6/recent/ticker-posts

WAZIRI JIHAD ATAKA UTALII ULINDWE

Na Ramadhan Makame

WAZIRI wa Habari, Utamadini, Utalii na Michezo Abdillahi Jihad Hassan amesema sekta ya utalii ni muhimu sana kwa uchumi wa Zanzibar, hivyo wananchi hawapaswi kuyafumbia macho mambo ambayo yanaweza kuiharibu sekta hiyo.

Waziri Jihad alieleza hayo jana ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View, kwenye hafla fupi ya kumkaribisha balozi wa AMREF nchini Italia, Francesco Gambella.


Alisema utalii Zanzibar unachangia asilimia 27 ya pato la taifa, hivyo ni wajibu wa Wazanzibari kuulinda utalii na sekta za kitaalii ili nchi iweze kupiga hatua za kimaendeleo.

Alisema serikali iko makini na imekuwa ikihakikisha vitisho dhidi ya sekta ya utalii kama vile kukindi cha al Shaabab ambacho kimekuwa na tabia ya kuteka nyara wageni, halitapewa nafasi Zanzibar.

“Vitendo vya kuteka watalii kweli vimetokea nchini Kenya, sisi kama serikali tumeshaviarifu vikosi vyetu vya ulinzi viwe macho na tatizo hilo”,alisema waziri huyo.

Aidha alitoa wito kwa wananchi na wavuvi kuwa makini na kutoa habari pale wanapohisi kuna vitu ambavyo wanavitilia mashaka, kwani nchi hulindwa na wananchi wake.

Akizungumzia ujio wa Balozi huyo, waziri Jihad alisema ziara yake ambapo ameandamana na waandishi wa habari itasaidia kuvitangaza vivutio vya Zanzibar nchini Italia.

Kwa upande wake Balozi Francesco Gambella ambaye anatokea katika Jumuiya ya Flying Doctors, alisema mbali ya kuutangaza utalii wa Zanzibar pia, watafanya harambee ambapo fedha zitakazopatikana zitatumika kwa wagonjwa kisiwani Pemba.

Alisema wakiwa Zanzibar ambapo watafanya mashindano ya mbio za boti, siku ya Jumatatu zoezi hilo litarushwa katika televisheni za nchini Italia, pamoja na kutengeneza DVD ambazo zitagawiwa nchini Italia.

Balozi huyo amevutiwa sana na madhari za Zanzibar na kueleza kuwa ni sehemu moja yenye vivutio vizuri vya utalii.

Post a Comment

0 Comments