Na.Mwashamba Haji Juma
Katibu Mkuu
Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi, amewataka watumishi wa umma
kuhakikisha wanatunza, kulinda na kukuza heshima ya taasisi wanazozifanyia kazi
pamoja na Serikali kwa ujumla.
Bw. Maswi
ameyasema hayo alipofunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya na wale
waliohamia Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora, yaliyofanyika ukumbi wa Ali Hasan Mwinyi uliopo Chuo cha Uongozi
cha Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani Julai 3, 2025.
Aidha, amewataka
watumishi hao kuzingatia nidhamu kazini, ushirikiano na kufanya kazi kwa
uaminifu ili kusaidia wananchi kupata huduma iliyobora.
“ Nategemea
mtakuwa na nidhamu ya kipekee kwani Serikali inawataka mutimize majukumu yenu
kwa wakati na kwa nidhamu thabiti mkishirikiana kutekeleza maagizo” Alisema
Katibu Mkuu Maswi.
Bw. Maswi pia
alisisitiza umuhimu wa watumishi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu
na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Vilevile, alieleza
taasisi za Serikali hupimwa kwa vitendo na mienendo ya watumishi wake, hivyo,
kila mtumishi anawajibika kuhakikisha anakuwa mfano wa kuigwa katika kazi,
mienendo na mawasiliano ya ndani na nje ya taasisi yake.
Naye, Mkurugenzi
Msaidizi Rasilimali watu, wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,
Bw. Gabriel Robi amewasihi watumishi hao kuyafanyia kazi kwa vitendo
mafunzo waliyoyapata, pia yakawe chachu na kuongeza ufanisi katika
utekelezaji wa majumu yao.
Akitoa shukurani
kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Bw. Evalist
Mashima ameishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuhakikisha watumishi
wamepata uelewa wakutosha kuhusu utumishi wa umma.
Mafunzo hayo
yalianza Julai 01, 2025 kwa kuwasilishwa mada mbalimbali zilizohusu sheria na
miundo ya utumishi wa umma ambayo yalihudhuriwa na watumishi wa umma wapatao 73
wakiwemo 39 kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
No comments:
Post a Comment