6/recent/ticker-posts

Dk Shein afanya mazungumzo na mabalozi wa Ujerumani na Misri nchini

  

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

  Zanzibar                                                                               6.1.2015

---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa mwaliko wa Zanzibar kushiriki katika Tamasha la Kimataifa la Muziki wa Afrika nchini Ujerumani mwezi Juni mwaka huu ni njia moja wapo ya kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini humo pamoja na nchi nyengine za Ulaya.
 
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Egon Kochanke aliyefuatana na Dk. Stefan Oscman ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Tamasha la Afrika, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
 
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alisema kuwa mwaliko huo ni nafasi ya pekee kwa Zanzibar kuweza kujitangaza kiutalii pamoja na kiutamaduni kutokana na Zanzibar kujaaliwa katika sekta hizo ambazo zimeweza kuijingea sifa kubwa ndani na nje ya nchi.
 
Dk. Shein alisema kuwa Ujerumani na Zanzibar ni nchi zenye uhusiano wa kihistoria ambao uhusiano huo umeweza kuleta mashirikiano makubwa katika sekta mbali mbali na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni ya pekee kwa Zanzibar ambayo itaweza kusaidia katika mikakati yake ya kukuza uchumi na kuimarisha utamaduni.


 
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Ujerumani kwa kuithamini Zanzibar na kuipa mwaliko katika tamasha hilo sambamba na kushiriki kikamilifu kwa wasanii wa Zanzibar ambao wataonesha tamaduni za kizanzibari ikiwa ni pamoja na muziki wa taarab na sanaa nyenginezo.
 
Dk. Shein alisema kuwa hivi sasa Zanzibar imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka Ujerumani ambapo anamatumaini makubwa kuwa Tamasha hilo litaongeza idadi kubwa ya watalii kutoka nchi za Ulaya.
 
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imekuwa na vipaji kadhaa vya wasanii, hivyo anaimani kuwa wasanii hao watafanya vizuri katika Tamasha hilo la Kimataifa nchini humo.
 
Dk. Shein alisema kuwa mbali ya kuwa Ujerumani itashirikiana na Zanzibar katika tamasha hilo lakini hata hivyo, Zanzibar imekuwa na uhusiano na ushirikiano mwema kati yake na nchi hiyo hasa katika masuala ya mila na utamaduni, elimu na muziki.
 
Nae Dk. Stefan Oschman alimueleza Dk. Shein kuwa Tamasha hilo la 27 lina lengo la kuwaalika wanamuzi kutoka pembe zote za bara la Afrika ikiwemo Zanzibar ambayo tayari imeshashirikiana nayo katika masuala mbali mbali ya kisanii na filamu.
 
Alisema kuwa katika sherehe hiyo kutakuwa na nafasi maalum kwa Kamisheni ya Utalii Zanzibar kuelezea juu ya utalii wa Zanzibar pamoja na vivutio mbali mbali vilivyopo nchini jambo ambalo litapelekea kuwavutia watalii wengi kutoka Ulaya kuja Zanzibar.
 
Pamoja na hayo, Dk. Oschman alitoa mwaliko rasmi kwa Dk. Shein ili kushiriki katika Tamasha hilo na kueleza kuwa  Zanzibar itapata nafasi ya kuonesha utamaduni wake, maisha ya Mzanzibar, kazi zake za sanaa na vivutio mbali mbali vilivyomo ndani ya Zanzibar.
 
Aidha, Dk. Oschman alisema kuwa Tamasha hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu wapatao laki moja kutoka nchi mbali mbali za Duniani wakiwemo viongozi wa ngazi za juu kutoka nchi za Ulaya ikiwemo mwenyeji Ujerumani pamoja na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini humo.
 
Katika mazungumzo yake hayo Dk. Oschman alisema kuwa tayari ujumbe huo umeshakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa juu wa Wizara husika pamoja na wasanii mbali mbali ambao wanatarajia kushiriki katika tamasha hilo.
 
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Hossam Moharam Ikulu mjini Zanzibar ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao walisisitiza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo.
 
Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano kati yake na misri hasa katika uimarishaji wa sekta ya elimu, utamaduni pamoja na sekta nyengine za uimarishaji wa uchumi.
 
Nae Balozi Moharam alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Misri itaendelea kutoa ushirikiano wake na kukuza uhusiano sambamba na kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kukuza uchumi na kuimarisha sekta zake za maendeleo kutokana na mafanikio yaliopatikana chini ya uongozi wa Dk. Shein.
 
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Post a Comment

0 Comments