Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba kuna
umuhimu mkubwa kwa taasisi na wadau mbali
mbali kufanya jitihada za kuvitangaza kwa ubunifu zaidi vivutio vya historia vilivyopo Mjimkongwe jambo litakalosaidia kukuza maendeleo ya sekta
ya biashara ya utalii katika mji huo na Zanzibar kwa jumla.
Mhe. Othman ameyasema hayo Ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokutana na Kamati ya Mandalizi ya Mashindano ya Marathon ya Kimataifa yanayotarajiwa kufanyika Jumaapili ijayo ya Novemba 3 mwaka huu.
Mhe. Othman
amesema kwamba mji huo una mambo mengi ya kihistoria ambayo hadi sasa
hayatangazwa ipasavyo kwa kufahamika na wageni pamoja na wenyeji kutokana na
kukosekana ubunifu wa kuyatangaza kwa wadau mbali mbali mambo hayo ya
kihistoria wakiwemo wageni.
Hivyo,
ameitaka Kamati hiyo na wadau wengine kuhakikisha kwamba wanakuwa wabunifu
kuyatafuta masuala muhimu katika mji huo yanayoweza kuwa kivutio cha utalii
kuyaingiza katika ubunifu wao ikiwemo mashindano kama hayo ya kimataifa ya
marathoni ambayo yatajenga uelewa kwa wenyeji na wageni na kuchangia ukuaji wa
biashara ya utalii katika eneo hilo.
Amesema
kwamba hatua hiyo ni muhimu pia katika kuithmani ipasavyo historia ya Zanzibar
ambayo, mbali na majengo yaliyopo ndani ya mji Mkongwe huo, lakini yapo
mambo mengi yanayohitaji kutangazwa zaidi
na kuweza kuleta manufua katika sekta ya utalii na Zanzibar kwa jumla.
Amesema
miongoni mwa mambo yanayohitaji kutangazwa ni pamoja na kuzifahamu na
kuzitangaza historia za majengo mbali mbali ya mji huo ambayo kimsingi
haifahamiki ipasavyo licha ya kuwa ni vivutio muhimu kutokana na kutotangazwa
ipasavyo .
Hivyo
amesema kwamba kupitia matamasha tofauti kunahaja na umuhimu mkubwa kuhakikisha
kwamba kunakuwa na juhudi za ubunifu wa kuutangaza mji huo pamoja na historia
yake ili iweze kuwa na manufaa zaidi katika kuendeleza biashara ya utalii hapa
Zanzibar.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mahindano ya Marathon Hassan Mussa, amesema
kwamba katika mashindano ya mwaka huu, kamati imejiongeza kwa kuutumia mji Mkongwe
kama kivutio cha utalii ambapo washiriki wa mbio hizo pia watapita katika
maeneo mbali mbali ya mji Mkongwe.
Aliyataja
maeneo hayo kuwa ni mtaa wa
Darajani kuelekea Kiponda, Hamamni ,Mkunazini,
barabara ya Soko Muhogo na
kumalizia maeneo ya Forodhani ambapo maeneo hayo kwa jumla yatakuwa ni urefu wa
kilomita moja ya ndani ya Mji Mkongwe kwa washiriki wote.
Hii ni
awamu ya nne ya kuwepo mashindano hayo ya marathoni ya kimataifa, ambapo kila
mwaka kunaongezwa ubunifu ikiwa ni pamoja na kupata ushiriki wa watu na
wanamichezo washuhuri kutoka nchi tofauti Afrika Mashiriki na duniani kwa
jumla.
Mwisho
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari, leo Jumatatu tarehe 28 Oktoba 2024.
No comments:
Post a Comment