Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Ndg. Stephen Wasira akizungumza na viongozi wa CCM wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu,Oktoba 18, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Bariadi
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema nchi ipo salama, wananchi wakumbushwe na kuhamasishawa kuwapigia kura wagombea wenye sifa ambapo kwa upande wa urais ni Dk. Samia Suluhu Hassan anayetokana na CCM.
Amesema zipo propaganda chafu katika mitandao ya kijamii lakini yanayooelezwa ni upotoshaji, hayana ukweli kwa lengo la kupotosha umma.
Makamu Mwenyekiti Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu, LEO.
"Wako watu katika nchi yetu ambao wanakerwa na amani na wanashirikiana na watu wa nje kutaka kuwavuruga.
"Siku hizi kuna mitandao ya kijamii inapeleka habari za uongo, kutisha na kuwafanya watu wafikiri kuna shida, mimi, nakuja kuwaambia nchi ipo salama kabisa, nchi yetu iko salama na zimebaki siku 10 twende tukapige kura," alisema.
Alisisitiza viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi mapema asubuhi siku ya kupiga kura watimize haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaofaa.
"Nimekuja kuwaambia nendeni muwaambie Watanzania wenzetu tangu shina wajitokeze kwa wingi waende wapige kura kwa sababu mamlaka ya nchi yapo mikononi mwao, na ndio wakati wao wa kukabidhi madaraka haya kwa watu wanaowaamini," alielekeza.
Wasira alifafanua kuwa, wananchi wanapaswa kuchagua viongozi wenye weledi, uadilifu na uaminifu katika kuwatumikia Watanzania.
"Hawapeleki tu madaraka mtu anapita anasema mnipe mimi lakini hawakujui, huna rekodi nao chama chako chenyewe ni cha siku moja tu...mnawezaje kuakabidhi madaraka kwa chama ambacho hamkijui, kwa watu ambao hamuwajui wala hamna hakika nao, hapana," alisema
Alieleza kuwa, Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikifika kwa Watanzania kila baada ya miaka mitano, kinawaeleza mipango ya maendeleo na kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.
"Kazi yetu sisi kila baada ya miaka mitano tunawaambia Watanzania tumefanya nini, tunawaambia tutafanya nini, ndicho chama ambacho sifa yake ni kuahidi na kutekeleza, ndicho chama cha mapinduzi kinaahidi halafu kinatekeleza na ushahidi tunao.
"Kwa mfano katika Wilaya ya Bariadi kwa miaka minne na nusu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tumejenga shule za msingi 10 kwa sababu ya ongezeko la watoto, yamejengwa madarasa ya shule za msingi 81 na nyie hamkuchangishwa, sekondari nane mpya zimejengwa katika wilaya ya Bariadi (mjini na vijijini).
"Madarasa mapya yamejengwa mazuri 143 na hatukuchangishwa ni kodi yetu tu inasimamiwa vizuri na Samia, inajenga...tunaahidi na tunatekeleza na hiyo ndiyo tofauti kati ya chama chetu na vyama vingine," alisisitiza.
MITANO IJAYO
Akizungumzia ahadi ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 kwa miaka mitano ijayo, itatatua changamoto za wananchi wa Bariadi katika sekta mbalimbali.
Akitoa mfano, alisema ilani hiyo imeahidi kufikisha maji zaidi kwa watu wa Bariadi na kwamba tayari jitihada zimeanza kufanyika kwa vitendo.
"Tumeanzisha mradi siyo tunasema tu, matenki yamejengwa 'inteki' kutoka Ziwa Victoria kuja Bariadi mpaka Meatu yatafika, mpaka Kisesa yatafika mpaka Maswa yatafika, mkoa mzima utapata maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria," alisema.
Mbali na maji alisema changamoto ya umeme nayo itafanyiwa kazi kwa kujenga kituo cha kupoza na kusambaza nishati hiyo kuondoa tatizo la kukatikakatika.
No comments:
Post a Comment