Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kufungua Chomeo la Takataka ( incinerator) liliopo Vitongoji Wilaya ya Chake - Chake Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema mradi wa chomeo la taka ni miongoni mwa miradi muhimu kati kuondosha changamoto ya uwepo wa taka hatarishi ambazo zinapelekea kuhatarisha Afya ya jamii na kuharibu mazingira.
Ameyasema hayo katika ufunguzi wa chomeo la taka ( incinerator) lililopo Vitongoji Wilaya ya Chake - Chake Mkoa wa Kusini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema kuwa Mapinduzi ndio yaliyoleta ukombozi na uhuru kwa wazanzibari na kupelekea kupatikana kwa maendeleo yaliyopo nchini ikiwemo kuweka mazingira bora ya waafanya kazi pamoja na wananchi kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais amewataka Viongozi na watendaji wa Wizra ya Afya kulisimamia na kulitunza vizuri chomeo hilo la taka pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili waweze kuendana na Teknolojia inayotumika katika kuendeshea chomeo hilo.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ametoa wito kwa watendaji wa Wizara ya Afya kufuata miongozo itakayotolewa na wataalamu ili kuliwezesha chomeo hilo kudumu na kutumika kwa muda mrefu na kufikia malengo ya serikali ya kujenga chomeo hilo.
Nae waziri wa Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazurui amesema uwepo wa chomeo la taka kisiwani Pemba una lengo la kusaidia uhifadhi wa uchafu na taka hatarishi jambo litakalopelekea kuwa na ustawi bora wa afya za wananchi.
Mhe. Mazurui amesema taka taka zote hatarishi kisiwani Pemba zitakusanywa na kampuni ya West Environmental Compay Ltd, na kuchomwa kitaalamu bila ya kuathiri Mazingira, Afya za Binaadamu na Wanyama kutokana na kutuia Teknoloji ya kisasa, ubora wa chomeo hilo na taaluma itakayotumika katika kuchomea taka hizo.
Amewataka wamiliki wa hospitali binafsi, maduka ya madawa na maduka ya vipodozi kutoa ushirikiano katika kulitumia chomeo hilo ili kulinda Afya za wananchi na kuweka mazingira safi na salama.
Akitoa Taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema Mradi wa ujenzi wa chomeo la taka ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 uliozingatia viwango vya Kimataifa vya usimamizi wa taka ili kuhakikisha usalama wa mazingira na kuimarisha huduma za Afya kwa ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa.
Dkt. Mngereza amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamu kujenga chomeo la taka katika kijiji cha Vitongoji Pemba lililogharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.8 lenye lengo la kukabiliana na changamoto ya kutokuwa na chomeo la taka la uhakika kwa kipindi kirefu hivyo chemeo hilo litasaidia kuteketeza taka hatarishi zinazozalishwa maeneo mbali mbali ikiwemo Mahospitali, Viwandani, na Bandarini.
Amefahamisha kuwa Mradi wa Chomeo la taka umezingatia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira kwa kufunga mitambo ya kisasa yenye vifaa maalum vya kudhibiti hewa chafu(scrubing system )ambayo inasaidia uchujaji wa hewa na kuifanya hewa inayotoka kuwa katika kiwango cha himilivu.
Sambamba na hayo Dkt Mngereza amesema kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa kubwa ya kuimarisha huduma za Afya kwa wananchi pamoja na kuwasaidia watendaji wa Wizara ya Afya kufanya kazi za usimamizi na uteketezaji wa taka bila ya hofu ya kupata maambukizi ya magonjwa mbali mbali.
Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )
Leo tarehe 31 / 12 / 2024.
No comments:
Post a Comment