Na Mwajuma Juma
UKIMYA wa uongozi wa klabu ya Yanga kutokuthibitisha ushiriki wake katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2012, unaendelea kuiweka njia panda na kuiumiza kichwa kamati ya michuano hiyo.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, amekaririwa akisema kwamba klabu zote zilizoalikwa zimejibu kuwa zitashiriki, lakini Yanga imekaa imekaa hadi sasa.
Mjumbe huyo amesema, muda uliobaki ni mfupi na endapo klabu hiyo itatoa majibu ya kukataa, itakuwa shida kupata timu nyengine mbadala kujaza nafasi yake.
"Tunapata wasiwasi kuwa Yanga inataka kukimbia, lakini haya si mashindano binafsi, ni ya serikali, kama hawakushiriki itakuwa wametudharau", alisema.
Zanzibar Leo iliwasiliana kwa njia ya simu na Msemaji wa klabu hiyo Louis Sendeu, ambaye alilihakikishia kuwa Yanga itashiriki na haina mpango wa kuyakimbia mashindano hayo.
Alisema kamati ya mashindano na ufundi ya mabingwa hao wa soka Tanzania Bara, itakutana baada ya sikukuu ya Krismasi kujadili ushiriki wa timu hiyo kwenye ngarambe hizo.
Sendeu alieleza kuwa, kwa vile wanao wapenzi wengi hapa Zanzibar,kutokushiriki mashindano hayo, itakuwa haikuwatendea haki mashabiki wa timu hiyo, hasa katika kipindi hiki cha kuadhimisha miaka 48 ya
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Aliwahakikishia wapenda soka wa Zanzibar, kuwa Yanga inathamini Mapinduzi yao hasa ikizingatiwa kuwa muasisi wake marehemu Abeid Amani Karume alikuwa miongoni mwa wapenzi wake wakubwa aliyetoa mchango wa hali na mali katika kuiimarisha wakati wa uhai wake.
"Kwa kuthamini mchango wa muasisi wa Mapinduzi, na heshima tunayoipata sasa kutoka kwa Mama Fatma Karume, tutakuwa wezi wa fadhila iwapo hatukuja kuungana na ndugu zetu wa Zanzibar katika kusherehekea
Mapinduzi kwa njia ya michezo", alifafanua Sendeu.
Katika mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Januari 2, mwakani, Yanga imepangwa katika kundi 'B' pamoja na timu za Azam FC, Kikwajuni na mabingwa wa soka Zanzibar, Mafunzo, huku kundi 'A' likiwa na timu za Simba, Miembeni United, Jamhuri na KMKM
0 Comments