Na Kadama Malunde,Shinyanga
KUCHELEWA kutolewa kwa fedha za kujikimu kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wako katika mazoezi ya vitendo mkoani Shinyanga, kumesababisha
baadhi yao kugeuka ombaomba na wale wa kike kuwa hatarini kuuza miili yao .
Wanafunzi hao wamekosa a fedha za kulipia
kodi za nyumba wanazopanga na huduma zingine muhimu ikwemo chakula na matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga , Waziri wa Sheria na Katiba
wa serikali ya wanafunzi ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) cha Dar es Salaam,
Kasanzu Luganga,alisema tangu waanze mazoezi kwa vitendo miezi miwili iliyopita
hakuna fedha iliyotumwa na serikali na kusababisha kuishi katika mazingira
magumu.
Alisema kutokana na changamoto hiyo,
imesababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa na kukatisha mazoezi kwa vitendo
huku wengine wakigeuka ombaomba kwa watu, ili wapate fedha za chakula na
kujikimu.
“Katika mkoa wa Shinyanga kuna wanafunzi
kutoka vyuo vikuu saba ambavyo ni SAUT Mwanza,Tumaini Makumila cha
Iringa,Mtakatifu Stephano Moshi,Jodani cha Morogoro, Kampasi ya SAUT ya Tabora
na IFM,hivi vyote hakuna aliyelipwa fedha za kujikimu ambazo kila mwezi ni shilingi
620,000 na ziko kisheria lakini
tunasikitika serikali ndiyo inakuwa ya kwanza kuharibu,”alisema.
Aliwataja wanafunzi walioacha mazoezi na
kurudi makwao kuwa ni Simon Daniel aliyekuwa akifanya mazoezi wilayani Kahama (TRA), Alikana Elick aliyekuwa
akifanya mazoezi wilayani Bariadi na yeye
ambaye alikuwa akifanya mazoezi (NHIF) mjini Shinyanga.
Naye Gabriel Ndogani mwanafunzi wa mwaka
wa pili chuo cha IFM, aliiomba serikali kutoa kipaumbele kwa wanafunzi walioko vyuoni na kuondoa changamoto
zinazowakabili.
“Jambo la kujiuliza kama
fedha zilitengwa shilingi bilioni 6.6 za mafunzo sasa zimekwenda wapi? basi hata Wabunge wa
Bunge Maalumu la katiba serikali iwakope na wao wacheleweshewe malipo,maana
mara nyingi tunaoteseka ni sisi, tunafanya kazi kwa tabu na mazingira magumu
huku wao wakineemeka,” alisema.
0 Comments