Na; Khamis Haji (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameonya kuwa tabia ya baadhi ya watu kuharibu
mazingira inasababisha athari kubwa, ikiwemo kupotea eneo kubwa la ardhi ya
Zanzibar inayotegemewa kwa shughuli za maendeleo na za kijamii.
Maalim Seif amesema hayo leo wakati
alipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbali mbali ambayo ardhi yake imeliwa na
maji ya bahari katika kisiwa cha Unguja. Akiwa ameambatana na Wakuu wa Mikoa ya
Mjini Magharibi, Kaskazini na Kusini Unguja.
Amesema ili hali hiyo iweze kukomeshwa,
Viongozi wa Mikoa, Wilaya na taasisi za Serikali zinazohusika na Kilimo na
Mazingira zinapaswa kushirikiana kuielimisha jamii kuacha uharibifu wa
mazingira, lakini pia kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wote wanaobainika
kuharibu wa mazingira.
Akiwa katika ziara hiyo, Makamu wa
Kwanza wa Rais alijionea ukuta uliojengwa na mwananchi mmoja katika eneo la
ufukwe wa bahari ya Mkokotoni kinyume cha sheria ukiwa juu ya bomba
linalopeleka maji katika kisiwa cha Tumbatu.
Kitendo hicho kimeelezwa na Viongozi wa
Mkoa wa Kaskazini Unguja na wataalamu wa mazingira kuwa kinaweza kuathiri
upatikakanji wa huduma ya maji kwa wakaazi wa kisiwa hicho cha Tumbatu, lakini
pia ni uharibifu mkubwa katika ufukwe huo.
Kutokana na hali hiyo, Maalim Seif
ameagiza ukuta huo uvunjwe kwa gharama za aliyeujenga, ili kuepusha uwezekano
wa wananchi kukosa huduma ya maji, pia kulindwa ufukwe huo na vitendo vya
uchimbaji mchanga na ukataji mikoko.
Maeneo mengine aliyoyatembelea ni eneo
la Kilimani, Mnazimmoja, Kisakasaka katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Pete na
Jambiani katika mkoa wa Kusini Unguja.
Maeneo hayo ni miongoni mwa 148 kote
Unguja na Pemba ambayo yamekumbwa
na athari kubwa kutokana na uvamizi wa maji ya bahari kulikosababishwa na
vitendo vya binaadamu kama vile, ukataji mikoko, uchimbaji mchanga, uvuvi
haramu, pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema ni
lazima sheria za kulinda na kuhifadhi mazingira zilizopo zitumiwe ipasavyo, pia
hali ya kuoneana muhali katika utekelezaji wa sheria ipigwe vita, ili kuinusu
ardhi ndogo ya Zanzibar isitowekwe kwa kuliwa na maji ya bahari.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa
Mazingira Zanzibar, Sheha Mjaja Juma, alieleza kuwa utafiti unahitajika
kufanywa katika maeneo hayo na yote yaliyoliwa na maji ya bahari, ili kuweza
kuchukuliwa hatua zinazofaa kitaalamu kuyalinda na kuyahifadhi.
Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amezitembelea familia pamoja na wenye
miradi ya vitegauchumi walioathiriwa na maafa ya upepo mkali ulioambatana na
mvua na radi, uliotokea juzi katika eneo la Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Miongoni mwa aliowatembelea ni pamoja na
familia ya Naliwe Mbarouk aliyefariki Dunia baada ya kupigwa na radi wakati wa
mkasa huo.
Aidha, kufuatia mkasa huo baadhi ya
wananchi wameumia na wengine kupata upofu, huku wengine makaazi yao yakiwa
yameharibiwa vibaya na upepo huo.
Aidha, alitembelea skuli ya Nungwi
ambayo imeathiriwa baada ya kuangukiwa na mti, pamoja na hoteli ya kitalii ya
Zulu, ambayo sehemu kubwa ya paa lake imeanguka na baadhi ya sehemu kuharibiwa
vibaya.
0 Comments