RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar
inahitaji wadau zaidi kuungamkono juhudi za kuutunza, kuuhifadhi na kuuendeleza
Mji Mkongwe wa Zanzibar kutokana na umuhimu wake kwa Uchumi wa nchi.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo, Ikulu Zanzibar
alipozungumza na ujumbe kutoka Taasisi ya “International National Trust
Organization” ya Uingereza iliyomueleza mafanikio waliyoyapata katika
kulifanyia ukarabati jengo la “Custom House” liliopo Forodhani maarufu jengo la
Mizingani.
Amesema Mji Mkongwe mbali ya kuwa ni eneo
la Urithi wa dunia pia ni muhimu la kukuza Uchumi wa Zanzibar kupitia Sekta ya
Utalii kwani linalotembelewa na wageni wengi.
Dk. Mwinyi ameeleza kufarajika kwake na
juhudi na hatua zilizochukuliwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Jumuiya ya
Uhifadhi wa Mji Mkongwe (JUHUMKO) kwa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la
Mizingani.
Pia, amezisisitiza taasisi na wadau
wengine kujitokeza kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuyahifadhi maeneo ya urithi kwani Mji Mkongwe una majengo mengi yanayohitaji ukarabati
na kutunzwa kwa fedha na utaalamu.
Akizungumzia changamoto za mabadiliko ya
Tabianchi, ikiwemo kuongezeka na kina cha bahari, Meneja miradi wa Taasisi ya
“International National Trust Organization” amesema ni miongoni mwa changamoto
inayoikabili miji mingi ya urithi duniani iliyoko pembezoni mwa bahari kama
ilivyo kwa Mji Mkongwe wa Zanzibar, na kuahidi taasisi yake kuendeleza
ushirikiano na Zanzibar kuhakikisha Mji Mkongwe kubaki kwenye ramani ya dunia.
Ameeleza kuwa taasisi hiyo ina uzoefu kwa
nchi 102 duniani walizozifanyia ukarabati wa miji mikongwe.
Zaidi ya paundi 80,000 sawa na takriban Shilingi
milioni 240 zilitumika kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Mizingani chini ya
ufadhili wa Mfuko wa Baraza la urithi la Uingereza.
Ujumbe huo uliosheheni wataalamu wa
masuala ya uhifadhi wa miji ya urithi, Uliongozwa na Waziri wa Utalii na Mambo
ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga ulijumuisha taasisi za uhifadhi miji ya urithi
kutoka Uingereza, Jordan, Misri na Uganda.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment