Na Mwantanga Ame
MKE wa Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar,mama Asha Suleiman Iddi, amewataka wananchi kuwasaidia watu wenye
hali duni ili kuwawezesha kukabiliana na maisha yao.
Aliyasema hayo jana wakati
akikabidhi misaada ya vifaa mbali mbali zikiwemo nguo, vitu vya nyumbani,
vitabu vya wanafunzi, vitabu vya dini na vyakula na mafuta, kwa wakazi wa vijiji
vya Matemwe Mbuyu Tende, Kijini, Mvuleni na Mgonjoni.
Akizungumza kwa niaba ya mama
Asha, Katibu wa CCM mkoa wa kaskazini Unguja,
Ame Omar Mkadam, alisema Zanzibar bado kuna watu wanahitaji kupatiwa
misaada ili kubadili maisha yao.
Alisema Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani
Karume, katika uhai wake alipenda kuona maisha ya Wazanzibari yanakuwa katika
usawa na ndio maana aliwaachia usia wa kugawana kidogo kwa alienacho lakini
waenee.
Kutokana na falsafa hiyo,
alisema,ameamua kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo ili kufuata maneno ya
hekima kivitendo ya kiongozi huyo.
Alisema ni jambo ka kusikitisha
kuona baadhi ya watu wenye vipato wanashindwa kuwasaidia watu wenye mazingira
magumu jambo ambalo linaondoa utamaduni wa kusaidiana.
Aliwaahidi wanavijiji hao
kuendelea kushirikiana nao kwa kuwasaidia kila pale atakapoona upo umuhimu wa
kufanya hivyo kwa vile ni sehemu ya kuendeleza sera ya CCM.
Baadhi ya wana vijiji hao,
wakitoa shukrani zao, walimpongeza mama Asha kwa jitihada anazofanya kuwapatia
misaada ya kibinaadamu.
0 Comments