6/recent/ticker-posts

Historia ya Vyombo vya Habari Iandikwe - Waziri Mbarouk



Mwajuma Mmanga na Kauthar Abdalla

WAZIRI wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk amesema Zanzibar ina historia ya kipekee kwenye tasnia ya habari katika bara la Afrika na kuliomba Baraza la Habari Tanzania (MCT), kusaidia wataalamu watakaoiandika historia hiyo.

Waziri huyo alieleza hayo katika ukumbi wa Zanzibar Beach Resort kwenye kongamano lililofuatiwa na mkutano mkuu wa mwaka wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).


Alisema wakati umefika wa historia ya vyombo vya habari Zanzibar kuandikwa kitaalamu hali itakayosaidia vizazi vijavyo kuifahamu vyema na kuwa kama muongozo wa kuendeleza mazuri waliyoasisiwa.

‘Naiomba sana MCT, itumie wataalamu wasaidie kuaindika upya historia ya vyombo vya habari ya Zanzibar’, alisema waziri huyo.

Aidha waziri huyo aliwataka waandishi wa habari Tanzania kuhakikisha wanafuata maadili kwani ndiyo nguzo muhimu ya kuipeleka mbele kada hiyo yenye umuhimu mkubwa katika kukuza maendeleo.

Awali akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Muhadhiri Muandamizi Ayub Rioba, alivitaka vyombo vya habari visilichukulie kwa mzaha suala la marekebisho ya katiba mpya.

Alisema mchakato wa mabadiliko ya katiba mpya ya Tanzania ni jambo lenye kuhitaji kuchukuliwa kwa umakini na vyombo vya habari kwani ndilo litakaloweza kuijenga Tanzania ijayo inayohitajiwa na vizazi vijavyo.

Aliwataka waandishi wa habari waichambue kuitafsiri katiba jambo ambalo litawasaidia wananchi sio kuifahamu tu bali pia litawawezesha kutoa maoni yenye mantiki.

Naye Timothy Kitundu akieleza hali ya ajira kwa vyombo vya habari, alisema waandishi wa habari wamekuwa mafundi wa kueleza dhiki za kiajira kwa taasisi nyengine huku wao wenyewe pia wakikabiliwa na matatizo ya aina hiyo hiyo.

Alishauri uwepo umoja ambao utawaunganisha wanahabari katika kutetea haki zao za msingi na kuwafanya kupata maslahi kama wanavyonufaika wafanyakazi wa kada nyengine.

Wakichangia katika kongamano hilo, Rose Mwalongo alisema limekuwepo tishio la kimaisha kwa waandishi wenye kuandika habari za kiuchunguzi kutokana na kugusa malahi ya watu wachache.

Naye Prof. Ruth Meyena aliwataka waandishi wa habari waache kulalamika na badala yake wakae pamoja kutafuta njia ambazo zitahakikisha wanaondokana na matizo waliyonayo.

Kongamano hilo lililoandaliwa na MCT liliwashirikisha waandishi wa habari za ya 150 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.



Post a Comment

0 Comments