Na Mwandishi wetu
Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA)
kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu
Duniani (UNFPA) na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali, leo kitaadhimisha
siku ya mtoto wa kike duniani kwa kufanya mjadala mpana juu ya kukomesha ndoa
za utotoni nchini.
Mjadala huo utakaofanyika
hoteli ya CMG-Motel mjini Tarime mkoani Mara na kufuatiwa na kilele chake
tarehe kesho ni mwendelezo wa kampeni ya kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni
ijulikanayo kama “Ndoa za umri mdogo, Ukanda Huru” iliyozinduliwa mwaka huu
ikiwa na lengo la kuimarisha mienendo ya Taifa kwa ajili ya kuhakikisha
viongozi wanawajibika katika kukomesha ndoa hizo kwa kuweka mikakati ili
wasichana wapate haki zao.
Mwaka 2011, Baraza Kuu la Umoja
wa Mataia lilipitisha maadhimio ya kuanzisha siku ya mtoto wa kike duniani.
Siku hiyo imetengwa kwa ajili ya kuendeleza,kukuza haki na kutatua matatizo
yanayowakumba wasichana. Kauli mbiu mwaka huu ‘Kuwawezesha Wasichana: Kumaliza
Mduara wa Ukatili’ ambayo inatoa wito kwa wadau mbalimbali kutambua umuhimu wa
kuwekeza, kuwawezesha na kutokomeza aina zote za ukatili zinazowapata wasichana
ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni.
Ndoa za utotoni ni suala
linalohusu haki za binadamu; linakiuka haki za binadamu na kuzuia maendeleo kwa
wasichana na wanawake.
Aidha Tanzania pekee, wastani
wasichana wawili kati ya watano wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18
wakati katika bara la Afrika zaidi ya
asilimia 42 ya watoto wa kike wanaolewa
kabla ya kufikia umri huo huku mamilioni wakiolewa wakiwa bado hawajafikia umri
wa kubalehe.
Vile vile nchi 31 kati ya 41 duniani ambapo
mwenendo wa kuozesha watoto wa kike unakaribia asilimia 30 zimo Afrika.
Katika miaka ya nyuma na hivi
karibuni kumekuwa na ongezeko la mahitaji makubwa kwa serikali na mashirika
mbali mbali duniani kutaka kutatua tatizo la mimba za umri mdogo kama vile kutolewa kwa Mkataba wa Kutokomeza
aina zote za Ukatili dhidi ya Wanawake (CEDAW) na Itifaki ya Maputo ambayo
inakataza ndoa za utotoni.
Hivyo ahadi, maazimio na
mikataba hiyo inapaswa ifanyiwe kazi kwa vitendo ili kuleta mabadiliko ya kweli
katika maisha ya wasichana.
0 Comments