SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema nyumba ya kulelea watoto yatima Mazizini inamilikiwa na Jumuiya ya ZAYEDESA na ya Forodhani itabakia kuwa nyumba ya Serikali.
Hayo aliyasemwa barazani jana na Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Zainab Omar wakati akijibu swali la Salmin Awadh Salmin (Magomeni), aliyehoji Mmiliki wa jengo hilo la Mazizini na je kama yapo makubaliano kati ya Serikali na ZAYEDESA iliyojenga.
Waziri Zainab alisema nyumba hiyo imejengwa na ZAYEDESA na ndio wamiliki halalali, ambapo Serikali inaendelea kuwatunza watoto hao.
Alieleza kuna hati ya makubaliano ambayo imetayarishwa na ZAYEDESA na kuletwa Wizarani kwa kupitiwa, ambapo tayari imeshapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushauri wa kisheria ili baadae pande zote mbili ziweze kutia saini.
Hata hivyo, alisema katika jibu la swali la nyongeza, alifahamisha kuwa, ZAYEDESA imejenga nyumba hiyo kwa nia ya kuwasaidia watoto hao waishi katika mazingira mazuri kwa vile la Forodhani lilikuwa na ufinyu wa nafasi.
Alisema ZAYEDESA hawana nia wala lengo la kufanya mizengo ya tamaa ya kubadilika katika kuishi watoto hao Mazizini hapo baadae isipokuwa wanachohimiza ni usafi na matunzo ya nyumba na kutumiwa kama lilivyokusudiwa kwa watoto na ndio maana ukaandaliwa waraka huo wa makubaliano.
Aidha, alifafanua kwa wajumbe wa Baraza hilo kwamba, jengo la Forodhani lililokuwa wakiishi watoto hao awali bado ni mali ya Serikali na litatunzwa licha ya kuwepo mikahawa na vitu vyengine, ambapo mapato yanayotokana na biashara hiyo yanaingia Serikalini
0 Comments