Na Asya Hassan
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania
(TASAF-3) upande wa Zanzibar umetumia shilingi 1,056,819,637 kuziwezesha kaya
masikini,ambapo shehia 40 za Unguja na Pemba zimefaidika na fedha hizo.
Kwa Unguja shilingi 401,477,884
zimetolewa kwa awamu sita kuanzia
Januari hadi Disemba na Pemba zimetolewa shilingi 655,341,753 kwa kwa awamu tano
kuanzia Januari hadi Septemba.
Akizungumza na gazeti hili ofisini
kwake Migombani, Mratibu wa mradi huo Unguja, Fatma Mohammed Juma, alisema kwa
upande wa Pemba mgao wa mwezi wa Disemba bado hawajaupata.
“Mpaka hivi sasa mpango huu wa
ruzuku ya kuziwezesha kaya masikini imeshatolewa kwa awamu sita ambapo Januari
zimetolewa shilingi 70.448 milioni,Machi 83.45 milioni,Mei 76 milioni,Julai 67.92
milioni , Septemba 78.11 milioni na Disemba shilingi 86.73 milioni,” alisema.
Alisema kwa upande wa Pemba Januari
ziligawiwa shilingi 123 milioni, Machi 136.272 milioni, Mei 136.34 milioni, Julai
123.4 milioni na Septemba 136 milioni na mwezi wa Disemba bado hatujapata idadi
yake,” alisema.
Alisema kaya 6,855 zinahusika
na mpango huo ambapo Unguja kuna kaya 2,674 na Pemba kaya 4,181.
Mratibu huyo alisema bajeti ya
malipo kwa awamu hizo ni shilingi 1,042,217,465 ambapo Unguja ni shilingi 489,669,633
na Pemba ni shilingi 552,547,832.
Alisema fedha hizo hutolewa kwa
mashariti maalum ikiwemo kuwasomesha watoto,kuwapeleka hospitali watoto pamoja
na mama wajawazito.
“Tokea kuwepo kwa mpango huu wa
kuziwezesha kaya masikini kwa kiasi fulani jamii imefanikiwa kwani wapo watoto
waliokuwa hawaendi skuli wamerudi skuli na wanaohitaji kwenda hospitali
wanapelekwa, kwa kweli mpango huu unasaidia kwa hatua kubwa katika kupunguza
umasikini kwa kaya hizi masikini,”alisema.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka
wananchi ambao wananufaika na mpango huo kuutumia kama inavyotakiwa ili kuweza
kujikwamua na ukali wa maisha.
1 Comments
fedha kama hii si ndio mwaka jana balozi Seif aliichota halafu akasema katumia kwa sherehe za mapinduzi? basi na hizo za pemba zifatiliwe haraka kabla sherehe za mapinduzi hazijafika.
ReplyDelete