Na.Mwandishi Maalumu.
MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema maradhi
ya Saratani ni hatari na yanarejesha nyuma juhudi za jamii na uchumi hata
kusababisha umasikini kwa jamii kutokana na gharama kubwa za matibabu yake kwa wagonjwa
wengi kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu.
Mama Mariam kwa huzuni ameyasema hayo Ofisini kwake Ikulu ya Migombani,
Mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza na wageni kutoka Hong Kong, Dk. Jeremy
Hon, Daktari na Mtaalamu wa maradhi ya Saratani akiambatana na Bi. Angel Hon wa
Taasisi ya Belt and Road Creation Resources waliofika kumtemelea.
Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya
Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF),
aliwaeleza wageni hao jinsi wanavyofanyakazi na kuwa karibu na jamii kwa
kuwashajihisha watu kuimarisha afya zao ili kujiepusha na maradhi
yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, presha na moyo.
Aidha, Mama Mariam aliueleza ugeni huo kwamba ZMBF katika
kuisaidia jamii juu ya maradhi hatari ikiwemo Saratani taasisi yake mara kadhaa
imekuwa na utaratibu wa kila baada ya miezi mitatu kuweka kambi za matibabu
bure Unguja na Pemba kwa Mikoa yote kuisadia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wakuu wa Mikoa kuwaalika wananchi kwaajili
ya matibabu na uchunguzi wa afya zao.
Amesema, kambi hizo zimesaidia kugundulika kwa kesi nyingi
zikiwemo Saratani za matiti zinazowasumbua kina mama wengi pamoja na maradhi
mengine.
Mama Mariam amemualika Dk. Jeremy Hon kuangalia uwezekano wa
kuja Zanzibar kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwani Serikali
tayari imekamilisha hospitali 10 za Wilaya Unguja na Pemba na moja ya Mkoa
pamoja na kuweka miundombinu imara na vifaa vya kisasa vya maabara.
Pia, Mama Mariam Mwinyi amewaeleza wageni hao jitihada za ZMBF
kuishajihisha jamii kufanya mazoezi kwa kuungana nao mara kadha kwenye
matembezi ya hiari ili kuimarisha afya zao sambamba na kuisajihisha jamii juu
ya umuhimu wa lishe bora kwa mama wajawazito na watoto.
Akiuzungumzia mradi wa "Tumaini kit” unaozalisha taulo za
kike kwa ajili ya hedhi salama kwa wasichana kupitia kiwanda chake kilichopo
Mnara wa mbao, Mama Mariam Mwinyi aliwaeleza wageni wake hao lengo la mradi huo
ni kutatua changamoto za hedhi kwa wanafunzi wa kike zinazorudisha nyuma maendeleo
yao ya elimu kwa Unguja na Pemba.
Ameeleza kupitia mradi wa "Tumaini kit” umewasaidia
wasichana wengi hasa wa vijijini kuhudhuria skuli na kufanya vizuri kwenye
masomo yao ambao awali wengi waliacha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo
kutomudu gharama za kujikimu kila wanapopata ada za mwezi.
Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amebainisha kuwa “Tumaini
Initiative” umelenga kuzalisha taulo za kike zaidi ya 20,000 kwa mwaka na hadi
sasa tayari ZMBF imefanikiwa kusambaza kwa wanafunzi na wasichana zaidi ya
7000 wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.
Katika hatua nyengine Mama Mariam Mwinyi aliueleza ugeni huo
umuhimu wa kutumia mwani kiafya na kiuchumi na kusema kuwa taasisi yake ya ZMBF
inawaungamkono wakulima wengi wa mwani amba oni kinamama kwa kuwasaidia mbinu,
vifaa na kuwawezesha kuvuna mwani wenye ubora wa lengo la kujipatia soko imara
la zao na bidhaa zinazotokana na mwani.
Kwa upande wao Dk. Jeremy Hon na Mrs Angel Hon wamepongeza
juhudi za maendeleo na kazi nzuri inayofanywa na “Zanzibar Maisha Bora
Foundation” ya kuhakikisha wasichana wa Zanzibar hasa wa vijijini wanakua
salama muda wote wanapokuwa kwenye ada zao za kila mwezi.
Pia wameeleza shauku yao ya kutaka kuendeleza ushirikiano wao na
Zanzibar hasa katika kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya Afya ili kupunguza
wimbi za maradhi ya Saratani yanayowasumbua wananchi wengi.
Naye, Ofisa Mkuu wa Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation”
(ZMBF), Fatma Fungo ameueleza ugeni huo kwamba taasisi hiyo mara nyingi imekua
na programu za nje ya taasisi kwa lengo la kuifikia na kuwa karibu na jamii kwa
kutoa elimu na kushajihisha jamii masuala mbalimbali ya Afya ikiwemo umuhimu wa
hedhi salama kwa wanafunzi, wazazi, viongozi wa Serikali za mitaa, Wakuu wa
Mikoa na Wilaya kwa maeneo yote wanayoyatembelea.
Aidha, amesema kupitia programu za kambi za matibabu tayari
wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu 17, 000 na kubaini kesi mbalimbali
zinasowasumbua kiafya na kupatiwa matibabu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya
na mdaktari kutoka China, aidha, kwa kesi za ugawaji wa taulo za hedhi salama, amesema
ZMBF imekua ikishirikiana kwa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali.
Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) iliasisiwa
Julai mwaka 2021 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka 2022.
“Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) inafanya kazi kwa
karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara
ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
IDARA YA
MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment