TAARIFA YA UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (UVCCM) KATIKA MAZUNGUMZO NA WAANDISHI WA HABARI WA VYOMBO MBALI MBALI IJUMAA 27 SEPTEMBER 2013. UKUMBI WA EACROTANAL KIKWAJUNI.
Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imesikitishwa na kushangazwa na matamshi yaliotolewa na Wenyeviti wa Vyama vya Siasa Freeman Mbowe wa CHADEMA, Ibrahim Lipumba CUF. James Mbatia NCCR MAGEUZI pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa CUF Abuubakari Khamis Bakari katika mkutano wa Kibandamaiti uliofanyika siku ya Jumatano tarehe 25 Septemba 2013.
Akimtaka Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Mhe Mathias Chikawe. Mhe William Lukuvi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jaji Fredrick Werema na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Job Ndugai wajiuzulu kwa madai ya kusema uongo Bungeni wakati yeye Abuubakari ndiye manju na bingwa wa kusema uongo na uzandiki.
Madai ya kusema Zanzibar haikushirikishwa katika kutoa mapendekezo ya muswada wa mabadiliko ya Katiba si ya kweli, zaidi wamekusudia kuwapotosha wananchi kwa nia ya kujitafutia umaarufu wa kisasa.
Mabadiliko ya Mchakato wa Katiba yanayoendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria kimsingi na uhalisia wake hayafanyiki kwa kufuata utashi ama matakwa ya vyama vya siasa au Asasi za kiraia, ndiyo maana ikatungwa sheria ya kusimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
UVCCM tunao ushahidi wa kutosha kuwa Waziri Chikawe hakuja Zanzibar kutaka mapendekezo ya vifungu vya Katiba na badala yake amekuja akiwa na rasimu ya mswada wa Katiba ambao ndio uliojadiliwa na kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kujadiliwa na wabunge ndani ya Bunge na si kujadiliwa papo kwa hapo.
Tabia ya Abuubakari inafahamika kuwa ni mwanasiasa na msomi asie kuwa na ukweli na msaliti tokea akiwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ pale aliposhiriki katika mradi maalum wa kumyumbisha kisiasa Rais wa awamu ya tatu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Idris Abdul Wakil.
UVCCM tunamuona Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad kwamba hakuwa na haki ya kumsakama Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi au kumsemea badala yake kila mmoja ana mipaka ya kazi zake.
Maalim Seif anastahili kusemea ofisi yake, kinyume na kitendo anachoonekana kukipenda katika dhana yake ya kutimiza azma ya kuendeleza upotoshaji na kuwadanganya wanachama wake kama alivyofanya katika mkutano wa Kibanda maiti wiki iliyopita.
Wakati Maalim Seif akisema mapendekezo yalioletwa Zanzibar yalikuwa na vifungu sita na SMZ ikatoa mapendekezo kwa vifungu vitatu na vitatu vingine waliridhika navyo.
Waziri Abubakari amesikika akidai kuwa vifungu vilivyoletwa ni vinne na kuongezeka hadi 12 jambo linalothibitisha kuwa wanasiasa wa upinzani huwa hawafanyi utafiti na hukurupuka na kutoa matamshi bila ya kuangalia athari zake.
Aidha, katika mkutano huo, Maalim Seif alilalamika kwamba viongozi wa CCM Bara wana mpango wa makusudi wa kuiburuza Zanzibar kwa kuchomeka mambo mbali mbali ndani ya muswada wa sheria wa katiba uliopitishwa hivi karibuni Bungeni, kwa maslahi ya CCM , wakati jambo hilo si sahihi.
UVCCM imejirizisha kwa kupata ushahidi uliowazi kwamba Waziri wa Katiba na Sheria wa SMZ Abubakar Khamis Bakari akiwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman wote kwa pamoja waliandaa mapendekezo ya vipengele vya muswada wa Katiba (vifungu 4) na ndani yake kuorodhesha maoni ya Zanzibar, ambayo yalipelekwa Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Katika mashauri hayo Abubakar alieleza wazi kwamba hana tatizo na Uteuzi wa nafasi 166 za Wabunge wa Bunge la Katiba kutoka maeneo mbali mbali kama vile asasi za kiraia, na makundi mengine.
Abukakari alipendekeza wabunge hawa kutoka ndani ya kundi hili wateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, lakini la kushangaza juzi katika mkutano wake wa kibandamaiti Maalim Seif amepinga mapendekezo yaliyotolewa na Abuubakari kutoka chama CUF kwa kusema Asasi za Kiraia zichague wawakilishi wao wenyewe na sio Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vile vile Abuubakar alipendekeza kuwa kati ya wajumbe 166 kuwepo na uwiano wa kijinsia tuu na sio uwiano wa pande 2 za Muungano kama ilivyodaiwa na Maalim Seif.
Hali hii inaonyesha wazi kuwa Viongozi hawa wa Upinzani hawajui nini wanachokifanya kutokana na kupingana kwa kauli zao katika suala hili.
Huu ni unafiki mwengineo wa Maalim Seif na Abuubakar katika siasa za Zanzibar . Iko haja ya wanachama wa CUF sasa kuzinduka na siasa za kiusanii zinazoendeshwa na viongozi wao huku wakifunika ukweli na kuhalalisha uongo.
Eneo hili peke yake lionaonyesha kuwepo kwa mkanganyiko wa matamshi kati ya Maalim Seif na mshirika wake Abuubakari, ukionyeesha ni jinsi gani wote kwa pamoja walivyo na uhodari wa kupika uongo na kupotosha mambo kama alivyofanya Abuubakari kwa kuisingizia Radio ya Chuchu FM imefanya mahojiano na Katibu Mwenezi wa CCM Waride Bakari Jabu wakati mahojiano yamefanywa na Zenj FM.
Mwenyekiti Mao The Dong wa China amewahi kusema kuwa hukuna mwenye haki ya kusema bila ya kufanya utafiti. Profesa Lipumba kama asingekuwepo umma ulikuwa umeshapotoshwa kwa uzushi huo, UVCCM hatushangai kwa vile Abuubakar anajulikana na kufahamika kuwa ni mtu anapenda kupayuka bila ya kufanya utafiti na kupata ushahidi.
UVCCM tunachelea kuyaamini matamshi yaliowahi kutolewa na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Chambani Abasi Juma Muhunzi kuwa Abuubakar ni “Bush Lawyer, sasa Vijana tunaamini kuwa usomi wa Abuubakar una mushkeli katika uchambuzi wa mambo na uwelewa wake.
UVCCM tumejiridha kuwa katika kila hatua ya utendaji unaohusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar imekuwa ikishikishwa kikamilifu katika hatua za maandalizi ya marekebisho ya sheria, na mjadala wa rasimu ya marekebisho ya Katiba, ambapo Zanzibar katika vikao vya Kitaalamu ilikuwa inawakilishwa na uwakilishi toka Wizara ya Katiba na Sheria na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar jambo ambalo tunaushahidi nalo wa kutosha.
Aidha, madai yaliyotolewa na wanasiasa hao akiwemo Maalim Seif kwamba kipengele cha kuruhusu kura ya Simple Majority ni kuingamiza Zanzibar na kutuhumu kuwa kifungu hiki kimeingizwa kinyemela nalo pia si sahihi kwani wakati wa wajadiliano kwenye kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, Mbunge Halima Mdee wa CHADEMA ndiye aliyetoa mapendekezo ya uamuzi wa kufuata mfumo wa wingi wa kura (simple majority) ikiwa kura zimepigwa zaidi ya mara 2 na hazikufika zaidi ya theluthi 2 kutoka kila upande wa Muungano basi kura ya simple majority itumike.
Baadhi ya wabunge walipendekeza kwamba Tume ya Katiba ikome kufanya kazi zake mara tuu Bunge la Katiba litakapoanza, mapendekezo haya yalitolewa na Mhe Jaku wakati wa Vikao vya Kamati na Mhe Jaku walipendekeza hoja hii wakati Bunge likijadili muswada huo. .
Kwa mujibu wa kanuni ya bunge ibara 84, 2 kamati ina mamlaka ya kualika wadau na kukaa nao kuzungumza kama mabavyo ilifanya. UVCCM tunaushahidi wa kutosha na vielelezo vya fomu walizojisajili wajumbe wa vyama 21 ambavyo vilihudhurika katika mkutano uliotishwa na kamati ya bunge miongoni mwao wakiwemo CUF, Chadema ADC, Jahazi asilia na vyenginevyo.
UVCCM tunashangaa sana leo vyama hivi vinapaza sauti kuwa Eti Zanzibar haikushirikishwa watuambie inamaana utendaji wao wa majukumu unafanyika kwa Bara tu. Na jee inakuaje kuja kufanya mkutano Zanzibar wakati wao sio wasemaji wa Zanzibar hicho ni kioja na daliali za wazi kuonyesha vyama hivyo vinavyojitia muungano wa kinafiki kuwa vimepoteza muelekeo kisiasa na sasa wanatafuta kujihami kwa kuwafitinisha na kuigiza mgawanyiko miongoni mwetu.
Tunasema vyema hivi kwa hakika havikuitendea haki Zanzibar leo wanataka kusema nini hata tuwaelewe.
Matamshi ya kutaka Zanzibar iwe na mamlaka pia yanayoonyesha ni kiasi gani kuwepo kwa viongozi wa upinzani ambao ni mbumbumbu wanaojifanya wamesahau historia ya nchi hii kwa kujitia ubabaifu usio na tija na kujifanya hawafahamu historia na nini maana ya mamlaka kamili ya nchi.
Zanzibar ilipata mamlaka yake kamili Januari 12, 1964, imeendelea kushikilia Mamlaka hayo hadi January 12, 2014 itakapotimiza miaka 50 ikiwa na mihimili mitatu ya Mahakama, Baraza la Kutunga Sheria na Utawala, ardhi na watu kama sifa ya kuwa nchi yenye Mamlaka yake.
Pia Ofisi mbili ambazo ni dhamana katika mambo ya utendaji ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, UVCCM tumekuwa na ushahidi wa kutosha kwamba zimekuwa na mawasiliano ya karibu katika kila hatua kabla ya suala hilo kufika kwa watendaji ambao wamejadili kwa kuzingatia maslahi ya pande zote na baade kutoa mapendekezo yake.
UVCCM tunaamini kuwa haikuwa muafaka kwa Makamo wa Kwanza wa Rais kuacha majukumu yake ya Kikatiba aliopangiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kujigeuza kuwa Msemaji Mkuu wa SMZ kwenye viriri vya siasa wakati wapo wasemaji wa Serikali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais .
Aidha, Kitendo cha Ismail Jussa kumtaka Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd ajiuzulu wadhifa wake kwa kutoitetea Zanzibar ni mbinu dhaifu ya CUF inayolenga kuleta mgawanyiko na kuvuruga mfumo mzima wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Uamuzi wa wabunge kupitisha mswada huo ni katika kutekeleza wajibu wao kama mhiimili mmoja wa dola, uamuzi huo hakupaswa kuhojiwa na chombo chochote kwa vile Bunge ndicho chombo kinachowakilisha wananchi, chenye jukumu na mamlaka ya kupitisha mswada na siyo mikutano ya hadhara, wanaharakati au mashirika ya kiraia ambao kazi zao si kutunga sheria.
Haki ya mashirika hiari ya kijamii na asasi nyingine ni kutoa maoni na si kubeba dhamana ya kutunga sheria kama inavyoshabikiwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini kwa utashi na ushabiki usio na mashiko wala mantiki.
Kwa mujibu wa sheria dhamana ya uwakilishi wa wananchi hutokana na wabunge pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishji Zanzibar na si Asasi za kiraia ambazo pia huwakalishwa na wabunge na Wawakilishi katika utungaji wa sheria kwenye vyombo hivyo.
Hata hivyo UVCCM inaridhishwa na utendaji wa Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ambaye amekuwa msimamizi makini, akishughulikia kutatua migogoro ya ardhi, uwajibikaji katika Utumishi wa Umma, usimamiaji na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015 kwa ufanisi na tija kama inayoonekana.
Amekuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya hujuma dhidi ya raia wasiokuwa na hatia. akipiga vita uhalifu, tofauti na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wakionekana ni chimbuko la matatizo yanayojitokea Zanzibar na wakikataa kujifundisha kutokana na majanga yanayotokea maeneo mablimbali ya dunia ikiwemo Afrika Mashariki.
UVCCM Tanzania tunamuomba Mhe, Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asaini muswada huu kwani kitendo cha kutosaini muswada huo ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu 97 . Bado watanzania wanaimani na matumaini makubwa na Rais Kikwete.
UVCCM inadhani huu ulikuwa si wakati wa kuvutana au kugawanyika kwa mitazamo ya kisiasa bali ni wakati muafaka wa kujenga Umoja na Mshikamano wa Kitaifa kwa vile jamii imeshafikia hatua ya maelewano kutokana na kuwepo kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
UVCCM inashangazwa sana na wenzetu wanaitumilia GNU kwa manufaa ya Chama chao katika kuhimiza vurugu, mipasuko ya kisiasa na hata kufanya udanganyifu ndani ya serikali na taasisi zake kwa kutumia dhamana za uongozi walizopewa ndani ya serikali.
UVCCM tunasema ikiwa wenzetu wamechoka na maridhiano yaliyokuwepo nchini basi sisi vijana wa Chama Cha Mapinduzi hatutosita kukishauri chama chetu kuwa tuko tayari kwa lolote nalitote tugawane mbao.
Tumejiamini na uwezo tunao hata tuende kwenye uchaguzi kesho Chama Cha Mapinduzi kitashinda na kuendelea kuongoza dola kwa vile kipimo cha uwezo mdogo wa upizani kushinda uchaguzi kiko wazi na sasa wanajaribu kutumia kila hila ili kutaka kuvuruga amani, umoja na mshikamano uliopo Tanzania .
Ni vyema wanasiasa tukae na kukumbuka umuhimu wa amani ambayo imezungumziwa hata katika vitabu vya dini.
Nabii Ibrahim (AS) alipoamrishwa na Mwenyezi Mungu amuache mkewe Hajra na mwanawe mdogo Ismail, Nabii Ibrahim dua ya mwanzo aliomba ilikuwa ni ‘Ewe Mwenyezi Mungu ujaalie mji huu uwe mji wa amani’ na baadae akaongeza kuomba ‘Wajaalie watu wa mji huu wapate rizikii ya matunda’
Sisi tunaamini kila mwenye nafsi dhaifu anakuwa daima ni mnafiki hapa duniani hivyo ni vyema viongozi wenye tabia hiyo wakabadilika na kurejea katika imani ambayo itasaidia kutetea taifa letu katika misingi ya amani, Umoja Mshikamano na upendo.
"KIDUMU CHAMA CHAMA MAPINDUZI"
SHAKA HAMDU SHAKA (MNEC)
NAIBU KATIBU MKUU UVCCM
TANZANIA ZANZIBAR
1 Comments
Hivi ccm, znz, haina wasemaji, naona, hawa wanao jiita vijana, kaziyao kukurupuka, sasa na, hawa wapinzani, uchara, wale pinzani uchara lengolao, ni kuwadanganya, watu wao inamana na hawa vijana, wa ccm, akili zao kama wafuasi, wahao wanao waita wapinzani, sisi, tunajua, cuf, chadema, nccr, vyote ni jumla ya chama tawala, tuna wa shanga wao na nanyie mnojiita vijana wa ccm, mlokuwa hamna uwezo wakufikri
ReplyDelete