6/recent/ticker-posts

Sakata la Ubadhirifu ZFA Mjini Bado Bichi

Na Salum Vuai, Maelezo

KUFUATIA Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Taifa kubatilisha uamuzi wa ZFA Mjini wa kuwafukuza kazi Katibu na Mshika Fedha wake, chama wilayani humo kimesema hakiridhishwi na uamuzi huo.

Barua ya ZFA Wilaya ya Mjini ya Februari 13, 2012 (kumb. nam. ZFA/11/2012/W MJINI) iliyotumwa ZFA Taifa baada ya kupokea agizo la kuwapokea watendaji hao, imesisitiza kuwa chama hicho hakikukosea kuwatimua watendaji hao.


Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita, ZFA Mjini iliwafukuza Yahya Juma Ali aliyekuwa Katibu, na Ali Abdallah Hassan, Mshika Fedha kwa tuhuma za ubadhirifu, kughushi nyaraka na kuiba fedha za chama.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, ZFA Mjini haina dhamira mbaya dhidi ya watendaji hao, na inaheshimu maamuzi ya ZFA Taifa ambayo ndiyo iliyo juu yake, lakini imeomba ipewe ufafanuzi sahihi na uhalali wa maamuzi hayo ili iweze kujenga hoja zenye mashiko kwa wanachama wake.

“Tambueni kuwa, kadhia hii inajulikana vyema na wanachama wetu na jamii kwa jumla, hivyo wanahitajia ufafanuzi wa kina lakini pia sisi kama ZFA Wilaya kuwa na mwega wa kuegemea,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa ZFA Wilaya ya Mjini Hassan Haji Hamza, ilielezwa kuwa chama hicho kimefadhaishwa na ZFA Taifa kutokuuona ukweli juu ya tatizo la kughushi ‘pay slip’ lililofanywa na Mshika Fedha, ambalo lilisababisha kutoweka isivyo halali shilingi 290,000 za chama.

Hamza alieleza kuwa, kutokana na hatua ya kumrejesha Mshika Fedha na kumtaka arejeshe shilingi 290,000, ni kama kwamba hakuna kosa alilofanya na wala hastahili adhabu yoyote.

“Tuna dhamira thabiti ya kutekeleza maelekezo yenu lakini ufafanuzi wenu wa haraka ndio utakaosaidia kutekeleza kwa ukamilifu na haraka maagizo mliyoyatoa,” alihitimisha Mwenyekiti huyo.

Post a Comment

0 Comments