6/recent/ticker-posts

KUTUWA KWA DHARURA NDEGE UCHUNGUZI UNAHITAJIKA ILI KUEPUSHA MAAFA.


Na Mwantanga Ame

ZANZIBAR jana ilipatwa na tukio la pili la kutua kwa dharura ndege ndogo katika vijiji vya Unguja ambapo hapo awali liliwahi kutokea tukio la kuanguka kwa ndege ndogo baharini iliyokuwa na watu watatu akiwemo mtu na mkewe.

Kutua huku kwa dharura kwa ndege hizi kumefanya matukio hayo kuwa matatu na tayari sehemu ya jamii imeanza kupatwa na mashaka kutokana na kuonekana matukio haya kuanza kuongezeka ingawa hadi sasa hakuna aliepoteza maisha.

Baya zaidi ambalo jamii inazidi kupatwa na hofu nayo ni aina ya ndege hizo zinazoanguka kuwa ni zile ndogo ambazo ni moja ya sehemu kubwa ya usafiri unaotumiwa na wananchi katika shughuli zao za kawaida, kibiashara na matembezi.

Kama hilo halitoshi jengine ambalo wananchi wanapatwa na mashaka juu ya matukio hayo ni kuona ndege hizo pale zinapopata hitilafu hulazimika kutua katika barabara za vijijini kama ile ya mwanzo ilipotua katika kijiji cha Kiwengwa na sasa kijiji cha Mtende ambapo wakazi wake ni nadra sana kuona vitu kama hivyo.

Ingawa hayo yameshatokea lakini kinachohitajika sasa kufanyika kwa utafiti ama uchunguzi ni kwanini ndege hizi zimekuwa zikitafuta dharura kila mara na pia baada ya kuliangalia hilo inapaswa kufikiria jee usafiri wa kutumia ndege hizo bado unahitaji kuwepo kwa viwango viliopo sasa.

Hili ni moja ya jambo la msingi ambalo linahitaji kuangaliwa kutokana na kuanza kujionesha mengi ya matukio yanayojitokeza hivi sasa yananasibishwa na hitilafu za ingini huku wengine wakieleza kuwa kampuni zinazotoa huduma za usafiri wa anga hutumia ndege zisizo na viwango ama uendeshaji makampuni hayo hufanywa kama duka la mtu binafsi kwamba leo anatamani kuuza vyungu kesho analigeuza na kuuza vitambaa.

Hii ni kutokana na kile kilichowahi kujitokeza ni katika mijadala mbali mbali kwa baadhi ya watendaji kuwalalamikia wamiliki wa vyombo vya usafiri wa anga kutoendesha taasisi zao katika viwango vya kimataifa kama sekta hiyo inavyotaka.

Mfano halisi wa baadhi ya madai hayo yaliowahi kulalamikiwa ni juu ya utaratibu wa utendaji kazi wa marubani kwa kukataa kuajiri marubani wa kutosha na badala yake kulazimika kurusha ndege wakiwa na rubani mmoja bila ya kuwepo wa akiba jambo ambalo ni la hatari pindipo rubani huyo akipatwa na dharura zikiwemo za chombo ama afya kutetereka.

Hili ni moja kati ya mengi ambayo watendaji katika sekta hiyo waliliweka bayana kwa vile lilikuwa likakiukwa viwango vya kimataifa katika sheria za anga lakini lipo na limekuwa likitendwa na baadhi ya wamiliki wa vyombo hivi vya usafiri wa anga.

Sababu kubwa ambazo wamiliki hao wameonekana kuzitoa ni juu ya kukimbia gharama za kuajiri marubani wengi katika huduma zao kwani rubani mmoja hulazimika kumgharimu malipo ya mshahara wake sichini ya shilingi milioni 2/= na ndege inayobeba abiria zaidi ya 10 ni lazima iwe kepteni na injinia na wasaidizi wengine.

Kutokana na mzigo huo wa watumishi kuna baadhi ya makampuni huwa na ndege zaidi ya 10 ambazo zinahitaji kuwa na idadi hiyo hiyo ya watumishi ama ziada wakiwemo watendaji katika ngazi ya utawala jambo ambalo husababisha kuwapo kwa idadi kubwa ya watumishi.
Kuwapo kwa hali hiyo ni moja ya chanzo kikubwa ambacho kimewafanya wamiliki wengi waliojitumbukiza katika biashara hizi kujikuta wakiendesha makampuni hayo vile wapendavyo.

Hali hii inawezekana kabisa ikawa ni moja ya matatizo ya kuwapo kwa mlolongo wa ndege zinazotoa huduma zenye viwango visivyoridhisha zinazomilikiwa na makampuni hayo huku nyengine zikiwa zikiendeshwa kama vile ni usafiri wa nchi kavu.

Mfano wa hilo ni pale inaposhuhudiwa baadhi ya abiria kufika katika viwanja vya ndege kwa muda waliopangiwa lakini wakajikuta wanashindwa kuondoka baada ya kuripotiwa kunafanyika marekebisho ama idadi ya abiria imezidi huku wengine wakipewa taarifa za ndege kuondoka saa 10 wakajikuta wanaongezewa na nusu saa ukiuliza sababu unaambiwa anasubiriwa mtu.

Ingawa yapo mengi katika sekta hii hasa kwa wamiliki wa ndege ndogo, lakini ipo haja kwa Mamlaka husika ikaanza kutanabahi na hilo kwa kulifanyia kazi ili kuepusha kutokea makubwa zaidi kwani leo zinatua katika uziri wa barabara za lami zilizojengwa na serikali ya mapinduzi ya zanzibar lakini kesho Mungu aepushe mbali hitilafu hizi zikitokea zinaweza zikatua katika mapaa ya nyumba za wananchi.

Suala la msingi kwa Mamlaka husika ni kuona kuwa uchunguzi wanaozifanyia ndege hizi kabla ya kuwapa leseni unakuwa ni wakina kwa kutambua ubora wake kama bado zinafaa kutumika kwa huduma za jamii ama laa na kama zinahitilafu basi wasisite kuzichukulia hatua kwa kufuta leseni zao.

Nasema hivi kwani haiwezekani kuona ni kampuni zinayopatwa na matatizo ya aina hii huwa ni zile zile inazojirudia kila baada ya muda kulikoni wakati kila mwaka unaambiwa hufanyiwa ukaguzi, sasa hapa isiwe wakati wa ukaguzi ndio mambo hubadilishwa na baada ya ukaguzi kukawana mbiruo wa mambo kama inavyoshuhudiwa kwa madereva wa magari ya abiria anapoenda kupasisha gari honi hutiwa mpya na viti huoshwa lakini baada ya siku mbili vyote havipo.

Sasa basi ipo haja kwa mamlka husika ikaanza kuliona hilo kwa kuhakikisha sheria ya marubani inafuatwa kwa kutotoa leseni kwa mmiliki yoyote wa usafiri wa anga ikiwa atabainika kushindwa kutekeleza masharti yaliomo katika sheria pamoja na kuwa na vyombo vya usafiri huo vilivyobora.

Kinga bora kuliko tiba.

Post a Comment

0 Comments