Habari za Punde

RASIMU YA AWALI YA KUKABILIANA NA MAAFA

Na Maelezo Zanzibar.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Islam Seif amesema kuwepo kwa mpango mkakati wa kukabiliana na maafa ni dhamira kuu ya kuhakikisha taifa linaimarika katika utayari, uimara na ustahamilivu dhidi ya maafa yanayoweza kutokea nchini.

Ameyasema hayo katika Ukumbi Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni katika Kikao cha Uthibitishaji wa Rasimu ya awali ya Mpango mkakati wa Kukabiliana na maafa wa mwaka 2025-2029 amesema nchi inahitaji mikakati ya muda mrefu, madhubuti inayotekelezeka ili kupunguza athari kabla hazijatokea.

Amesema kumekuwa na ongezeko la matukio ya maafa ya asili na yale yanayosababishwa na binadamu yakiwemo mafuriko, matetemeko ya ardhi, vimbunga na, maradhi ya mripuko ambapo vichocheo vya maafa hayo ni mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu mijini, uharibifu wa mazingira na migogoro ya kijamii na kiuchumi ambayo yamezidi kuongeza hatari ya kuathiriwa  na maafa hayo.

“Kutokea kwa maafa mbali mbali kunatufundisha kuwa hatuwezi tena kuendelea kukabiliana na maaafa kwa njia ya dharura pekee pale yanapotokea tunahitaji mipango mikakati ya muda mrefu, madhubuti na inayotekelezeka ili kupunguza athari kabla hazijatokea”, ameeleza Katibu huyo.

Dkt. Islam amefahamisha kuwa mkakati huo uliofanyiwa mapitio umezingatia tathmini ya mazingira na viashiria vya maafa vilivyopo na vinavyoendelea kujitokeza, ushirikishwaji wa wadau wa sekta husika katika ngazi zote na tathmini ya utekelezaji wa mipango iliyopita na mafunzo yaliyopatikana.

Aidha ameeleza kuwa mpango mkakati huo wa miaka mtano umejika kuimarisha uwezo wa kitaasisi na kijamii katika kujiandaa na kukabiliana na maafa, kuweka mifumo madhubuti uratibu na usimamizi wa maafa, kuboresha mifumo ya tahadhari za mapema na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati pamoja na kujenga uwezo wa kitaifa na kijamii katika kurejesha hali baada ya maafa.

Dkt. Islam amezisistiza taasisi zinazotekeleza mpango mkakati huo kuutekeleza kwa vitendo ili ulete ufanisi na tija, kuufuatilia na tathmini za kila mwaka juu utekelezaji wake pamoja na kuwa ushirikiano wa karibu katika ya Serikali , sekta binafsi, jamii na wadau wa maendeleo.

Akiwasilisha rasimu ya awali ya mpango mkakati wa kukabiliana na maafa ya mwaka 2025-2029 Mshauri Elekezi Abdalla Bakar Hamad amesema mpango huo unalengo la kuiwezesha Kamisheni ya Kukabiana na maafa kuepusha maafa na kuijenga jamii kuwa vumilivu na kuweza kukabiliana na majanga yote ya kimaumbile na kibinadamu.

Aidha amewashauri watekelezaji wa mpango huo kuufuata na kuutumia ipasavyo ili jamii ibaki salama bila ya athari za majanga yoyote nchini.

Nao washiriki wa kikao hicho wamesema watahakikisha kuwa 

mpango mkakati wa kukabiliana na maafa unatekelezeka 

watafuata mikakati iliyowekwa na kufuata sheria kwa kutoa 

tahadharisha na kuelimisha jamii kuhusiana kujikinga na kuepukana na maafa ili yasitokezee.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.