Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Aziza Idd Suwed amewataka wananchi wa Wilaya ya Magharibi ‘B’ waliotimiza vigezo kujitokeza kuandikisha katika daftari la wapiga kura awamu ya ya pili linalotarajiwa kuanza kesho Mach 4 ili kupata haki ya kupiga kura.
Wito huo ameutoa skuli ya Regeza Mwendo Mwera Wilaya ya Magharibi A, wakati akitembelea vituo vya kuandikisha wapiga kura Wilayani humo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea vituo vya uandikishaji wa daftari la wapiga kura.
Amesema kuwa Tume ya Uchaguzi inaendelea na zoezi la kutembelea vituo hivyo kwa lengo la kuangalia hali ya uandikishaji inavyendelea pamoja na kuangalia changamoto zilizopo ili kuwaondoshea usumbufu wananchi .
Aidha ameeleza kuwa wananchi wamehamasika kujitokeza kujiandikisha katika daftari hilo na bado wanaendelea kuwasisitiza wapiga kura katika Wilaya zilizobakia kufika kwa wingi kwenye vituo vya uandikishaji ili kupata haki yao ya msingi.
Nao Mawakala na Wakuu wa Vituo vya kuandikisha wamesema kuwa vituo vipo katika hali ya usalama hakuna tatizo lolote na wananchi wanaendelea kujitokeza na kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Kwa upande wao wananchi waliyojiandikisha katika daftari hilo wamesifu utaratibu unaotumika na zoezi linaendelea vizuri hakuna matatizo kila mwenye sifa ya kuandikishwa anapata fursa hiyo na zoezi hilo linatarajiwa kukamiliika leo Wilayani humo.
No comments:
Post a Comment