Na. Benny Mwaipaja
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Victoria Kwakwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anaye simamia masuala ya Utawala, Bi. Anna Bjerde, Jijini Dar es Salaam, Kando ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaohusu nishati, ambapo pamoja na mambo mengine, Mhe. Dkt. Nchemba aliwaeleza wageni wake kuwa Tanzania inahitaji zaidi ya dola za Marekani bilioni 12.9 zikiwemo dola za Marekani bilioni 4.04 kutoka Sekta Binafsi kwa ajili ya kuwekeza kwenye eneo la uzalishaji nishati nchini.
Katika kikao hicho kilichomhusisha pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Naibu wake, Bi. Amina Hamisi Shaaban, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza na Viongozi wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Dkt. Nchemba alieleza kuwa kiwango hicho cha fedha kitaiwezesha Tanzania kufikia uzalishaji wa nishati kwa asilimia 75 ifikapo Mwaka 2030 na kiwango cha asilimia 80 cha matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo Mwaka 2034 na kutimiza lengo la kufikisha asilimia 65 ya nishati mchanganyiko itakayowezesha nchi kuzalisha Megawati 1,800 za umeme kwa njia ya umeme jua, upepo, joto ardhi na umeme wa kutumia nguvu ya maji.
Mwisho
No comments:
Post a Comment