6/recent/ticker-posts

Ziara ya Maalim Seif yaleta faraja hospitali ya Wete.Kitanda chumba cha upasuaji, friji vyatafutwa haraka


Na Khamis Haji, OMKR
WAGONJWA waliolazwa na wale wanaopata huduma katika hospitali ya Wete, Kaskazini Pemba wamepata faraja kubwa kufuatia ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliyoifanya Novemba 23 mwaka jana hospitalini hapo.
Katika ziara hiyo alipotembelea taasisi zilizopo chini ya wizara ya Afya, Makamu wa Kwanza wa Rais alitoa maagizo ya kutafutiwa ufumbuzi wa haraka baadhi ya huduma zinazokosekana katika hospitali hiyo.
Huduma ambazo Maalim Seif aliagiza zipatiwe ufumbuzi ni kuharibika  kitanda katika chumba cha upasuaji, kutafutwa friji la kuhifadhia dawa na vifaa vya matibabu, kuongezwa vitanda katika wodi za hospitali pamoja na kuzingatiwa mazingira ya usafi.
Maalim Seif, juzi alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa mwezi Novemba, ambapo alikuta takriban yote yamepatiwa ufumbuzi na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma zilizokuwa zikikosekana kwa ufanisi mkubwa.

Daktari Dhamana wa hospitali ya Wete, Othman Maalim Haji alimueleza Maalim Seif kuwa friji tayari limepatikana, kitanda kilichokuwepo kimefanyiwa matengenezo pamoja na kuletwa chengine kutoka Mkia wa Ng’ombe, ambapo pia vitanda vyengine vipya kwa ajili ya chumba hicho vinatarajiwa kuwasili hivi karibuni.
Aidha, daktari huyo dhamana alisema tayari wamepokea vitanda 20 pamoja na magodoro yake ambavyo vimeshafungwa katika wodi kwa ajili ya kusaidia kutatua tatizo la uhaba wa vitanda pamoja na uchakavu wa vitanda, magodoro na matandiko yaliyopo hivi sasa.
“Kwa kweli ziara yako Mheshimiwa Makamu imekuwa chachu ya utatuzi wa changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili hospitali, hivi sasa takriban zote zimepata ufumbuzi,” alisema daktari dhamana alipokuwa akizungumza na Maalim Seif.
Daktari huyo alisema maagizo mengine ambayo yameweza kutekelezwa ni kuwekwa utaratibu mzuri na kumbukumbu sahihi za utoaji na uingizwaji wa dawa, zikiwemo zinazotolewa kwa wagonjwa pamoja na zinazoingia katika bohari ya hospitali hiyo, kutoka Bohari Kuu ya Wizara ya Afya.  
Pamoja na maagizo katika hospitali hiyo, Maalim Seif pia mwezi Novemba aliutaka uongozi wa Wizara ya Afya kushughulikia kwa haraka malalamiko ya wafanyakazi, ikiwemo yanayohusu mafao yao pamoja na malalamiko ya kuwepo upendeleo.
Afisa Dhamana wa Wizara hiyo Pemba, Dk.Ukasha alisema baadhi ya maagizo hayo yameshatekelezwa, ikiwemo tatizo la wafanyakazi wapya waliopelekwa Pemba kucheleweshewa mishahara na posho zao, pamoja na mfanyakazi Sanura Salehe wa hospitali ya Chake Chake aliyedai kudhulumiwa kwenye mkopo wake wa baiskeli. 
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi na wagonjwa waliokuwepo hospitalini hapo walisema ni kweli kumekuwa na mabadiliko makubwa hospitalini hapo tokea kufanyika ziara ya Maalim Seif mwishoni mwa mwaka jana.
Walisema hata suala la usafi katika hospitali hiyo limeimarika vizuri, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa huko nyuma.
Wakati huo huo, Maalim Seif amezindua maabara ya kisasa katika hospitali ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa maabara hiyo, ambayo ujenzi wake ulifadhiliwa na kituo cha Center for Diseases Control (CDC) cha Marekani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Maalim Seif alisema hatua hiyo ni ukombozi kwa wananchi wote wa Micheweni kwa sababu hivi sasa wataweza kuchunguzwa maradhi yao hapo hapo.
Alisema awali wananchi walikuwa wakipata shida kubwa kwa kulazimika kukaa siku nyingi kusubiri matokeo ya uchunguzi wa maradhi yanayowashumbua, ambao ulikuwa ukifanywa katika hospitali za Chake Chake, Wete na Mkoani, lakini pia maabara hiyo itakuwa ya rufaa kwa vituo vyote vya afya vya Wilaya ya Micheweni.

Post a Comment

0 Comments