Habari za Punde

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA KIUYU MINUNGWINI MKOA WQA KASKAZINI PEMBA

Muonekano wa Jengo la Kituo cha Afya Kiuyu Minungwini Mkoa wa Kaskazini Pemba, lililowekwa Jiwe la Msingi la Ujenzi huo na Makamu wa Pili wa Rais wa Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, ikiwa ni shamrashamra za Maadhmisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiweka  Jiwe la Msingi la Kituo cha Afya Kiuyu Minungwini Mkoa wa kaskazini Pemba ikiwa ni katika shamra shamra za miaka 61 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka Uogozi wa Wizara ya afya pamoja na wakandarasi wanaojenga kituo cha Afya cha Kiuyu Minungwini kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unakamilika ndani ya kipindi kifupi ili wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani waendelee kufaidika na matunda ya mapinduzi.

Ameyasema hayo wakati akiweka  Jiwe la Msingi katika Kituo cha Afya Kiuyu Minungwini Wila ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema ni lazima Mkandarasi wa ujenzi wa kituo hicho kufanya  jitihada za ziada katika kuhakikisha anamaliza na kukabidhi jengo hilo kwa wakati  ili wananchi wa Kiuyu Minungwini na maeneo jirani waweze kupata huduma ya Afya karibu na maeneo yao.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali inawekeza fedha nyingi katika Sekta ya Afya kwa kujenga na  kuboresha miundombinu ya Afya pamoja na kununua vifaa vya kisasa kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi ikIwa ni adhma ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Mhe.Hemed amewataka wananchi kushirikiana katika kuyalinda na kuyatetea Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyomkomboa Mzanzibari kutoka katika makucha ya kikoloni ambao hawakuwa na nia njema na Zanzibar.

Sambamaba na hayo amewataka wananchi wa Kiuyu Minungwini na maeneo mengine kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu inayoendelea kujengwa katika maeneo yao na kuacha jazba zinazopelekea uharibifu wa miundombinu hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Zanzibar, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Rais Dkt.Hussein Mwinyi imejenga hospitali za Wilaya na Mkoa kisiwani Pemba ambazo zimezingatia ubora na viwango vya kitabibu ikiwemo kuweka madaktari bingwa, kuwepo kwa huduma ya  ICU, huduma za mionzi, upasuaji, usafishaji damu na nyenginezo ili kuimarisha huduma za matibabu Kisiwani humo.

Mhe. Hafidh amesema Wizara ya Afya itaendelea kubuni miradi mbali mbali ya maendeleo katika sekta ya Afya kwa ustawi na upatikanaji wa huduma bora za Afya na kwa wakati kwa wananchi wa Unguja na Pemba.

Akitoa  Taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Afya cha Kiuyu Minungwini, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema kwa muda mrefu wananchi wa Kiuyu Minungwini na vijiji jirani wamekuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za Afya hivyo kumalizika kwa Ujenzi wa kituo hicho kutaondoa changamoto hio na kuwanufaisha wananchi wa Minungwini na maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dkt Mngereza amesema ujenzi wa kituo cha Afya cha Kiuyu Minungwini cha ghorofa moja(G+1) kinachojengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo hadi kumalizika kwake kitagharimu zaidi ya  shilingi za Kitanzania Bilioni 1.7 na kitawanufaisha wananchi wote wa Mkoa huo.

Amesema kuwa kituo hicho cha Afya kinatarajiwa kutoa huduma mbali mbali za kitabibu ikiwemo huduma ya mateniti, huduma ya mama na mtoto, huduma ya mionzi, huduma ya meno, upasuaji mdogo na nyenginezo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

30 / 12 / 2024

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.