taasisi na wadau kuifanya ajenda ya mazingira kuwa ni moja ya
vipaumbele vyake.
Ametoa
wito kwa wajumbe watakaoshiriki katika mkutano huo watambue kuwa wanakwenda
kutafuta fursa hususan za kifedha kwa ajili kuwezesha nchi kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kila
mmoja wetu aguswe na suala la mazingira, tunapokwenda kushiriki COP29 tusiende
kimazoea, maazimio tunayoyafikia yasiishie kwenye makaratasi tuyawasilishe
kwenye mkutano na yaje na matokeo, tunataka mkutano huu ulete mabadiliko katika
nchi yetu,” amesisitiza.
Aidha,
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa lengo la Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuhakikisha
kila wizara, taasisi na wadau wanawekeza katika sekta ya mazingira kwani
inagusa maeneo yote.
Akifafanua
zaidi, Katibu Mkuu Luhemeja amesema kuwa mazingira yanagusa maisha ya mwanadamu
kwa asilimia kubwa katika sekta mbalimbali kupitia Malengo ya Milenia ikiwemo
kuondoa umaskini na njaa.
Ili
kuepukana na njaa, ametoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji
wa mazingira hususan kwenye vyanzo vya maji kwani maji ni uhai wa mwanadamu.
Kwa
upande wa nishati safi ya kupikia, Mhandisi Luhemeja amesema kuwa ajenda hiyo
ni mbadala wa mapambano dhidi ya ukataji wa miti huku akiwahimiza wananchi kuacha
matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira.
Amesema
nishati safi ya kupikia si gesi pekee bali inahusisha mbinu mbalimbali huku
akipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwa na mikakati ya kuendeleza
nishati mbalimbali zikiwemo umeme, hatua inasaidia kupunguza ukataji wa miti.
Kwa
upande wake Mshauri wa Rais katika Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na
Mazingira Dkt. Richard Muyungi amesema washiriki wa CO29 watakuwa na kazi ya
kuhakikisha ajenda za nchi zinakubalika na kupita.
Amesema
mabadiliko ya tabianchi ni fursa ambayo Tanzania inapaswa kuitumia ipasavyo katika
kufanya majadiliano na nchi zitakazoshiriki katika mkutano huo kupitia matukio
299.
Dkt.
Muyungi ameeleza kuwa ushirikiano uliopo baina ya nchi na wadau wa maendeleo
duniani ambao unapaswa kuwa ni mojawapo ya hatua zitasaidia katika maendeleo ya
nchi.
“Unapokwenda
kwenye COP hivi sasa unakuta watu wengi kama private sectors (sekta binafsi), kampuni,
NGOs, ili sasa kutafuta ushirikiano wa kupunguza gesijto na hili sasa sio suala
la Serikali tu ni suala la uashirikiano na wadau,” amesisitiza.
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akizungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29) kilichoanyika Oktoba 29,2024 mkoani Dodoma.
Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Bi. Kemilembe Mutasa akizungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29) kilichoanyika Oktoba 29,2024 mkoani Dodom.
Baadhi ya viongozi walioshiriki kikao cha
Makatibu Wakuu cha Maandalizi ya Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa
Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 29) kilichoanyika Oktoba 29,2024 mkoani
Dodoma.
No comments:
Post a Comment