6/recent/ticker-posts

TAMKO LA MUWAZA KUHUSIANA NA KATIBA MPYA



MUWAZA‡ inawapongeza wanaharakati, wadau na wananchi kwa ujumla waliotoa msukumo wa kuelekea kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania.

Wakati huo huo, inaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuukubali wito huo.
MUWAZA inaamini kwamba suala la katiba mpya limechelewa sana na inatoa wito kwa serikali zote kulianzisha kwa haraka sana na kwamba lifanyike kwa uwazi na ufanisi mkubwa. Aidha, Baraza la Wawakilishi (BLW) la Zanzibar lichukue hatua za haraka kuwa mbele kwa maslahi ya Zanzibar katika kupatikana kwa haraka katiba mpya ya Tanzania na hatimaye ya Zanzibar kabla ya uchaguzi unaofuata.

MUWAZA inawapongeza wote waliotoa mawazo yao katika mustakbali wa katiba mpya. Aidha, inampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) kwa ujasiri na maelezo yake yanayotetea kupatikana kwa katiba mpya.

MUWAZA inawaomba na kuwahimiza Wazanzibari wote kuungana na kuendelea kutoa mawazo yao kwa nia ya kuipatia Zanzibar na Tanganyika serikali zitakazoshirikiana katika muungano wenye haki sawa kwa washiriki wake.

Katika hatua ya sasa hivi, MUWAZA inapenda kutoa mapendekezo yafuatayo kwa maslahi na mustakbali wa Zanzibar katika kuelekea kuipata katiba mpya ya Tanzania:

1. Mchakato wa kuipata katiba mpya ya Tanzania uzingatie malalamiko, kasoro (kero) na udhaifu wa muungano uliopo sasa ili katiba hiyo iweze kuuimarisha muungano huo na kuufanya kuwa wenye uwazi, haki, maslahi, kueleweka, kukubalika na kupendwa na washirika wake.

Mchakato huu uwe na uwakilishi wa serikali zote, wananchi, asasi za kiraia, na wadau wengine na usiwe wenye kuendeshwa kwa utashi wa chama fulani.
2. Katiba mpya ibadilishe mfumo mzima wa muungano na kuufanya kuwa ni Shirikisho la Tanzania linalojumuisha Zanzibar na Tanganyika. Kwa maana hiyo kuwepo na serikali tatu zenye marais wake kamili – yaani Serikali za Zanzibar, Tanganyika, na Shirikisho la Tanzania.

Mustakbal wa Zanzibar (MUWAZA) ni jumuiya iliyo ughaibuni inayowaunganisha Wazanzibari wa ndani na nje ili kuleta utambulisho wa Wazanzibari na kuleta umoja baina yao kwa kupigania mustakbali wa Zanzibar kama nchi, pamoja na kulinda maslahi yake ya kidola, kitaifa na uhuru.

3. Katiba ya Shirikisho la Tanzania itoe heshima sawa kwa Zanzibar na Tanganyika kama nchi kamili ili kulinda mamlaka na haki za nchi mbili hizo. Maamuzi yote ya Shirikisho yapitishwe kwa makubaliano ya kura za kila upande bila ya mchanganyiko. Mamlaka na utendaji wa Shirikisho uwe na uwakilishi sawa kutoka kila upande wa Shirikisho.
4. SUK pamoja na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW) izingatie jukumu zito iliyopewa na katiba ya Zanzibar la kuhakikisha kwamba mipaka, mamlaka, rasilimali, heshima na utamaduni wa nchi ya Zanzibar unalindwa kwa hali zote.
5. Katika kuyalinda mamlaka na haki za Zanzibar, BLW lipitishe kwa haraka hoja/maazimio juu ya mambo mahsusi ambayo ni muhimu na lazima kuwemo katika katiba mpya ya Tanzania. Pamoja na mengine, BLW lizingatie kwa uchache mambo yafuatayo:

a. Zanzibar inaingia katika mchakato wa kupata katiba mpya ya Tanzania ikiwa ni nchi kamili inayoshirikiana sawa kwa sawa na Tanganyika katika mjadala huo. Kwa njia yeyote ile, Zanzibar isiwe yenye kusukumwa katika majadiliano na maamuzi,

b. Serikali ya Zanzibar, rais wake, na bunge lake (BLW) ni sawa sawa na serikali, marais, na mabunge ya nchi nyengine zilizo huru duniani,

c. Rais wa Zanzibar pamoja na BLW wawe na mamlaka ya kuyakataa maamuzi yeyote ya serikali ya Shirikisho la Tanzania pale inapoona kwamba hayana mustakbali mwema kwa Zanzibar,

d. Kuyapitia upya makubaliano ya muungano na kujadili kila kipengele na baadae kuyapatia makubaliano hayo mapya ya aina ya Shirikisho ridhaa ya wananchi wa Zanzibar,

e. Kuhakikisha kwamba hata katika mambo ambayo yanabakia katika mamlaka ya Shirikisho, Zanzibar inakuwa na kielelezo chake kinachotambulika, (kwa mfano (a) maaskari/majeshi waliopo Zanzibar wawe ni Wazanzibari na hawahamishwi kikazi kwenda upande wa pili wa muungano au kinyume chake, (b) mtiririko wa wageni wanaongia Zanzibar uwe unadhibitiwa kwa njia na hati zinazokubalika, n.k.),

f. Shirikisho la Tanzania liwakilishwe katika Umoja wa Mataifa kwa viti vya Zanzibar na Tanganyika. Kwa maana hiyo, Zanzibar irejeshe kiti chake katika umoja huo na hivyo hivyo kwa Tanganyika,

g. Zanzibar itambulike kama nchi kamili katika mikataba na makubaliano yote ya kimataifa. Aidha, Rais wa Zanzibar awe ndie mwenye mamlaka ya juu kwa Zanzibar ndani ya Shirikisho na kimataifa,

h. Mambo yote yanayohusu uhuru wa kiuchumi na kisiasa yabakie ndani ya mamlaka ya Zanzibar. Aidha, mamlaka ya kuteua wagombea uongozi na kuchagua yawe ni ya Wazanzibari wenyewe. Kwa njia yeyote ile, masuala haya yasiingiliwe na upande wa pili wa Shirikisho,

i. Urais wa Shirikisho uwe wa mtindo wa kupokezana baina ya marais wa Zanzibar na Tanganyika katika kila muhula mmoja wa uongozi. Kwa mfano, katika kipindi cha uongozi cha miaka 5, miaka miwili na nusu iwe kwa Zanzibar na mengine miwili na nusu iwe kwa Tanganyika,

j. Zanzibar ipate haki zake zote kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kulingana na mtaji wake wa uanzishwaji wa benki hiyo. Aidha, Zanzibar iwe na kiwango cha ushiriki katika benki hiyo kinachojuilikana kwa wastani wa asilimia kulingana na mtaji wake wa uanzishi,

k. Mchakato na makubaliano ya katiba mpya ya Shirikisho la Tanzania yafanyike kwa uwazi, haki, na ufanisi mkubwa na kukamilika haraka iwezekanavyo kabla ya mwezi Juni 2012.

6. Katika kipindi chote cha mpito wa kuipata katiba mpya, ihakikishwe na ionekane kwamba kanuni ya kupitisha sheria bungeni inayotaka thuluthi mbili ya kura za wabunge wa Zanzibar inaheshimiwa ipasavyo. Vile vile, mamlaka ya BLW kutoka ndani ya katiba ya Zanzibar juu ya kuidhinisha au kukataa mabadiliko yanayohusu muungano inaheshimiwa.

7. Katiba mpya iwaelekeze marais wote kujiengua kutoka katika vyama kabla ya kuapishwa ili wawe huru na misukumo ya vyama vyao na wawajibike kwa mabunge yao. Kwa kufanya hivyo wawe na mrengo wa
ki-nchi badala ya ki-chama na waepukane na ukiritimba wa siasa za chama kimoja.

8. Katiba mpya iondoe ulazima wa vyama kuwa vya kitaifa ili itoe uhuru wa kuundwa vyama vya siasa vya aidha Zanzibar, Tanganyika, au Tanzania. Sambamba na hilo, katiba mpya itoe uhuru wa kuwepo wagombea binafsi wa kujitegemea.

9. BLW lihakikishe kwamba makubaliano ya mwisho ya katiba yanapitishwa kwa kura huru za maoni kutoka kwa wananchi. Kura hizo mbili ziwaulize

Wazanzibari masuala ya (i) kuukubali muungano au kuukataa, na (ii)kuikubali katiba mpya au kuikataa.

10.Mara baada ya mafanikio ya kupatikana kwa katiba mpya ya Shirikisho, na kupatikana pia ridhaa ya Wazanzibari juu ya katiba ya Shirikisho jipya, SUK kupitia BLW iipitie katiba ya Zanzibar na kuiandika upya ili iendane na wakati. Kwa kufanya hivyo, SUK na BLW izingatie pamoja na mengine mambo yafuatayo kwa nchi ya Zanzibar:

a. Katiba ya Zanzibar iende sambamba na demokrasia ya vyama vyingi na iwe yenye mwelekeo wa mabadiliko ya kuijenga Zanzibar mpya yenye nguvu, maadili, utamaduni, amani na haki sawa kwa wananchi wake,

b. Kutoa njia na fursa ya kusameheana na kusahau maonevu na makovu yaliyopita katika historia kwa kuijenga Zanzibar mpya yenye nguvu na upendo,

c. Kuzieleza, kuzitekeleza, kuzilinda na kuziheshimu haki za raia wa Zanzibar bila ya kujali tofauti zao za ama itikadi, dini, rangi, asili au jinsia,

d. Kutoa maelekezo ya kupata mahkama huru na tume huru ya uchaguzi itakayowajibika katika mahkama iliyo huru,

e. Kuweka sheria imara ya uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari za ndani na nje kwa wananchi wake,

f. Kuweka bayana haki ya Wazanzibari kushika nyadhifa za nchi yao kulingana na ujuzi na uwezo wao bila ya upendeleo,

g. Kubainisha na kusimamia kisheria kwamba uongozi na utendaji ni dhamana ya utumishi wa umma iambatanayo na uadilifu na uwajibikaji, na kwamba dhamana hiyo sio haki miliki ya mwananchi au kikundi fulani,

h. Kuzidisha mshajiisho wa kuyapa nguvu zaidi maridhiano na kuboresha uendeshaji wa SUK pale panapostahiki,

i. Kuweka sera maalum za Zanzibar ambazo zitalindwa na kila mwananchi au kiongozi bila ya kujali itikadi za ki-chama,

j. Kuondoa mwanya wa rais kujilimbikizia madaraka yanayofanana na udikteta,

k. Kuziheshimu na kuziimarisha asasi za kiraia zisizo za serikali, na kuzishirikisha katika uendeshaji wa nchi pale panapostahiki,

l. Kuijengea Zanzibar njia za uchumi na biashara huru na kuzilinda kisheria rasilimali za nchi kama vile mafuta, bahari, n.k. Pia, kuipa Zanzibar uhuru wa kutumia bandari zake na viwanja vyake vya ndege katika kuuhuisha uchumi wake,

11.BLW lihakikishe kwamba katiba mpya ya Tanzania inajadiliwa na kukamilika ifikapo mwezi wa Juni 2012. Endapo muda huo hautazingatiwa, au maagizo ya BLW hayatopewa kipau mbele, au mustakbali mwema kwa Zanzibar hautaonekena katika mchakato mzima wa katiba mpya ya Tanzania, BLW lichukue hatua ya kuiandika upya katiba ya Zanzibar na kuyaingiza angalau mambo yaliyomo katika mapendekezo haya kabla ya uchaguzi unaofuata.

MUWAZA inaihimiza serikali adhiimu ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) pamoja na Wazanzibari wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa kisiasa hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba mpya ya Tanzania.

Aidha, MUWAZA inaipa hadhari SUK na BLW kukwepa mtego wowote utakaotokea wakati mjadala wa katiba mpya utakaposhika kasi, kama vile kutiwa katika mazonge au mgogoro utakaowagawa Wazanzibar kwa njia yeyote ile.

MUWAZA inaziomba asasi za kiraia kuwaelimisha Wazanzibari ili waungane kwa kauli moja katika kutetea haki za nchi yao. Elimu hiyo ni muhimu ili kutoa nafasi nzuri kwa Zanzibar kujikita katika kulishughulikia ipasavyo suala muhimu la katiba mpya ya Tanzania.

MUWAZA inaamini kwamba mjadala wa kuipata katiba mpya ya Tanzania ni fursa muhimu katika kuuzaa upya na kuudumisha muungano wa aina ya Shirikisho na kuupatia ridhaa ya washirika wake.

Hivyo basi, ni wajibu wa kila Mzanzibari mwenye kuipenda nchi yake kujidhatiti katika kuilinda nchi yake kwa sababu pindipo Wazanzibari tutaipoteza fursa hii adhimu, tutakuwa hatuna wa kumlaumu wala njia ya kujinasua kwani muungano huu tunaoulalamikia siku zote utaonekana kama kwamba umehalalishwa na wananchi wenyewe.

MUWAZA inaamini kwamba Zanzibar inahitaji kujiimarisha ndani ya muungano wa Tanzania sambamba na kujiimarisha kimataifa katika mamlaka na haki zake za kitaifa. Mwanzo wa safari hiyo ni kuirudisha serikali ya Tanganyika ndani ya muungano huo.
Kama ilivyo kawaida yake, MUWAZA itaendelea kutoa maoni yake kuhusu mustakbali wa kupatikana kwa katiba mpya ya Tanzania kadri mchakato wake utakavyoendelea.

Kwa niaba ya MUWAZA, imetolewa na:

Dr. Yussuf Saleh Salim
Mwenyekiti wa MUWAZA
Copenhagen, Danmark
Februari 5, 2011

Post a Comment

0 Comments