MAFANIKIO makubwa ya kiuchumi na kijamii yameweza kupatikana kupitia makundi ya wanawake,watoto na vijana katika kipindi cha miaka 20 ya kuwepo kwa jumuiya ya kuhamasisha maedeleo ya wanawake Zanzibar (COWPZ).
Hali hiyo inatokana na utekelezaji wa mpango wa kupunguza umaskini Zanzibar (MKUZA) na mpango wa utekelezaji wa malengo ya milenium (MDG).
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa jumuiya isiyo ya kiserikali ya (COWPZ) Mgeni Hassan Juma katika mkutano wa kutathmini miradi inayofadhiliwa na umoja wa wake wa mabalozi wa nchi za Ulaya waliopo nchini Tanzania uliofanyika nyumbani kwa balozi wa Oman Mikocheni Dar es Salaam.
Katibu huyo ameseam juhudi kubwa zinazochukuliwa na Jumuia hiyo zimeelekezwa katika makundi hayo ili kuyawezesha na kuyasaidiakatika utekelezaji wa programu zao ili kufikia malengo.
“Tangu kuanzishwa Jumuia hii mafanikio na maendeleo makubwa yamepatikana kwa makundi haya katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa Jumuia ya COWPZ.”alisema Mgeni.
Afahamisha kuwa COWPZ katika kipindi cha miaka 20 imeweza kusimamia utekelezaji na uendelezaji miradi mikubwa iliyofadhiliwa na wadau wa kitaifa na kimataifa miradi ambayo imewajengea sifa ndani na nje ya nchi.
Aidha Katibu huyo amewashukuru wake wa mabalozi wa Umoja wa nchi za Ulaya kwa misaada yao wanayoitoa na kuahidi kuendelea kujiimarisha vyema katika kusimamia na kufikia malengo yaliokusudiwa.
“Kwa niaba yangu na COWPZ kwa ujumla napenda kutoa shukurani za dhati kwa wake wa mabalozi wote kwa misaada yenu mnayoitoa na COWPZ inaahidi kuendelea na kujiimarisha vyema katika kusimamia na kufikia malengo yaliyokusudiwa,”amefahamisha.
Mapema mwenyekiti wa umoja wa wake wa mabalozi (DSG) Mama Tudy Wasinger, amesifu juhudi za Jumuiya hiyo katika utekelezaji wa malengo yake sambamba na kuipongeza kwa kuwa makini katika kipindi chote cha miaka 20 ya kuwepo kwake.
Amesema kuwa hii ni faraja kubwa kuona akinamama hao kuweza kuwasaidia akinamama wenzao, vijana na watoto katika kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi.
Mapema wajasiriamali kutoka Zanzibar walipata nafasi ya kuonesha na kuuza bidhaa zao mbali mbali wanazozalisha ambazo wamefadhiliwa na umoja huo.
0 Comments