MUASISI wa Chuo cha Mafunzo na Uongozi cha UVCCM Zanzibar, Ramadhan Mohamed Kombo “Makwire”,akiangalia Kalenda ya Chama Cha Mapinduzi baada ya kukabidhiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa.(Picha na Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar).
Na.Mwandishi Wetu Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amewataka viongozi, watendaji na wanachama wa Chama hicho kuendeleza utamaduni wa kufanya ziara za mara kwa mara za kuwatembelea wazee, viongozi wastaafu pamoja na waasisi wa Chama na Jumuiya zake, ili kurithi mbinu, hekima na nasaha zao za kiuongozi na kiutendaji.
Dkt. Dimwa ametoa wito huo alipofanya ziara ya kumtembelea kiongozi mstaafu wa Chama, Ramadhan Mohamed Kombo maarufu “Mzee Makwire”, nyumbani kwake Jumbi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Wilaya ya Magharib ‘B’, Unguja.
Alisema viongozi hao wastaafu ni hazina muhimu ya maarifa na uzoefu uliopatikana kupitia miaka mingi ya utumishi ndani ya Chama na Serikali, hivyo ni muhimu kwa viongozi na wanachama wa sasa kuwathamini na kujifunza kutoka kwao.
Alieleza kuwa kuimarika kwa Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya zake kumetokana na busara, hekima, maarifa na ushauri wa viongozi wastaafu ambao kwa muda mrefu walilitumikia Chama na Serikali kwa uadilifu na kujituma.
“Chama Cha Mapinduzi tunajivunia kuwa na hazina ya wazee imara waliowahi kulitumikia Chama kwa juhudi kubwa.
Mchango wako kama mwalimu umetufundisha mambo mengi yaliyotusaidia katika masuala mbalimbali ya kiutendaji na kiuongozi hivyo mwezi huu mtukufu wa Ramadhani nimeona ni vyema nije kukutembelea na kujua hali yako,” alisema Dkt. Dimwa.
Aidha, alimueleza kiongozi huyo mstaafu kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuwa imara na kinaongoza kwa ufanisi mkubwa kutokana na misingi thabiti iliyowekwa na viongozi wa vyama vya ASP na TANU, waliotekeleza kwa vitendo malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Aliongeza kuwa mafanikio ya maendeleo yanayoonekana nchini yanathibitishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, ambayo inaendelea kutekelezwa kwa kasi katika sekta mbalimbali za maendeleo bila ya ubaguzi wa dini, kabila wala itikadi za kisiasa.
Katika maelezo yake, Dkt. Dimwa aliwataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwaombea dua viongozi wakuu wa nchi ili Mwenyezi Mungu awaongoze katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi Viongozi hao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Kwa upande wake, muasisi wa Chuo cha Mafunzo na Uongozi cha UVCCM Zanzibar, Ramadhan Mohamed Kombo “Makwire”, alimshukuru Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Dimwa kwa kumtembelea pamoja na kumpatia sadaka ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Pia alimpongeza kwa utendaji wake tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, akisema unaonesha juhudi na dhamira ya kuendelea kukiimarisha Chama.
Makwire alisema Tanzania na Zanzibar zimeendelea kuwa na ukuaji mzuri wa kiuchumi pamoja na maendeleo katika nyanja mbalimbali, hali inayochangiwa na uongozi imara unaotokana na Chama Cha Mapinduzi.
Aliahidi kuendelea kutumia elimu, maarifa na uzoefu wake kuwashauri wanachama na wananchi kwa maslahi ya Taifa, ili vizazi vya sasa na vijavyo viendelee kuishi katika misingi ya maadili, upendo, amani na uongozi bora.
Katika ziara hiyo, Dkt. Dimwa pia alitoa sadaka ya vitu mbalimbali kwa kiongozi huyo mstaafu kama sehemu ya kuenzi na kushiriki matendo ya kheri katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

.jpg)
.jpg)
0 Comments