MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Juma Kassim Tindwa, ameitaka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha wanawasomesha wanafunzi kwa kina somo la historia ili waijue nchi yao inapotoka na ilipo sasa.
Alisema vijana wengi wamekua hawatambui nchi ilikoanzia na ilipo sasa pamoja na muwelekeo wake na wanadhani tokea awali iko hivi bila ya kuelewa kwamba imekombolewa hadi kufikia taifa huru.
Tindwa ametoa kauli hiyo jana huko uwanja wa Michezo Gombani, Chake Chake alipokua akizungumza na wananchi kwenye mkesha wa mwenge wa uhuru mara baada ya kumaliza mbio zake kwenye Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema kutokana na vijana walio wengi kutofahamu taifa lao linakotokea ndio maana leo hii kuna mambo kadhaa yanadharauliwa na kuonekana hayana maana ikiwa ni pamoja na ujio wa mbio za mwenge.
Alieleza kuwa somo la historia halijapewa kipaumbele kwa kina maskulini na kusababisha baadhi vijana kumaliza masomo ya ngazi ya juu bila ya kuwa na uelewa wa kutosha juu ya historia ya nchi yao.
“Vijana hebu jifunze sana sosmo la historia ya taifa letu, mtafaidika na mambo kadhaa na mtaona jinsi wazee na viongozi wetu walivyojitahidi hadi leo hii kufikia hapa tulipo’’, alisema Tindwa.
Hata hivyo aliwapongeza vijana wanaotembeza mwenge wa uhuru mwaka huu 2011, kwa kueleza vizuri historia ya taifa hili na kuwaomba kuendelea kufanya hivyo kwenye maeneo mengine ambamo mwenge utapita.
Mapema kiongozi wa mbizo za mwenge kitaifa mwaka huu, Mtumwa Rashid Khalfan alisema kuwa suala la kutunza amani na utulivu ndani ya nchi ndio linalofaa kuungwa mkono na kila mmoja.
Katika kufanikisha hilo amewataka vijana kutokubali kutumiwa kwa kujiingiza kwenye makosa yasiyokuwa ya lazima pamoja na kuwatahadharisha juu utumiji wa dawa za kulevya.
Aidha kiongozi huyo wa mbio za mwenge, aliwataka wananchi kuendelea kuwafichua wanaojihusisha na hujuma ya magendo ya zao la karafuu kwani serikali imeongeza bei kwa ajili ya kutokomeza hilo na kuinua kiwango cha mapato kwa wakulima wa zao hilo.
Akisoma risala ya wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba, Ofisa Tawala Mkoa wa huo, Hanuna Ibrahim Massoud, alisema kuwa ujio wa mwenge mkoani humo umeamsha ari na hamasa ya kufanyakazi kwa vile umezindua na kuweka mawe ya msingi kiasi ya miradi 10 ya wananchi.
Alieleza kua miradi iliyopitiwa na mwenge ndio iliyotoa dira na mwanga kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba na kuona umuhimu wa kuchangia mwenge kila mwaka.
Mwenge wa uhuru uliopokewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa ukitokea Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo mwenge huo kwa sasa uko Mkoa Tanga kuendelea na mbio zake.
0 Comments