Habari za Punde

WATUMISHI WA UMMA KIBAHAWatumishi watakiwa kutunza heshima za taasisi zao.

 

Na.Mwashamba Haji Juma

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanatunza, kulinda na kukuza heshima ya taasisi wanazozifanyia kazi pamoja na Serikali kwa ujumla.

Bw. Maswi ameyasema hayo alipofunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya na wale waliohamia Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, yaliyofanyika ukumbi wa Ali Hasan Mwinyi uliopo Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani Julai 3, 2025.

Aidha, amewataka watumishi hao kuzingatia nidhamu kazini, ushirikiano na kufanya kazi kwa uaminifu ili kusaidia wananchi kupata huduma iliyobora.

“ Nategemea mtakuwa na nidhamu ya kipekee kwani Serikali inawataka mutimize majukumu yenu kwa wakati na kwa nidhamu thabiti mkishirikiana kutekeleza maagizo” Alisema Katibu Mkuu Maswi.

Bw. Maswi pia alisisitiza umuhimu wa watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Vilevile, alieleza taasisi za Serikali hupimwa kwa vitendo na mienendo ya watumishi wake, hivyo, kila mtumishi anawajibika kuhakikisha anakuwa mfano wa kuigwa katika kazi, mienendo na mawasiliano ya ndani na nje ya taasisi yake.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi  Rasilimali watu, wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Gabriel Robi amewasihi watumishi hao kuyafanyia kazi kwa vitendo  mafunzo waliyoyapata, pia  yakawe chachu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majumu yao.

Akitoa shukurani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Bw. Evalist Mashima ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuhakikisha watumishi  wamepata uelewa wakutosha kuhusu utumishi wa umma.

Mafunzo hayo yalianza Julai 01, 2025 kwa kuwasilishwa mada mbalimbali zilizohusu sheria na miundo ya utumishi wa umma ambayo yalihudhuriwa na watumishi wa umma wapatao 73 wakiwemo 39 kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.