6/recent/ticker-posts

Wazanzibari Wengi Hawafahamu Misingi ya Utawala Bora


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheir, ameliambia Baraza la Wawakilishi kuwa wananchi wengi wa Zanzibar bado hawajui misingi mikuu ya inayojenga utawala bora.

Waziri huyo aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, aliyetaka kujua matokeo ya utafiti juu ya utawala bora uliofanywa na wizara hiyo kwa kushirikiana na International Law and Policy Institute.


Akijibu suala hilo waziri huyo alisema tayari ripoti hiyo inafanyiwa kazi, lakini katika hatua za awali zimeonesha bado Wazanzibari hawaijui misingi mikuu inayojenga utawala bora.

Alisema katika utafiti huo pia iligundua wananchi wengi wanajua vyema maana ya rushwa na madhara yake na matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kuwekwa hadharani mara baada ya kukamilika hatua za upokeaji wa ripoti hiyo kutoka kwa watafiti.

Alisema kuchelewa kutolewa hadharanai kwa ripoti hiyo kunatokana na kubainika kuwapo kwa makoseo ndani ya ripoti hiyo baada ya Makatibu wakuu kuipitia na kubaini kuwapo kwa matatizo ya aina hiyo.

Alisema kazi hiyo baada ya kukamilika serikali inafikiria kuigawa ripoti hiyo kwa wananchi ikiwa ni hatua ya kuona utafiti huo unawafikia wengi.

Waziri huyo alieleza kuwa serikali katika kuhakikisha inalifanya hilo kwa kuzifanyia kazi tafiti hizo kama ni taarifa za msingi kwa mfumo wa mawasiliano kwa tafiti ambazo zitafanywa hapo baadae.

Alisema katika kuufanya utafiti huo wizara hiyo iliwahoji makundi mbali mbali wakiwemo wananchi mbali mbali katika shehia za visiwa vya Unguja na Pemba, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Watumishi wa Umma ambapo mambo waliyoulizwa ni pamoja na Utawala bora, rushwa na huduma za kijamii kwa umma.

Akijibu suala la nyongeza la Mwakilishi huyo aliyetaka kujua ni kwanini ripoti hiyo iliwasilishwa kwa makatibu wakuu pekee, alisema ilifikishwa huko kutokana na kuwa ndio utaratibu wa serikali kufikisha ripoti hizo kwa kamati ya wataalamu na baada ya kujirisha inakusudia kufikishwa mbele zaidi.

Post a Comment

0 Comments