Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Ziarani Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitoa maelekezo kwa mshauri elekezi Mhandisi Said Maliki anaesimamia ujenzi wa dakhalia mbili zinazojengwa katika skuli ya Sekondari Mauwani Kiwani Pemba mara baada ya kukagua ujenzi huo.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na ujenzi wa dakhalia unaoendelea katika skuli ya sekondari Mauwani iliyopo Kiwani mkoa wa KusiniPemba.


Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo inayojengwa katika wilaya ya Mkoani.

Alisema kukamilika kwa ujenzi wa dakhalia mbili zinazojengwa katika skuli hiyo, kutatoa fursa kwa zaidi ya wanafunzi 500 wanawake na wanaume kupata nafasi ya kusoma kwa utulivu hatua ambayo itasaidia kuwaondolea changamoto wanafunzi ya kutembea masafa ya mbali.

Amewataka wakandarasi na washauri elekezi wa ujezi wa dakhalia hizo kuhakikisha wanaharakisha ujenzi wa maeneo yaliyobakia ili kutoa fursa kwa wanafunzi hao kuendelea na masomo yao wakiwa na uhakika wa makaazi bora na salama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, ametoa agizo kwa wakandarasi hao kujenga uzio katika eneo lote linalozunguka dakhalia hizo ili kuziweka katika hali ya usalama.

Kwa upande wake mshauri elekezi kutoka wakala wa majengo Zanzibar (ZBA) Mhandisi Said Malik, amesema ujenzi wa dakhalia hizo unatarajiwa kukamilika mwezi September mwaka huu ambapo utajumuisha vyumba 24 vya makaazi, ofisi mbili, vyoo, kumbi mbili za kulia na maeneo ya kufulia kwa wanafunzi watakaoishi hapo.

Mhandisi Said amesema dakhalia hizo zinajengwa na mkandarasi Mwinyi Building Contract hadi kumalizika kwake inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 6 za ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Akiwa katika ziara hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, amekagua ujenzi madara katika skuli ya maandalizi na msingi Nanguji ambapo aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanamaliza kwa wakati ujenzi wa madarasa hayo pamoja na kuweka sawa maeneo yote yanayozunguka skuli hiyo ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi ya kusomea na kufundishia.

Amewataka wananchi wanaokaa karibu na skuli hio kushirikiana katika kuyatunza na kuyalinda na uvamizi maeneo yaliyopo karibu na skuli ili kuepusha usumbufu wakati yatakapohitajika kwa ajili ya utanuzi na ujenzi wa miundombinu mbali mbali skulini hapo.

Nae Mratibu wa Tasaf Pemba, Mussa Ali Kisenge, amesema ujenzi huo wa madarasa sita yenye miundombinu ya kisasa unaojengwa kwa ufadhili wa Tasaf utakaogharimu zaidi ya milioni 180 na kutarajiwa kumaliza mwezi Agosti mwaka huu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemkabidhi mwalimu mkuu wa skuli ya Sekondari Kiwani shilingi milioni 5 ambazo zitatumika kwa mahitaji ya wananfunzi waliopatwa na changamoto ya kuunguliwa kwa darasa moja katika skuli yao.

Pamoja na miradi hiyo Makamu wa Pili wa Rais amekagua ujenzi wa kituo cha kununulia karafuu Kiwani, ukarabati wa ujenzi wa skuli ya Sekondari Kiwani, kukagua ujenzi wa madarasa katika skuli ya Msingi Chwaka na kukagua eneo linaloathiriwa na maji ya bahari Mtangani Pemba.






Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 30. 06.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.