Na Benedict Liwenga, Maelezo
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la
Katiba, Samuel Sitta, amewahakikishia watu wenye ulemavu nchini kuwa
wanatendewa haki katika katiba mpya itakayopatikana.
Aliyasema hayo jana katika
mkutano wake na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), ambao walifika bungeni kwa lengo la kuwasilisha
hoja zenye msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika mchakato wa
katiba.
Alisema makundi yanayofika
bungeni, hayaendi na hoja mpya bali ni mawasiliano ya kawaida yanayohusu safari
kutoka rasimu ya katiba mpaka kufikia katiba mpya.
“Jambo lolote lililoandikwa na
binadamu halikosi kasoro, katika rasimu hii ya katiba tumegundua mapungufu
kadha,kuna baadhi ya maoni ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi
ili yawemo katika katiba mpya,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Inclusive Development Promoters and Consultants kutoka Dar es Salaam, Kaganzi Rutachwamagyo, ambaye
pia ni mwanachama wa shirikisho hilo,alisema kikosi cha ushauri kuhusu masuala
ya watu wenye ulemavu kimeweka kipaumbele cha msisitizo wao ambao unajielekeza
katika hoja za kuongeza masuala ya mambo ya Muungano.
Alisema hoja nyingine ya
msisitizo inahusiana na uanzishwaji wa chombo cha uratibu wa haki, usawa wa
fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye ulemavu.
Aligusia pia juu ya hoja
nyingine inayohusu suala la uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwenye Bunge,Baraza
la Wawakilishi na mabaraza ya Madiwani.
“Mathalani, tunapendekeza kifungu 113 kisomeke
kuwa asilimia 5 ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
watakuwa ni watu wenye ulemavu wakiwakilisha kundi hili na watapatikana kwa
kuchaguliwa na wahusika wenyewe,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya watu
wenye ulemavu, Amon Mpanjo, ambaye ni mjumbe wa bunge hilo alimuomba Mwenyekiti
wa bunge maalum kuunga mkono sio kupokea maoni mapya, bali kuyaboresha yale
yaliyokwisha wasilishwa hapo awali.
“Tukuombe Mwenyekiti
ulisisitizie bunge letu maalum la katiba liweze kuzingatia haki za watu wenye ulemavu
ili nao wapate kuwa na maisha bora,” alisema.
0 Comments