Na Khamis Amani
ILI kupambana na kudhibiti tatizo sugu la uingizwaji, uuzwaji na utumiaji wa dawa za kulevya hapa nchini, kunahitajika marekebisho makubwa ya sheria.
Imefahamishwa kuwa, sheria iliyopo hivi sasa inaonekana ina mapungufu makubwa ambayo yanahitaji kurekebishwa ili iweze kudhibiti janga hilo la kitaifa na kimataifa.
Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Ali Salum Haji, alieleza hayo alipokuwa akibadilishana mawazo na Wanapolisi jamii wa Shehia ya Kwahani, muda mfupi baada kuwakabidhi vitambulisho vya ulinzi vilivyotolewa na Jeshi la Polisi wilaya ya Magharibi Unguja.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ameir Tajo kiliopo Kwaalinato mjini hapa, Mwakilishi huyo alisema kuwa, biashara ya dawa za kulevya ina mtandao mkubwa ambayo inahitaji
sheria madhubuti ili kuweza kukabiliana nayo.
Alisema kuwa, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia semina wanazofanyiwa na Kitengo cha kupambana dawa za kulevya, walibaini kuwepo hali hiyo ambayo ikiachiwa itaendelea kuathiri taifa.
Alifahamisha kuwa, ijapokuwa serikali ipo makini juu ya suala hilo na kuelekeza nguvu zake katika kupambana nalo, lakini uingiaji wa dawa hizo hatari bado unaoendelea, kutokana na udhaifu wa sheria ziliopo
hivi sasa.
Hivyo alisema kuwa, Baraza la Wawakilishi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa sheria na Kitengo cha kupambana na dawa za kulevya wanahitajika kukaa pamoja ili waweze kutunga sheria itakayoweza
kudhibiti hali hiyo.
Alisema kuwa, suala hilo hivi sasa limekuwa ni janga kubwa la taifa, ambalo hukosa nguvu kazi ya uchumi wake kutokana na wengi wa watumiaji wake ni vijana, ambao ndio chachu yao ya maendeleo pamoja na familia zao.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Maofisa mbali mbali wa Jeshi la Polisi wilaya ya Magharibi, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa wilaya hiyo Salma Khamis, Mwakilishi huyo alilipongeza Jeshi hilo
kwa kazi kubwa wanayoifanya juu ya kudhibiti hali hiyo.
Pamoja na pongezi hizo kwa Polisi, Mwakilishi huyo alisema kuwa jitihada za makusudi zinahitajika za kutoa elimu ya kutosha juu ya vijana hasa watumiaji wa dawa hizo, juu ya hasara na faida inayotokana
na utumiaji wa dawa za kulevya.
Alisema kuwa, wauzaji wa dawa za kulevya ni wauaji kama walivyo wauaji wengine, ambao wao maisha huangalia maslahi ya maisha yao kuliko kuangalia maisha ya walio wengi jinsi wanavyoathirika na wengine
kufariki kutoka na sumu hiyo ya utumiaji wa dawa za kulevya.
Hivyo Mwakilishi huyo alisema kuwa, kuwepo kwa sheria iliyo makini na kukamilika janga hilo litaondoka na jamii itaweza kuishi bila ya hofu na serikali kujipanga katika mambo mengine ya kimaendeleo.
0 Comments