Na Ramadhan Makame
WAZIRI wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary amesema wazanzibari waziweke pembeni hitilafu zao wawe na uzalendo wa nchi yao, wakati wa utoaji wa maoni ya katiba mpya utakapowadia.
Alisema tume ya kukusanya maoni itakapoundwa ni fursa muhimu na ya kipekee ambayo itawawezesha kutoa dukuduku na hatimaye kuondosha matatizo mbali mbali yaliyopo.
Alisema ni juu ya wazanzibari wenyewe wakati huo, kuamua lipi liendelee kuwepo na lipi liondoshwe ikiwa kwenye muungano na hata mambo mengine nje ya muungano.
Waziri Bakary alieleza hayo ukumbi wa wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Vijana alipokuwa akizungumza na makundi mbali mbali ya kijamii kuelezea mchakato mzima wa uundwaji wa katiba unavyoendelea.
“Hii ni fursa muhimu ndugu zangu, tusiichezee tuseme yale tusiyoyapenda ambayo leo yapo katika nchi yetu na tuyaingize yepi kwa mustakabali wa nchi yetu, ni wakati wa kuweka mbele uzalendo na utaifa”, alisema waziri huyo.
Akizungumzia juu ya kupitishwa kwa mswada wa sheria ya kuundwa kwa tume ya kukusanya maoni ya katiba uliopitishwa wiki iliyopita Bungeni mjini Dodoma, alisema Zanzibar ilipata fursa kama nchi kamili.
Alisema tofauti na watu wanavyouponda mswada huo, viongozi wa Zanzibar waliopewa jukumu la kupeleka mawazo hayo walipita kila hatua na kujiridhisha kuwa mawazo na mtazamo wa Zanzibar yaliingizwa baada ya kujadiliwa katika kila hatua.
“Tulipita katika hatua zote katika kuhakikisha mawazo ya wazanzibari yanaingizwa kwenye mswada huo, tangu haujapitishwa na baada ya kupitishwa, hilo lilikuwa jukumu letu tulilopewa na wazanzibari”,alisema waziri huyo.
Aidha alifahamisha kuwa katika semina kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyojadili mswada huo Novemba 12 mwaka huu waliibuka na mapendekezo 13 ambapo 10 kati ya hayo yalifikishwa Bungeni siku iliyofuata na kuongezwa.
Alisema si vyema watu kutafsiri vibaya na kupotosha mswada huo kwani umezingatia kwa kiasi kikubwa maslahi ya Zanzibar.
Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Asaa Rashid alisema makubaliano yaliyofikiwa ni kuamuliwa kwa katiba hiyo kwa kutumia theluthi tatu 2/3 ya wabunge wa bunge la katiba kutoka Zanzibar na Tanzania bara.
Aidha alisema nafasi nyengine ni kwa wananchi kupewa nafasi ya kupiga kura ya maoni ama kukubali au kuikataa katiba hiyo baada ya mchakato wa kukusanywa kwa maoni kukamilika.
Wakichangia katika kongamano hilo, washiriki walisema ni muhimu wananchi wakapewa taaluma ya mchakato huo sambamba na kuisoma katiba ili waweze kutoa michango ambayo itainufaisha Zanzibar.
Kwa upande wake Hamad Yussuf alisema katika suala la katiba ni lazima uzalendo uwe mbele katika kutetea maslahi ya wazanzibari.
Naye Salum Bimani alisema NGOs na vikundi nyengine vya kijamii lazima vifikiwe katika kupewa taaluma ya suala hilo kutokana na mchango wa vikundi hivyo kwa jamii.
Kongamano hilo la siku moja liliandaliwa na wizara ya Katiba na Sheria, ambapo wanaharakati, waandishi wa habari na vikundi mbali mbali vya jamii, pamoja na wananchi walihudhuria.
0 Comments