6/recent/ticker-posts

Mlemavu Aliepewa Ujauzito Kusaidiwa


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema itaangalia uwezekano wa kukaa pamoja na wizara ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuona namna watavyoweza kumpatia msaada mtoto mwenye ulemavu aliyebakwa na kupewa ujauzito.

Waziri wa Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Zainab Mohammed Omar, aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea mjini Zanzibar, wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake Wanu Hafidh Ameir.


Mwakilishi huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kumsaidia mtoto huyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa vile mtoto huyo hana uwezo wa kumtunza mtoto huyo.

Akijibu suala hilo, waziri huyo alisema ni kweli serikali imeliona hilo tatizo na itafikiria kukaa pamoja na wizara ya Makamu wa Kwanza wa Rais baada mtoto kuonekana uwezo wake ni mdogo wa kujitunza huku akiwa ni mlemavu.

Alisema wataliangalia hilo ili kuona mtoto huyo anapata misaada itayoweza kumsaidia kukimu maisha yake kwani hivi sasa yupo katika hali itayoweza kumpa mzigo kuendesha maisha yake.

Akijibu suala la nyongeza la Asha Bakari Makame, aliyehoji kama ina mpango wa kukata rufaa kwa vile inaonekana katika suala la mtoto huyo kudaiwa na vyombo vya sheria kukosa ushahidi juu ya suala hilo na huenda kukawa na uzembe wa makusudi unaofanywa na taasisi hiyo.

Waziri huyo alisema wizara hiyo mara zote imekuwa na utaratibu wa kukata rufaa juu ya matukio ambayo huyaona ipo haj ya kufanya hivyo.

Akiendelea kujibu suala la Mwakilishi wa Wanawake Amina Iddi Mambrouk, aliyetaka kujua ni lini kipimo cha DNA kitaweza kupatikana.

Akijibu suala hilo Waziri huyo alisema serikali bado inahangaika kupata kipimo cha DNA, na ni vyema wananchi wakasubiri kufanikishwa kwa mpango huo.

Kuhusu suala la Msingi la Mwakili wa Wnawake Mgeni Hassan Juma, aliyetaka kufahamu kama Wizara hiyo inafahamu taarifa za kubakwa kwa mtoto huyo baada ya kuripotiwa katika Gazeti la Zanzibar Leo, alisema Wizara hiyo ilifuatilia suala hilo katika kituo cha mkono kwa mkono pamoja na Polisi Mazizini na mtuhumiwa tayari amechukuliwa vipimo vya D.N.A.

Alisema kutokana na taratibu za kisheria suala hilo bado lipo katika kituo cha Polisi cha Mazizini ikiwa inasubiri kupatikana kwa ushahidi  wa kipimo cha D.N.A ili kuweza kuifikisha Mahakamani kesi hiyo.

Alisema ingawa Wizara hiyo imekuwa ikichukua hatua mbali mbali za kukabiliana na tatizo hilo lakini bado kuna mambo ambayo yameonekana kukwaza jitihada hizo likiwemo suala la ushirikiano mdogo kwa jamii katika suala zima la kutoa ushahidi Mahakamani, upelelezi wa Polisi kuchukua muda mrefu kutokana na ushirikiano na jamii na hukumu kuchelewa.

Post a Comment

0 Comments