6/recent/ticker-posts

Mbeya Yawafukuza Madaktari Waliogoma


Na Thompson Mpanji, MBEYA
SERIKALI mkaoni Mbeya imelimaliza sakata la mgomo wa Madaktari kwa aina yake baada ya kupitisha maamuzi magumu ya kuwatimua kazi madaktari zaidi ya 72 wa mafunzo ya vitendo walioajiriwa na hospitali ya Rufaa mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Dk.Norman Sigalla kwa niaba  ya Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Abbas Kandoro, alisema bodi imefikia kuchukuwa uamuzi  mgumu  kutokana na madaktari kutotekeleza wajibu wao wa kuwahudumia wagonjwa.


Alisema  sababu nyingine ya kuchukuwa uamuzi huo madaktari hao  hawakufika kazini na kukaidi ombi  la Mwenyekiti wa bodi kukutana nao kuwasikiliza sababu za kutofika kazini na kujadili namna ya kumaliza matatizo  yao.

Alifahamisha kuwa kutokana na maamuzi hayo madaktari hao waliotimiliwa wametakiwa kuondoka katika majengo ya hospitali waliyokuwa wanaishi.

Dk.Sigalla alisema Juni 23 mwaka huu jumla ya  madaktari 15 waliokuwa zamu  wakiwemo wa mafunzo 12 na walioajiriwa watatu hawakufika kazini, Juni 24 madaktari 19 wakiwemo wa mafunzo 15 na ‘registrars’ wanne  hawakufika kazini  na kuanzia Juni 25 hadi jana imethibitika madaktari wa mafunzo 54  na walioajiriwa 18  hawajafika  kazini.

Alifafanua kuwa Bodi iliamua madaktari wote ambao hawafiki kazini waandikiwe barua za kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia na hospitali na pia kukiuka kanuni za kudumu za utumishi wa umma toleo la 2009 kif.f.16-f.17 na F.27.

Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa alisema hadi kufikia jana siku zilizotolewa na bodi zilikuwa zimemalizika  na hivyo wamewaandikia barua za  kusitisha  ‘internship’   katika hospitali ya Rufaa Mbeya na kuwarudisha kwa Katibu Mkuu na kuwataka wanaokaa hosteli waondoke kabla ya saa 11.00  za jioni leo.

Alisema madaktari 18  walioajiriwa   wanakabidhiwa barua zao za kusimamishwa  ajira yao  katika hospitali ya Rufaa Mbeya  na kurudishwa wizarani  kwa Katibu Mkuu  kwa hatua stahiki za kinidhamu na kutakiwa kukabidhi mali za ofisi.

Dk.Sigalla alikiri kuongezeka   kwa  mzigo lakini hawajatetereka,bodi iliwasiliana na Taasisi mbalimbali Mbeya na nje ya mkoa  ili kupata wafanyakazi wa kusaidia kupunguza makali ya upungufu wa wafanyakazi  na wamepata ushirikiano  kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya  kwa kupatiwa madaktari watano kusaidia.

Akizungumzia hali ilivyo kwa sasa Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk.Eliuter Samky alisema licha ya kuongezeka kwa mzigo lakini wanatarajia madaktari wataalamu (specialist) 22 waliobaki na na walioajiriwa 13 watafanyakazi   za kutoa huduma bila wasi wasi.

Awali gazeti hili limeshuhudia baadhi ya madaktari katika hosteli wakiwa katika pilika za kupakia mizigo  katika gari  ndogo ya  kukodi  ya abiria taksi na kuondoka katika eneo la hospitali ya Rufaa huku  wakiwa hawataki kupigwa picha wala kuhojiwa.

Juni, 22 mwaka huu Mahakama kuu ya kazi Tanzania kanda ya Dar es Salaam chini ya jaji S.C.Moshi ilitoa natisi ya kuzuia mgomo wa madakatari.


Post a Comment

0 Comments