Habari za Punde

NAIBU WAZIRI UMMY AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUGHARAMIA MAZISHI WALIOFARIKI SAME

Na Mwandishi Wetu - KILIMANJARO

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa upendo  kwa kugharamia mazishi ya  miili  42 ya watu waliofariki dunia kufuatia  ajali iliyotokea  Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Mhe. Nderiananga ametoa shukrani hizo  tarehe 03 Julai, 2025 wakati aliposhiriki tukio la kuaga miili 35 katika viwanja vya Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) akisema miili Saba ilichukuliwa na ndugu zao na miili miwili bado vipimo vya DNA vinafanyiwa kazi ili kutambulika.

Tukio hilo lilioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Nurdin Babu ambapo Mhe. Nderiananga alimpongeza kwa kujitoa kwa kiasi kikubwa tangu ilipotokea ajali hiyo akishirikiana na watendaji wake wote.

Amesema Serikali  kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro kwa juhudi kubwa zilizofanyika kuokoa manusura wa ajali hiyo pamoja na miili ya walioungua kwa moto mara baada ya ajali kutokea.

Vilevile ameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuchukua  sampuli za miili hiyo (DNA)  kuhakikisha ndugu wanatambua miili ya wapendwa wao.

Hata hivyo  Mhe. Nderiananga ameendelea kutoa pole kwa Serikali, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia msiba huo mzito kwa Taifa  huku akiwaomba kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu hadi watakapokamilisha kuwahifadhi wapendwa wao. 

Aidha, ajali hiyo iliyotokea Juni 28 2025 katika Kitongoji Mahuu, Kata ya Same, takribani kilomita nne kutoka Same mjini, ililihusisha basi kubwa la abiria, Mali ya Kampuni ya Chanel One, lenye namba za usajili T 179 CWL na basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster, lenye namba T 199 EFX linalomilikiwa na Kampuni ya Mwami Trans.



Coaster hiyo, ilikuwa ikitokea Same kuelekea Manispaa ya Moshi, wakati basi la Chanel One lilikuwa likitokea Arusha kuelekea Tanga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.