RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk.
Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi kusimamia hifadhi za barabara na kuwazuia wananchi kutojenga
na kufanya biashara maeneo hayo ili kukwepa mzigo mkubwa wa fidia kwa Serikali
pale inapotaka kupitisha miundombinu mengine muhimu.
Amefahamisha kuwa hivi sasa kumezuka tabia ya wananchi kuzitumia
hifadhi za barabara kwa kujenga na kufanya biasharara bila kujali umuhimu wa
hifadhi hizo na wakati mwengine kuziathiri barabara zilizojengwa.
Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo alipofungua barabara mpya ya
Jozani, Charawe, Ukongoroni hadi Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja yenye urefu wa
kilomita 24.5.
Ameeleza kuwa wananchi wanawajibu mkubwa wa kutunza barabara
zinazojengwa katika maeneo yao, kuonesha kuthamini juhudi kubwa zinazochukuliwa
na Serikali kuwajengea miundombinu bora ya usafiri na kuwaondoshea usumbufu
waliokuwa wakiupata siku za nyuma.
Aidha, amewahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendeleza
ujenzi wa miundombinu ya barabara nchi nzima na kuwasisistiza kuunga mkono
juhudi hizo.
Rais Dk. Mwinyi amewathibitishia wananchi wa Mkoa wa Kusini
Unguja kuwamalizia barabara ya Tunguu - Makunduchi kwa kiwango cha njia nne
zenye taa kutoka Mwanakwerekwe hadi Makunduchi.
Akizungumzia tatizo la maji kwa mkoa huo, Rais Dk. Mwinyi,
amesema tayari Serikali imejenga skim nne kuu za maji safi ambazo zitamaliza
tatizo la maji mkoani humo.
Kuhusu tatizo la umeme mdogo katika mkoa huo, amesema Serikali
inatambua kwa muda mrefu kuwepo kwa tatizo hilo katika eneo hilo na kwamba
imeshanunua “Grid Stabilization” na amefarajika kusikia tatizo hilo limeanza
kupungua katika baadhi ya maeneo ya Mkoa huo.
Pia Dk. Mwinyi amemridhia ombi la Wananchi wa Kusini la
kujengewa daraja lililoombwa na wananchi wa mkoa huo, litalounganisha Mkoa huko
na wa Kaskazini Unguja lengo ni kurahisisha Mawasiliano baina ya mikoa miwili
hiyo na huduma nyengine za uchumi na jamii.
Alibainisha kuwa tayari msanifu amekamilisha michoro na
kuiwasilisha kwa Serikali kwa hatua za awali na kuwahakikishia wananchi kuwa
Serikali inasubiri kujua gharama ili hatimae kulijenga daraja hilo.
Akigusia sekta ya Elimu Rais Dk. Mwinyi amewaahidi wananchi wa
Zanzibar kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa skuli za ghorofa 26 unakuja na Mkoa wa
Kusini Unguja utakuwa miongoni mwao.
Mapema akiwasalimia wananchi wa Kijiji cha Charawe, Rais Dk.
Mwinyi amewasisitiza kutumia fursa za kuwepo kwa barabara hiyo kujinufaisha
kiuchumi nakuwaeleza kuwa itawarahisishia kusafirisha kwa wakati bidhaa
wanazozizalisha pamoja na kupata huduma nyengine kwa haraka.
Akizungmza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kufunguliwa kwa barabara hiyo ni
kichocheo cha kufungua fursa za kiuchumi Mkoani humo pia Serikali inakwenda
kutekeleza miradi mengine 162 katika sekta za maji, afya, elimu na barabara
nchi nzima kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid
Muhamed Salum, amesema, Zanzibar imeingia kwenye ramani ya dunia katika ujenzi
wa haraka wa miundombinu kutokana na juhudi na kazi kubwa zinazofanywa na Rais
Dk. Mwinyi ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya nane.
IDARA
YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment