WAKATI Zanzibar na Tanganyika zilipoungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zipo wizara kadhaa zilizoamuliwa ziwe za muungano.
Kiutaratibu wizara hizo zinakuwa na mawaziri na manaibu wao ambao wanatumikia pande zote mbili sawia.
Mfano wa hizo, ni ile ya Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje na Wizara inayoshughulikia mambo ya Afrika Mashariki, lakini kwa wizara nyengine, kila nchi inakuwa na yake yenye mamlaka ya kujisimamia kwa niaba ya nchi husika.
Na katika wizara zisizokuwa za muungano, haijapata kuelezwa kwamba elimu ni miongoni mwa hizo, lakini tangu zamani kumekuwa na utaratibu wa elimu ya juu kusimamiwa na Tanzania Bara, huku ile ya maandalizi, msingi na kati zikiachwa kila sehemu ijitegemee kivyake.
Katika hali kama hiyo, baada ya wanafunzi wa Zanzibar kudima kwa miaka yote tangu maandalizi hadi sekondari ya kati, wanapoingia kidato cha nne, hulazimika kufanya mitihani inayotungwa Tanzania Bara chini ya Baraza la Mitihani NECTA.
Sina hakika kama wakati wa kutunga mitihani hiyo Zanzibar inawashirikishwa na walimu wake, na kama ndivyo, sijui ni kwa kiwango gani.
Na je, kama upo uwakilishi huo, ni kwa kiwango gani basi wanapata nafasi ya kutoa masuala wanayoyaona yanastahili wakati wa kutunga mitihani hiyo ili kuweka uwiano ulio sawa kati ya Bara na Zanzibar.
Kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho ni ushiriki wa walimu wa Zanzibar katika kusainisha mitihani hiyo ambapo mara kadhaa wamekuwa wakipelekwa hata mikoa ya Tanzania Bara kufanya kazi hiyo.
Yumkini utaratibu huu ulikuwa lazima ufanywe hapo nyuma kwa sababu wakati nchi zetu zinajikomboa, Zanzibar ilichelewa kuanzisha vyuo vikuu vyake ambapo wale wahitimu wa sekondari waliofaulu walilazimika kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi, na hata baadhi ya vyuo vya taaluma nyengine kama vile uhasibu na kadhalika.
Pamoja na hayo, hapo nyuma, malalamiko kuhusu kuonewa, kunyanyaswa, kufelishwa kwa makusudi kwa wanafunzi wa Zanzibar waliojiunga na vyuo vikuu Bara, yalikuwa nadra kusikika.
Lakini katika miaka ya karibuni, vilio vya wanafunzi na watahiniwa wa Zanzibar wanaofanya mitihani ya taifa kwamba hawatendewi haki hata pale viwango vyao vya ufahamu vinapokuwa vikubwa kuwazidi wenzao wa upande wa pili, limekuwa jambo la kawaida.
Baya zaidi, malalamiko hayo mara nyengine yanahusishwa na mitazamo ya kidini, ikidaiwa kuwa watendaji wanaohusika na usainishaji mitihani, huangalia mtahiniwa ni wa dini gani na apewe nini kulingana na itikadi yake.
Mimi hili sitaki nilizungumzie kwa undani kwa sababu sina hakika nalo, lakini napenda nitumie usemi maarufu wa Kiswahili, "Lisemwalo lipo, kama halipo lipo njiani laja".
Siku chache zilizopita NECTA iliweka katika mtandao matokeo ya mitihani ya kidato cha nne, ambapo kila mmoja aliyapokea kwa hisia tafauti.
Pamoja na kuwa vitendo vya udanganyifu hutokezea katika mitihani, lakini wengi wamefadhaishwa na hatua ya kundi kubwa kufutiwa kabisa mitihani yao, wakidai hata kama walifanya hila, suluhisho ni kurudiwa mitihani hiyo na sio kuwafuta kabisa.
Aidha kama, inaaminika kuwa mitihani ilivuja, kwa nini waadhibiwe wanafunzi tu huku ikijulikana kwamba hilo haliwezekani bila kuwepo mkono wa maofisa wanaosimamia mitihani hiyo au wanaoitunga?
Kwa kuwa katika kipindi hiki hali hiyo ya upande mmoja kudai kuonewa na kubaguliwa katika mitihani ya elimu ya juu, ni busara hili nalo liorodheshwe katika kero za muungano kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi.
Aidha, nadhani suluhisho la tatizo hili, ni kuiondoa elimu ya juu katika muungano ili Zanzibar iweze kuanzisha Baraza lake la Mitihani, na hivyo kuendesha yenyewe utaratibu wa elimu na mitaala yake kikamilifu.
Kama hoja ilikuwa kutokuwepo kwa vyuo vikuu, sasa hali imebadilika na hilo si tatizo tena kwani tayari tunavyo vyuo vikuu vitatu, mbali na vyengine vya kitaaluma kama kile cha usimamizi wa fedha, cha Kiislamu, Ufundi Mbweni na Mikunguni, pamoja na chuo cha Utumishi wa Umma.
Vyuo hivyo vyote kwa pamoja vimekuwa vikitoa wahitimu wazuri katika fani tafauti na kuongeza idadi ya wasomi na wataalamu wa Kizanzibari, sifa inayotupa uwezo wa kuanzisha Baraza la Mitihani na kujivua katika mbeleko ya muungano kwa elimu ya juu.
Kimantiki, haiingii akilini elimu za ngazi za chini iwe tunafanya kivyetu, lakini ile ya juu tufuate mitaala ya Bara, kwani yawezekana wanafunzi wetu wa Zanzibar wakawa wazuri, lakini wanapofika sekondari ya juu wanaongezewa mzigo kwani huenda mbele ya safari mambo ni magumu zaidi.
Hapa sikusudii kusema tuwatungie wanafunzi wetu mitihani myepesi, la hasha, lakini inapobainika wenzetu hawana uadilifu wakati wa kusainisha na kupanga madaraja, iko haja ya kuzinduka na kujiuliza kulikoni.
Tel: 0777 865050
E mail: salumss@yahoo.co.uk
7 Comments
Namshukuru sana mtoa mada kwa umahiri wake ktk kuchambua sakata hili la kufutwa kwa matokeo ya wanafunzi wa form 4, Zanzibar pamoja na suluhisho alilolipendekeza.
ReplyDeleteMimi kwa upande wangu, namuunga mkono ktk mengi lkn. sikubaliani nae ktk baadhi ya mambo.
Kwanza, ni kuiondoa elimu ya juu ktk mambo ya mungano,na hii ni kutokana na sababu zifuatazo;
Kwanza, kuendelea kufanya mitihani ya NECTA kunatufanya Wtza sote tiliopata elimu ya sekonadari tuwe na vyeti vinavyofanana na kutambulika chini ya chombo kimoja(necta)
Hali hii itamwezesha mhitimu kuweza kuajiriwa na kujiunga na chuo chochote ktk jamhuri yetu na sio tuu Z'bar..tumeyaona hayo wakati wa siasa chafu(1995-2005)
2Pili,SMZ haina historia nzuri ktk kusimamia masuala ya elimu..tunahofia watu kuja kupelekewa vyeti nyumbani au kupasishwa kwa mizengwe.
Nadhani, mtoa mada kwa muda mrefu huenda hayupo z'bar lkn. sisi tuliopo tumeshuhudia mambo yafuatayo;
1)Vijana wasio na sifa wakipelekwa kwenye vyuo vya ualimu kwa madai eti ni form 4.
2)Vijana wengi wa form 4 wakiruhusiwa kufanya Diploma za ualimu kwa madai eti ni form 6 hadi pale NECTA walipozuia matoke(2005) na kuomba wapelekewa namba za mitihani ya O'LEVEL za wahusika.
Hata hivyo SMZ ilihakikisha NECTA wanayaachia matokeo kwa faida ya muungano!
3)Kuna vijana hapa wameshawahi kupatiwa vyeti vya chuo cha kiislamu wakati hawajawahi kua chuoni na hatimae kuajiriwa na 'wizara-tul-ulum'...mambo hayo!
4)Wanafunzi wa form 11 wengi wanakua hawana sifa za kuendelea na masomo ya form 111 lkn. kwa kuwafurahisha wazee wa wanafunzi, SMZ huwatangaza karibia wote na hatimae kujisifu kua kiwango cha ufaulu kimepanda.
Matokeo yake ni kufeli form 4.
5)Nakumbuka kuna wakati wanafunzi wengi wa form 11 kutoka Z'bar waliruhusiwa kujiunga na chuo cha jeshi la polisi, matokeo yake wengi wakafeli, SMZ walipotakiwa ushauri wakataka wapitishwe hivo hivo! matokeo yake sasa wanadai..ooh Polisi wa Z'bar hawapandishwi vyeo!
Sote tunaipenda Z'bar lkn. kwa kweli yanayofanyika hapa kwetu bado yanatupa wasiwasi.
Ingawa wengine wanaweza kudhani kua sisi si wazaledo lkn. wakumbuke:
Zanzibar,ndipo petu
hatuna, pengine katu
Asikudanganye, mtu!
Kujenga, wajibu wetu
Kwa nguvu na jasho letu
Tuishi kama wenzetu!
Ahsante mtowa mada kwa uchambuzi wako katika sakata hili la mitihani nakubaliana na wewe kwa mambo karibu yote ila kwa tahadhari kubwa kama alivoainisha mtowa maoni na mimi nna wasiwasi kama wake kwani historia yetu ya elimu imechafuliwa kwa kiwango kikubwa katika awamu ya Waziri haruna kwani wanafunzi wengi wasio na sifa walipelekwa katika vyuo vya elimu Nkrumah na Chuo cha kiislamu pia wanafunzi wa FII walikuwa wanapelekwa kusomea chuo cha afya ambayo ni hatari zaidi katika mustakbali wa nchi.
ReplyDeleteKwa hiyo wazo la kuanzisha baraza la mitihani la Zanzibar pekee ni wazo zuri ila wizara ya elimu kunahitaji mabadilik ya hali ya juu (reforms) kurekebisha uozo wote aliousababisha maalim Haruna.
Hata kuko vyuoni kuna vituko vya tende kwa uji wa maji. Vyuo viwili tu hapa ndio vya kuaminika;
ReplyDeleteChukwani na Chwaka ela vyengine havifai, kuna watu nawajua washamaliza degree Suza na Tunguu na hawana principal mbili wala hawajafanya Pre ha..siuhuni huo?
Assalamu alykum, kwanza tukupongeze kwa juhudi zako za kuelimisha jamii. Kuna jambo limetokea la kufutiwa matokeo wanafunzi hasa huku Zanzibar ndio mwaka huu tumeathirika zaidi kiasi cha wanafunzi wa skuli 30 wamefutiwa matokeo hayo. Waathrika zaidi ni wale School candidates. Wahusika inabidi kuangalia zaidi kama wanafunzi wamefutiwa mitihani kwa tuhuma za kuvuja mithani. Kwa nini vile vile matkeo ya skuli za Private pia zi siwe na matokeo mazuri? pia uzoefu waonyesha wanafunzi wa mitihani ya private wana hangaika zaidi kutafuta fursa kama hizo za kuvuja mithani.
ReplyDeleteHuenda ikawa haki haikutendeka, Zanzibar hivi sasa wengi ya walimu wake wanaosomesha sekodari ni wahitimu wa degree ya ya kwanza ya ualimu haiwi ni changamoto ya wanafunzi hawa kufanya vizuri. hii ni tofauti na kile kilio cha sekondari za kata ambapo wanafunzi wake wamekosa walimu wenye sifa kama hizo.
Hili suala la Elimu ya Juu Litolewe katika orodha ya mambo ya muungano kwa maoni yangu.Haidhuru tuanze kutumia kigari kujifunza kutembea lakini kuna siku tutasimama kwa miguu yetu.Binaadamu alie timamu kiakili hawezi kuogopa au kukimbia mabadiliko.Zanzibar ni yetu na tusitegemee hatma yetu na vizazi vyetu isimamiwe na upande mwengine wa muungano (Tanganyika).Mtu akilia hasemi mamayetu,husema mamayangu..........
ReplyDeleteMungu Ibariki Zanzibar.
Mnaosapoti kubaki katika NECTA wacheni woga, hadi lini mtatawaliwa kiakili?. Sababu zenu zote haziingii akilini kuwa ukiziweka kwenye mizani uzito wake kuwa ni kheri kubaki NECTA. Hata iwe ni kweli mnayoyaeleza, je hayarekebishiki! Mlio utaja nyinyi ni udhaifu wa sheria kutofuatwa ipasavyo Zanzibar.
ReplyDeleteVyuo tunavyo na wataalamu tunao, elimu ya juu haimo katika masuala ya muungano. I say lets get rid of NECTA bugudha...
Mimi nadhani bado ikali mapema mno kuwaamini 'wahadimu' kiasi chote hicho!
ReplyDeleteLabda GNU iendelee kuwepo siku zote, lkn. kubwa zaidi wacha tuone namna watavyoendesha uchaguzi wa 2015 kwanza. unajua kuna watu mpaka leo hawajawapa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi?
Ah..hawa!...labda wanambie Mungu mmoja