WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad
Masoud Hamad, amesema kwamba haoni sababu ya kujiuzulu nafasi yake kutokana na
matatizo yaliojitokeza katika mikataba ya ujenzi wa jengo jipya la kupokelea
abiria katika kiwanja cha ndege cha Zanzibar.
Waziri huyo, aliyaeleza hayo jana wakati
akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, aliyetaka
kujua kwanini hajiuzulu yeye na viongozi wa wizara yake waliohusika kusaini
mkataba huo ambao umeonekana kuwapo kwa uzembe walioufanya wa kuitia hasara
serikali na kusababisha kuweka saini mkataba mwengine.
Suala hilo
pia liliulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija, na Mwakilishi
wa Muyuni Jaku Hashimu Ayoub, waliotaka kujua kama
kulikuwa na uzembe ndani ya mikataba hiyo.
Akijibu suala hilo waziri huyo alisema suala
la kujiuzulu kwa viongozi wa wizara hiyo halipo kwani kilichofanyika kilikuwa
hakitokani na viongozi wa wizara hiyo bali ni mapendekezo yaliotokana na
wataalamu wa ujenzi na usanifu wa michoro ya jengo hilo.
Alisema hapo awali serikali ilikabidhiwa
michoro ya jengo hilo
ikionesha kuwapo kwa mikonga miwili, lakini baadae mjenzi alipokabidhiwa aliona
kuwa baadhi ya maeneo yamepewa nafasi ndogo kwa kuwa na vyumba vidogo.
Alisema eneo jengine ambalo lilionekana kuwa
na tatizo ni kuokana na ujenzi wa mikonga katika kiwanja hicho ingelikuwa
midogo kutokana na hivi sasa serikali inaadhimia kupokea ndege kubwa.
Alisema mikonga iliyoainishwa katika michoro
ya awali ilionekana ndege ambazo zingeweza kuhudumiwa na mikonga ya kupokelea
abiria ingeliwafanya abiria kushuka ndani ya uwanja wa ndege huku ndege ambazo
zingeweza kutumia mikonga hiyo zingekuwa ni za mashirika madogo kama Precision.
Alisema kutoka na sababu hizo hivi sasa
mabadiliko hayo yatasababisha kuwapo kwa mabadiliko ya ujenzi wa mikonga kutoka
minne hadi kufikia mikonga miwili ikiwa ni hatua itayoweza kukifanya kiwanja
hicho kuwa na hadhi ya kimataifa.
Kutoakana na hali hiyo waziri huyo alisema
haoni sababu ya kuwapo kwa madai ya kutakiwa yeye na watendaji wake kuwa
ajiuzulu kwani kilichofanyika ni urekebishaji wa mikataba na hivi sasa kampuni
iliyopewa kazi hiyo inaendelea na kazi zake.
Mapema Naibu waziri wa wizara hiyo, Issa
Haji Gavu, akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim
Ayoub aliyetaka kujua sababu za msingi zilizosababisha kuwapo mikataba miwili
yenye gharama tofauti za ujenzi.
Naibu huyo alisema kutokana na mabadiliko ya
usanifu ambayo muajiri alitaka kufanyika na ndiko kulikosababisha gharama zake
kubadilika kutoka dola za kimarekani 57.5 milioni, na kufikia dola za
kimarekani 70.4 milioni zikiwa na lengo la kufanikisha ongezeko za vifaa kwa
ajili ya ujenzi huo.
Alisema mradi huo unatarajiwa kumalizika mwezi
Januari 2014, na umezingatia takribani huduma zote muhimu za kuhudumia ndege za
mizigo ikiwemo mikonga ya kuhudumia ndege.
Alisema hadi hivi sasa tayari serikali
imeweza kuwafidia wananchi 60 ambao waliathirika na kuwapo kwa ujenzi huo ikiwa
ni hatua ya kuweza kufanikisha ujenzi huo.
0 Comments